ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 22, 2013

Ally Remtullah kuipeperusha Afrika Mashariki katika mkutano wa ‘The Economics of the Africa Fashion Industry’

Meneja Masoko wa Kampuni ya Tanzania Hair Industry ltd James Walwa - Jimmy akimkabidhi mbunifu wa mavazi nchini Ally Rehmtullah tiketi kwa ajili ya kwenda kuiwakilisha Afrika Mashariki katika mkutano wa 'The Economics of the Africa Fashion Industry' utakaofanyika nchini Marekani mwezi wa Februari. Tanzania Hair Industry ltd ambao ndio watengenezaji wa nywele maarufu aina ya Darling ndio wadhamini wa safari ya mbunifu huyu kwenye mkutano huo wa kihistoria utakaofanyika katika Kikuu cha Havard nchini Marekani.

Mbunifu mahiri wa mavazi nchini Tanzania Ally Remtullah amechaguliwa kuiwakilisha Africa Mashariki katika ‘East Africa Fashion Industry’ kuongea katika mkusanyiko wa Afrika Business Conference utakaofanyika Harvard Business School nchini Marekani.
Akizungumza na Mo Blog jijini Dar es Salaam leo, Mbunifu huyo Remtullah amesema shughuli hiyo itakayofanyika katika Chuo Kikuu cha Marekani cha Harvard ambacho ni kikubwa kuliko vyote duniani itafanyika Februari tarehe 15 mwaka 2013.
Akifafanua amesema kuwa kila mwaka Chuoni hapo kunafanyika mikutano ya ‘Africa Business Conference’ ikiwa na kauli mbiu tofauti na sasa mwaka huu yeye amechaguliwa kuwa mmoja wa wazungumzaji kuhusiana na ‘The Economic of Africa Fashion’.
Ally Remtullah amesema kwa ujumla anaiwakilisha Afrika Mashariki katika kategori hiyo ambapo anatarajiwa kuzungumzia changamoto zinazoikabili na fursa zinazopatikana katika tasnia ya fasheni Afrika Mashariki, ikiwemo tatizo la umeme na gharama za manunuzi ya vitambaa vya Pamba ambayo kimsingi huzalisha katika ukanda huu.
Amesema anafurahi kuchaguliwa na wandaaji hao kuziwakilisha nchi za Afrika Mashariki na sasa si kwenda tena kuonyesha mavazi, bali ni kuzungumza mbele ya wadau wakubwa wa kidunia kuhusu nafasi ya masuala ya ubunifu na uchumi.
Wazungumzaji wengine katika mkutano huo ni pamoja na mbunifu maarufu wa Afrika Magharibi Ituen Basi kutoka Nigeria.
Katika maandalizi hayo Ally amesema pamoja na kusoma vitu vingi kuhusiana na uchumi katika tasnia ya fasheni na gharama za uzalishaji za viwanda vya nguo, pia amekutana na wafanyabiashara wakubwa wa viwanda vya kutengeneza nguo hasa za kiafrika akiwemo Mfanyabiashara Mkubwa nchini Mh. Mohammed Dewji ambaye kwa namna moja ama nyingine amempa ushirikiano wa kutosha.
Safari hiyo ya mbunifu wa mavazi nchini Ally Remtullah katika mkutano mkubwa wa kihistoria wa Boston nchini Marekani, imedhaminiwa na kampuni ya Tanzania Hair Industry Ltd, ambao ni wazalishaji wa nywele maafuru aina ya Darling.

No comments: