ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 17, 2013

Mchina akamatwa na Takukuru akitoa rushwa kwa DC Bunda


mkuu wa wilaya ya Bunda, Joshua Mirumbe
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, imemkamata raia wa China, kwa tuhuma za kutoa rushwa ya Sh. 500,000 kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, ili kampuni yake iruhusiwe kusambaza pembejeo kwa wakulima wilayani humo.

Raia huyo wa China, Mark Wang Wei, ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Panda International Co. Limited ya mkoani Shinyanga, ambaye alikamatwa jana mchana katika ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo, Joshua Mirumbe, baada ya kumuwekea mtego huo wa Takukuru.

Mirumbe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, alisema Mchina huyo kupitia kampuni yake, ambayo ni ya usambazaji wa pembejeo, juzi alimwandikia ujumbe wa simu ya mkononi (sms) akimshukuru sana, huku akiahidi kumuona jana ofisini kwake ili ampe zawadi.
Alisema baada ya kuahidiwa na Mchina huyo, hali hiyo ilimtia shaka kwani hakuwa na ahadi yoyote kutoka kwake.

Kutokana na hilo, alisema aliamua kuwaarifu Takukuru, ambao waliweka mtego ofisini kwa mkuu huyo wa wilaya.

“Baada ya kuahidiwa na Mchina huyo kwa kweli hali hiyo ilinistua sana na kunitia shaka, maana mimi binafsi sikuwa na ahadi yoyote na Mchina huyo. Sasa nilichokifanya nilimtaarifu Kamanda wa PCCB (Takukuru) na ndipo tukaweka mtego uliofanikiwa kumtia mbaroni,” alisema.

Alisema Mchina huyo alifika jana mchana na kuingia ofisini kwake na kumpa barua kutoka Idara ya Uhamiaji ikimtambulisha kuwa ana kibali cha kuishi hapa nchini hadi Machi, mwaka huu.

Mirumbe alisema Mchina huyo pia alitoa Sh. 500,000 na kumpa, huku akisema kuwa hiyo ni zawadi yake, ili airuhusu kampuni yake iweze kusambaza pembejeo kwa wakulima wilayani hapa.

Alisema suala la usambazaji wa pembejeo linatakiwa kusimamiwa na mtu makini, kwani msimu uliopita mawakala waliopewa jukumu hilo walichakachua pembejeo hizo na kusababisha wakulima kutozipata kwa muda muafaka na wengine kuzikosa kabisa.

Mirumbe alisema kufuatia hali hiyo, baadhi ya watendaji wa hamashauri hiyo walioshirikiana na mawakala hao wamesimamishwa kazi na wengine wameshitakiwa mahakamani, huku baadhi yao wakitorokea kusikojulikana.

Alisema hali hiyo ndiyo iliyowasukuma kuwa makini katika suala la kupitisha mawakala wa kusambaza pembejeo wilayani hapa na kubaini kuwa Mchina huyo alikuwa na kibali cha kumruhusu kukaa hapa nchini, ambacho muda wake ulikuwa umebakia wa siku 10 tu.

Mirumbe alisema walichukua hatua ya kumtaka Mchina huyo, kupeleka vitambulisho vyake kutoka Uhamiaji na sehemu zote zinazohusika.

Ilielezwa kuwa baada ya kutoa fedha hizo Takukuru walimkamata na fedha hizo kuhesabiwa mbele ya mashahidi ofisini humo.

Hadi jana jioni alikuwa akiendelea kuhojiwa na Takukuru, ambao walisema kuwa baada ya maelezo yake watamfikisha mahakamani.

Akihojiwa na waandishi wa habari, Mchina huyo alikiri kutoa fedha hizo, huku akisema alimpa mkuu huyo wa wilaya kama zawadi yake na kwamba, hakukusudia kutoa rushwa.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: