MPENZI msomaji, naendelea kuelezea ‘topiki’ inayoelezea namna mapenzi yanavyokuwa imara yakijengwa. Tuwe pamoja hadi nitakapoishia.
Mwenzi wako atakuheshimu mno kama nawe unamuonesha utiifu. Hata wasaliti wengi, wamejikuta wakisalitiwa baada ya kuwaonesha wenzi wao jinsi wasivyo waaminifu.
Onesha utu ili uendelee kufaidi upendo na huduma. Mwenzi wako amekuwa akitumia fedha nyingi kukuhudumia, jambo unalodaiwa kwake ni utu.
Hakikisha unampa faraja mpaka hajutii kile anachokitoa kwake. Faraja siyo mapenzi ya kitandani peke yake.
Unapaswa kutuliza akili na ujue mwenzi wako anahitaji nini kutoka kwako. Ukishakifahamu, ni juhudi yako kuhakikisha hakikosi. Kufanya hivyo ndiyo utu na ndivyo utakavyoweza kumteka zaidi na zaidi. Atakapokuwa anakutendea lakini maombi yake huyapokei vizuri, unakuwa unamkatisha tamaa.
Kadiri unavyomkatisha tamaa ndivyo unavyoelekea kumvunja moyo. Tambua kwamba moyo unapovunjika inakuwa ni ngumu mno kuurejesha kwenye hali yake ya kawaida. Kwa maana hiyo unakuwa umepoteza upendo na huduma zote ulizokuwa unazipata kutoka kwake.
Mapenzi ni mchezo wa nipe nikupe. Nipe upendo na wewe nikupende. Inawezekana yeye ndiye alianza kukupenda ndiyo maana akafanya juu chini mpaka mkawa pamoja. Baada ya hatua hiyo ni muhimu kwako kuhakikisha unaonesha upendo kwa sababu mmekubaliana kupendana.
Kupenda siyo maigizo, kusema utamfanyia magirini mwenzi wako ili utimize matakwa yako fulani. Kila aliyeingia kwenye uhusiano kwa malengo tofauti na upendo alifeli. Unaposoma makala haya, ikupe njia nzuri ya kutimiza wajibu wako kwenye mapenzi halafu umuache naye atimize kwa upande wake.
Unapokuwa unatimiza wajibu wako, hebu jiulize naye anafanya nini? Ni hatari sana kuendelea kuonesha unampenda na kumjali, wakati yeye hakujali kwa chochote. Mapenzi siyo tu kwamba yapo, ila yamekuwepo kwa ajili ya kupeana faraja.
Kama mwenzi wako hakufariji maana yake unatakiwa uhame hapo ulipo. Jinsi utakavyokuwa unazidisha upendo, haitakusaidia, kwani ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa. Badala ya kukushukuru, yeye atakuona zezeta uliyekufa kwake. Unatakiwa kuutetea moyo wako.
Naomba nikushauri kuwa akili yako iwe hai kila siku. Uwekezaji wako uendane na kile ambacho wewe unakipokea kutoka kwa mwenzi wako. Kufanya zaidi au pungufu ni kosa kubwa. Kufanya zaidi maana yake unakuwa unaunyanyasa moyo wako na pungufu unakuwa humtendei haki mwenzio.
Labda nisisitizie kitu. Sina maana kwamba kama wewe unatoa fedha ni sharti naye awe anakupa, la hasha! Uhusiano bora wa mapenzi huboreshwa na namna ambavyo wahusika wanavyohudumiana. Kila mmoja kuhakikisha anakuwa jirani na mwenzake wakati wote.
Mmoja anaweza kuwa na matatizo ya kipato, ni vizuri sasa mwenzake kuwa naye karibu kuhakikisha changamoto hiyo inakwisha. Ni ajabu pale mtu anapokabiliana na hali ngumu ya muda mfupi na anahitaji tu faraja kutoka kwa mwenzi wake lakini akawa hapati.
Hizo ndiyo dalili za unyonyaji. Kama wewe matatizo yako ya kifedha unayaweka mstari wa mbele na unatatuliwa, iweje mwenzako umeshindwa kumfariji wakati wa shida zake? Hiki ni kipengele kibaya ambacho kimewafelisha wengi. Baadhi wamepoteza wapenzi bora kwenye maisha yao.
KUNA MFANO KHALID NA GIFT
Khalid akiwa na upendo wa dhati kwa Gift, alimtabiria mema na kumtegemea kwamba ndiye atakuwa mke wake wa ndoa. Walipokuwa wanaanza uhusiano, Gift alikuwa amemaliza kidato cha sita Shule ya Sekondari Mwanza, wakati huo, Khalid alikuwa ni mfanyabiashara wa mitumba, Soko la Mlango Mmoja (Langolango), Mwanza.
Walifahamiana kwenye daladala, siku ambayo Khalid alimkuta Gift akiwa kwenye muonekano wa kukata tamaa ya maisha. Alikuwa amepata alama ambazo asingeweza kuendelea na chuo kwa udhamini wa serikali. Hilo lilimkatisha tamaa, ndoto zake za kuwa daktari bingwa wa kike aliona zimefika ukingoni.
Hata mwanzoni Khalid alipojitahidi kuzungumza na Gift amueleze tatizo lake, alimdharau. Alimuona wa kawaida, asingeweza kumpa msaada wowote. Kwa maana hiyo alimdharau lakini Khalid aliongeza juhudi kujua kilichopo ndani ya mrembo huyo.
Baada ya mzunguko wa muda mrefu, ikabidi Khalid aombe japo mawasiliano. Wakabadilishana namba za simu. Tangu siku hiyo, Khalid aliendelea kumfikiria sana Gift, aliwaza vitu vingi. Kubwa zaidi alihisi kuna kitu kikubwa kipo ndani yake, alijihisi kumpenda mrembo huyo.
Kingine kilichomsumbua Khalid ni hali ya Gift, alihisi kuna tatizo kubwa ndani yake. Siku moja akamtafuta kwenye simu, alipompata alimuomba wakutane, akamkatalia. Akaendelea kumjaribu mara kwa mara, akawa anagonga ukuta lakini baada ya wiki mbili, Gift alikubali kukutana na Khalid.
Walikutana kwa mara ya kwanza Ilemela, Tunza Beach, wakazungumza mengi, wakaweza kufahamiana. Gift akatambua kwamba Khalid ni mfanyabiashara wa mitumba, vilevile Khalid akaelewa nini hasa kinachomtesa Gift. Khalid akaamua kulibeba tatizo la Gift kama lake.
Itaendelea wiki ijayo.
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment