ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 4, 2012

YANGA YAALIKWA RWANDA


Kikosi cha Young Africans Sports Club
Mabingwa wa soka wa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) na vinara wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga
Mabingwa wa soka wa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) na vinara wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga wamealikwa jijini Kigali, Rwanda kushiriki mashindano maalum yatakayofanyika nchini humo kuanzia Desemba 16.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mratibu wa Mashindano hayo (RPF Cup) na kiongozi wa Chama cha Soka cha Rwanda (FERWAFA), Richard Gezahure, alizitaja timu nyingine zilizoalikwa kutoka nje ya nchi yao kuwa ni pamoja na Vital'O ya Burundi na SC Villa ya Uganda.
"Hata hivyo, bado Villa inatuchanganya kwa sababu timu hiyo imegawanyika… kuna Villa Halisi ambayo kwa sasa haitambuliwi na FUFA (Chama cha Soka cha Uganda) na Villa nyingine inayoshiriki Ligi Kuu ya Uganda," alisema kiongozi huyo.
Aliongeza kwamba FERWAFA iko katika hatua za mwisho za maandalizi ya mashindano hayo na italipia gharama za usafiri na malazi kwa klabu zote zilizoalikwa kushiriki michuano hiyo.
Alisema kwamba mashindano hayo ni maalum na, ni mwanzo wa kuandaa ligi itakayokuwa inashirikisha timu sita za Afrika Mashariki.
Hii itakuwa ni mara ya pili kwa Yanga kwenda Kigali mwaka huu kwani kabla ya msimu wa ligi kuanza Septemba 15, ilikwenda nchini humo kuweka kambi ya wiki moja na kucheza mechi mbili za kirafiki.
Yanga imejizolea mashabiki wengi Rwanda baada ya kuwasajili nyota wawili waliokuwa klabu ya APR, Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite.
Vinara hao wa ligi kuu Bara pia wanatarajia kwenda Uturuki baadaye mwaka huu kuweka kambi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao ya mzunguko wa pili wa ligi kuu utakaoanza mwezi ujao.

Hata hivyo, hakuna kiongozi wa Yanga aliyepatikana jana jioni kuzungumzia mwaliko huo kutoka Rwanda.

No comments: