Aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha netiboli nchini
Anna Kibira
|
NA RENATHA MSUNGU
Aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha netiboli nchini (CHANETA), Anna Kibira amejitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya mwenyekiti katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Machi 23 mkoani Dodoma.Kibira ambaye Agosti 31, 2009 alisimamishwa kwa muda usiofahamika na Kamati ya Utendaji ya CHANETA kwa madai ya kukiuka taratibu, amekuwa nje ya madaraka tangu wakati huo licha ya suala lake kufanyiwa kazi na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ambalo liliamua kuwa yuko huru kugombea katika uchaguzi mkuu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kibira alisema fomu ya nafasi hiyo anakwenda kuichukua leo saa tano asubuhi, na atairejesha mara moja.
Alisema ameamua kujitosa kuwania nafasi ya juu ya uongozi kwa kuwa ana uwezo na uzoefu wa kutosha katika mchezo huo na ana imani kwamba kwa kushirikiana na viongozi wengine wa mikoa watauendeleza mchezo wa netiboli nchini.
Kibira aliongeza kuwa endapo atapewa ridhaa ya kukiongoza chama hicho, atatoa nafasi ya kushirikiana na viongozi wa michezo kutoka mikoa yote ambayo ni wanachama wa CHANETA ili kuhakikisha mchezo wa netiboli unainuka nchini.
Naye kaimu katibu mkuu wa CHANETA, Rose Mkisi alisema mpaka sasa ni wagombea watano wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi za uongozi katika uchaguzi huo.
Aliwataja wagombea waliojitokeza awali kuwa ni Rose Kisiwa anayewania nafasi ya makamu mwenyekiti, wakati nafasi ya ujumbe waliochukua fomu ni Sara Mbwana, Mary Protasi, Mwajuma Kisengo na Yasinta Silvester.
Mkisi aliwataka watu zaidi wajitokeze kuchukua fomu za kugombea. Usaili kwa ajili ya uchaguzi huo utafanyika Machi 21.
No comments:
Post a Comment