Wachezaji wa Yanga wakijifua kwenye Uwanja wa Bora uliopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam jana asubuhi kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Yanzania Bara. Uwanja huu uliojaa vipara na kokoto |
Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), na ambao waliondoka kwa kishindo kuelekea Uturuki kujiandaa kwa kambo yao ya wiki mbili iliyoambatana na ‘maraha ya aina yake, walitua Jumapili iliyopita na juzi walianza mazoezi yao ya kawaida kwenye uwanja wa ‘uswazi’ wa Bora uliopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Kabla ya kuanza kwa mazoezi yao kwenye uwanja huo ambayo jana yaliingia katika siku ya pili tangu warejee kutoka Ulaya, NIPASHE ilishuhudia wachezaji wakiingia uwanjani wakitokea makwao na siyo hotelini tena kama ilivyokuwa kwenye kambi yao ya Uturuki.
Kabla ya kuanza mazoezi yao jana yaliyowachukua takriban saa 2, wakianzia mishale ya saa 2:00 hadi saa 4:00 asubuhi, wachezaji walionekana wakiwasili kivyao uwanjani hapo.
Mwandishi aliwashuhudia wachache kati yao wakiingia na magari binafsi wanayoendesha wenyewe. Hawa baadhi yao walikuwa ni pamoja na Haruna Niyonzima ‘Fabregas’, Kelvin Yondani, Nurdin Bakari na pia kocha wao Mholanzi, Ernst Brandts.
Wachezaji wengine waliwasili uwanjani kwa miguu kuashiria kwamba walitumia daladala, wengine kwa taxi za kawaida na ‘taxi’ bubu, wengine ‘bodaboda’ na baadhi yao kwa basi dogo jeupe aina ya Toyota Coaster lililodaiwa kutolewa na uongozi kwa ajili yao.
Wakiwa uwanjani, mwandishi aliwashuhudia wachezaji wakijitahidi kuzingatia maelekezo ya kocha kadri walivyoweza, huku wakionekana kujituma mwanzo – mwisho.
Hata hivyo, wapo baadhi walioonekana kusumbuliwa na hali ya uwanja huo ambao ni vigumu kuamini kuwa unatumiwa na klabu kubwa kama ya Yanga kujiandaa kwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Kwenye mahala pa kuchezea palionekana kutofautiana mno na wachezaji wenye hadhi ya juu wa klabu hiyo pamoja na kocha wao Brandts. Kamwe hakukaribiani na viwanja vizuri walivyoenda kujifua kwa wiki mbili Uturuki.
Baadhi ya maeneo yaliyobahatika kuwa na majani; nyasi zake zilionekana kutofautiana sana. Nyingine zilikuwa ndefu zaidi kiasi cha miguu kuzama na baadhi zilikuwa fupi kwa kiwango cha kawaida.
Hata hivyo, maeneo makubwa ya uwanja huo wa Bora yamejaa ‘vipara’ na kokoto.
Baadhi ya wachezaji waliozungumza na gazeti hili baada ya kumalizika mazoezi hayo yaliyosimamiwa kwa pamoja na Brandts na msaidizi wake, Fred Felix Minziro, walikiri kusumbuliwa na hali ya uwanja huo.
Baadhi walisema tofauti kubwa kati ya viwanja walivyokuwa wakivitumia kwa wiki mbili nchini Uturuki na huo wa Bora imewaongezea ugumu kwani sasa wanalazimika kufanya kazi ya ziada kuepuka majeraha yatokanayo na ama kokoto zilizojaa uwanjani hapo au kuchunwa na ‘chaka’ la nyasi katika baadhi ya maeneo.
“Kuna tofauti kubwa sana kati ya viwanja vya wenzetu (Ulaya) na hivi vya kwetu. Katika uwanja huu (Bora) inafikia wakati unashindwa kufanya baadhi ya vitu kwa kuhofia kuumia,” alisema mmoja wa wachezaji wa ‘Wanajangwani’.
“Kwa mfano, kabla hatujasafiri kwenda Uturuki, Kavumbagu aliumia vibaya mguu wake baada ya kujikita kwenye kokoto za uwanja huu huu. Sasa tumerudishwa tena kufanya mazoezi hapa… tuna kazi kubwa ya kufika mbali kwakweli,” aliongeza mchezaji mwingine aliyezungumza klwa sharti la kutotajwa gazetini.
Tofauti na ilivyokuwa wakiwa Uturuki ambako mabingwa hao wa soka Afrika Mashiriki na Kati (Kombe la Kagame) walifaidi ‘maraha’ ya Ulaya kwa kusafiri kwenye barabara za ‘juu na chini’, wachezaji wa Yanga waliondoka kwenye uwanja huo wa Bora kila mtu kivyake kama ilivyokuwa wakati wakiwasili.
Klabu hiyo iliyoanzishwa 1935, inakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na uwanja salama wa mazoezi.
Kwa kawaida, wasipofanya mazoezi kwenye Uwanja wa Bora, Yanga hukimbilia kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola, Mabibo jijini Dar es Salaam ambao pia umejaa vipara na tofauti yake kwa ubora na Uturuki ni kama mbingu na ardhi.
Cha kusikitisha, uwanja wa Yanga wa Kaunda uliopo katika mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam ndiyo una hali mbaya zaidi kiasi cha wao wenyewe kuukimbia. Miezi miwili iliyopita uongozi wa klabu hiyo uliingia mkataba na kampuni ya Beijing Construction kutoka China, iliyojenga Uwanja wa Taifa wa jijini Dar es Salaam ili iwajengee uwanja wa kisasa, ujenzi ambao wanadai utakamilika 2017.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment