ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 17, 2013

Jeuri ya kuichezea serikali hii hapa.


Jeuri ya fedha ya Meli Mt. Al Biraq iliyoingia nchini mafuta ya ovyo ya dizeli ambayo hayana viwango vya ubora ya kutaka kuyauza nchini kwa lazima licha ya kukataliwa na Shirika la Taifa la Viwango (TBS), imekwama na sasa imepewa saa 24 kuondoka nchini na shehena yake.

Kwa jeuri ya kiwango cha juu, meli hiyo yenye namba za usajili IMO 9381732, iliwasili nchini Desemba 27, mwaka jana ikiwa na shehena ya tani 100,010 ya dizeli, lakini ikagundika kuwa mafuta hayo hayana ubora na kutakiwa kurejea nayo yalikotoka.
Siku tisa baadaye yaani Januari 5, mwaka huu ilirejea nchini ikiwa na shehena ile ile kwa nia ya kudanganya mamlaka za Tanzania ili kuruhusiwa kuuza mafuta katika soko la Tanzania.

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, alisema kuwa Januari 15, mwaka huu meli hiyo baada ya kuingiza mafuta hayo yalipimwa na TBS na kukuta matatizo yale yale na hivyo kuagiza yasiingizwe nchini kutokana na kuwa chini ya viwango vya ubora.

Dk. Mwakyembe alisema serikali imelazimika kuchukua hatua hiyo kwa sababu ni mara ya pili kwa meli hiyo kuingiza mafuta yasiyo na viwango.

“Nimeamua kutumia mamlaka niliyopewa chini ya Sheria ya Bandari ya mwaka 2004, kifungu cha 57 (2) kuiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kuhakikisha kuwa meli hiyo inaondoka eneo la Tanzania ndani ya saa 24 kuanzia leo (jana) jioni,” alisema Dk. Mwakyembe.

Alisema mbali na kuamuru meli hiyo kuondoka nchini, pia atatumia mamlaka aliyopewa kisheria chini ya kifungu cha sheria 57 (3) kuizuia na kuwafungulia mashataka ya jinai watu wote wanaohusika nayo pamoja na shehena ya mafuta iliyoingizwa.

Alisema mwaka jana meli hiyo iliingiza mafuta kiasi hicho ambayo baada ya kupimwa na TBS ilizuiliwa kushusha shehena hiyo kwa sababu ya kushindwa kukidhi viwango stahili vya ubora.


Waziri huyo aliongeza kuwa serikali imebaini kuwa baada ya kukataliwa na TBS kushusha shehena hiyo ya mafuta, meli hiyo iliondoka katika Bandari ya Dar es Salaam kwa muda, lakini siku tisa zilipopita ikarejea tena nchini ikiwa na shehena ya mafuta ya awali kwa kudai kuwa ni mafuta mapya.

“Januari 15, mwaka huu TBS waliipima upya shehena hiyo ya mafuta na kukuta ina matatizo yale yale na kuagiza tena kuwa shehena hiyo isiingizwe nchini kutokana na kuwa chini ya viwango vya ubora,” alisema Dk. Mwakyembe.

Dk. Mwakyembe aliipongeza TBS kwa kuonyesha uadilifu, uzalendo na weledi wa hali ya juu kwa kutokubali kuyumbishwa na wafanyabiashara wasiotaka kuheshimu sheria za nchi kwa lengo la kujipatia faida iwe halali au haramu.

Waziri huyo aliongeza kuwa serikali baada ya kubaini kuwa kuna dalili zote zinazoonyesha kuwa meli hiyo itaendelea kuzengeazengea maeneo ya bandari kwa nia chafu ya kupenyeza mnafuta hayo duni kwenye soko la Tanzani hivyo ameamua kuifukuza nchini.
CHANZO: NIPASHE

No comments: