Advertisements

Tuesday, January 22, 2013

JIKINGE NA UGONJWA HATARI WA MAWE KWENYE FIGO KWA CHAKULA


UGONJWA wa mawe kwenye figo ni miongoni mwa magonjwa yanayowapata na kuwasumbua watu wengi hivi sasa. Hata hivyo, kudhani kwamba wewe huwezi kupatwa na ugonjwa huo bila kuchukua tahadhari mapema nisawa na dereva kudhani gari lake haliwezi kuishiwa mafuta wakati hajaenda kwenye kituo cha mafuta kuweka.

Kama kweli unahitaji kujiepusha na ugonjwa huu ambao tiba yake mara nyingi huwa ni operesheni, ni vizuri ukaanza kuchukua tahadhari mapema ya kujikinga kwa kula vyakula ambavyo vitakusaidia kuzidumisha na kuziweka figo zako katika hali ya usalama na usafi daima. Zifuatazo ni dondoo muhimu za vitu vya kula ambavyo hutoa kinga hiyo:

JUISI HALISI NA MATUNDA
Figo husaidiana na kibofu katika usagaji wa chakula na uondoaji wa sumu mwilini. Lakini kiungo kimoja kati ya hivi viwili kikijaa uchafu kwa sababu ya lishe duni au kula vyakula vyenye sumu, vitu mfano wa vimawe vidogo hujitengeneza kwenye figo, na vikifikia hatua hii, huwa vigumu kuyeyuka na huwa ndiyo mwanzo wa matatizo ya kiafya.
Hata hivyo, tatizo hili linaweza lisikupate ukiwa na tabia ya kunywa juisi halisi za matunda (ya kutengeneza nyumbani, siyo viwandani) pamoja na mboga za majani kila siku, kwani juisi na mboga za majani huondoa mrundikano wa uchafu na sumu katika kibofu na figo hivyo kuuacha mwili wako salama.
Miongoni mwa matunda yenye uwezo mkubwa wa kutoa kinga na hata nafuu kwa mgonjwa wa mawe kwenye figo ni pamoja na ‘epo’ (apple), ambalo lina kirutubisho aina ya ‘pectin’ ambacho kina uwezo wa kulainisha na kuyeyusha mawe na kuzuia mengine kujitengeneza kwenye figo. Pia juisi za limau, machungwa (jamii zote), nyanya pamoja na ‘beet root’ hutoa kinga imara dhidi ya ugonjwa huu hatari.

MAFUTA MAZURI
Ingawa wataalamu wengine huwashauri wagonjwa wa mawe kwenye figo kujiepusha na ulaji wa mafuta kabisa, hasa wale waliofanyiwa operesheni ya kuondolewa mawe, lakini kuna baadhi ya mafuta ni muhimu katika kuondoa mawe yaliyopo na kuzuia kutokea kwa mengine kwenye figo.
Kwa mafano, mafuta ya mzeituni (Olive Oil) hutumika mara nyingi katika tiba mbadala ya kusaidia usafishaji na uondoaji wa mawe kwenye figo. Vilevile mafuta ya nazi na hata mafuta ya wanyama wanaofugwa katika mazingira asilia ya kula majani porini, yanahusika katika afya ya kibofu na figo kwa kuziepusha sehemu hizo kupatwa na mawe.
Epuka kutumia mafuta yatokanayo na Soya ambayo yanaelezwa ni miongoni mwa mafuta yanayosabibisha magojwa ya uvimbe na kolestrol mbaya mwilini na mafuta mengine ya mimea ambayo yamesafishwa kiwandani na kuondolewa virutubisho vyake vyote vya asili.

BIZARI
Bizari au manjano, kama inavyojulikana na wengine, ni miongoni mwa viungo vya mboga ambavyo huzuia utengenezaji wa mawe kwenye figo. Pendelea kutumia bizari kwenye mboga kwani utafiti unaonesha kuwa kiungo hiki, ambacho kina kiwango kingi cha madini ya kashiamu, kina uwezo mkubwa wa kutoa kinga na kuzuia magonjwa ya uvimbe, likiwemo la utokeaji wa mawe kwenye figo. Pia husadia sana usagaji wa chakula tumboni.
Mwisho, wakati ukizingatia ulaji wa vyakula vilivyotajwa hapo juu katika kutoa kinga au kupambana na mawe kwenye figo, jiepushe na ulaji wa sukari nyingi na ulaji wa vyakula vya kusindika, kwani hivyo ndivyo huchangia kwa kiasi kikubwa matatizo haya. Kumbuka kinga ni bora kuliko tiba, chukua tahadhari mapema kabla ya hatari.

Chanzo: GPL

No comments: