ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 17, 2013

Bungeni kwachafuka tena

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi (kulia) akizungumza na wabunge wa Chadema baada ya kikao cha kunge kualishwa jana mchana. Picha na Edwin Mjwahuzi.

Dodoma.Wabunge watano wa Chadema jana walitimuliwa bungeni na kuamriwa kukaa nje ya Bunge kwa siku tano kutokana na vurugu zilizotokea jana usiku.Wabunge hao ni Lissu, Hezekiah Wenje (Nyamagana), Highness Kiwia (Ilemela), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) Godbless Lema (Arusha Mjini) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini).
Chanzo za kufukuzwa kwao ni kuwazuia askari wa Bunge kumtoa nje Lissu ambaye alikuwa ameamriwa kutoka nje na Naibu Spika, Job Ndugai baada ya kuingilia hotuba ya Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba.
Kutokana na tafrani hiyo, Nchemba hakuweza kuhitimisha hotuba yake hivyo Ndugai alilazimika kukatisha mkutano wa Bunge.Hata hivyo wakati akiahirisha mkutano huo, tayari wabunge hao walikuwa wameshatolewa nje baada ya askari kuongezwa.
Mapema Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba alitoa tusi zito la nguoni wakati wa hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, licha ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kupiga mkwara wa kuwashughulikia wabunge watakaorusha matusi.
Mbali na tukio hilo Lema naye alichafua hali ya hewa baada ya kuwatuhumu viongozi wa CCM akiwamo Rais Jakaya Kikwete kwa udini, madai ambayo Bunge limempa siku saba kuyathibitisha.
Lema aliituhumu CCM na Serikali yake chini ya Rais Kikwete kwa kushindwa kutatua mgogoro wa kidini na badala yake kuwa kama analikwepa tatizo. Alionya kuwa Taifa linapasuka kwa migogoro kutokana na viongozi wa Serikali kushindwa kulishughulikia.
Kauli iliwanyanyua vitini Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Uratibu na Sera), William Lukuvi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Lukuvi na Jaji Werema walisimama wakidai kuwa Lema alikuwa amemdhihaki Rais Kikwete kwa kauli zake za kumhusisha na masuala ya udini.
Hata hivyo, Mnadhimu Mkuu wa Upinzani, Lissu alisimama kumtetea Lema akidai hakuwa amemdhihaki Rais bali alikuwa amemkosoa kitu ambacho kanuni za Bunge zinaruhusu.
Lema aliruhusiwa kuendelea na hoja yake na ndipo akamtolea mfano Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira wakati alipokwenda Mwanza kutatua mgogoro baina ya Wakristo na Waislamu kuhusu suala la kuchinja.
“Wassira akifahamu yeye ndiye, Waziri alikwenda Mwanza na kuwaacha viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu watatue wenyewe suala la kuchinja. Sasa alitaka diwani atatue mgogoro ule?”
Baada ya kumaliza kuchangia, Naibu Spika alitangaza kuwa Lema anatakiwa kuwasilisha katika muda wa siku saba uthibitisho kuwa Rais anahusika na tatizo la udini.
Serukamba alipewa nafasi ya kutoa taarifa wakati wabunge walipokuwa wakilumbana juu ya uhalali wa Msemaji wa Upinzani, Profesa Kulikoyela Kahigi kuzungumzia bungeni masuala yaliyoko mahakamani na shughuli za Idara ya Usalama wa Taifa.
Wakati akijiandaa kusoma vifungu vya kukatiza hotuba ya Profesa Kahigi, alitukana tusi zito la nguoni kwa lugha ya kimombo ambalo kwa sababu za kimaadili hatukuweza kuliandika, kisha akaendelea kuzungumza huku baadhi ya wabunge wakipigwa butwaa.
Hata hivyo, Naibu Spika, Job Ndugai aliyekuwa akiongoza shughuli za Bunge wakati huo, hakutoa karipio lolote huku akimruhusu Serukamba kuendelea kwa muda kabla ya kumkatiza na kumruhusu Mbunge wa Simanjiaro (CCM), Christopher Ole Sendeka kuzungumza.

Ubishi ulivyoanza
Muda mfupi kabla ya Profesa Kahigi kuanza kusoma hotuba yake, Serukamba alisimama na kuomba mwongozo wa Spika kupitia Kanuni ya 68(1) akitaka isisomwe kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa nne kwa kuwa unaingilia uhuru wa Mahakama... “Ni juzi tu Akoonay (Mustapha, Mbunge wa Mbulu - Chadema), alitukumbusha kwamba mambo hayo ni ‘prejudice’ kwa Mahakama kwa hiyo ukiruhusu hilo Naibu Spika itakuwa ni ajabu.”
Kabla Naibu Spika hajatoa mwongozo wake, alimtaka Profesa Kahigi kuzungumza kama anakubaliana na Serukamba, lakini Profesa Kahigi alisema anaomba kuendelea kusoma hotuba yake kama ilivyo.
Baadaye Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika aliomba kumpa taarifa Serukamba kwamba katika kurasa alizozitaja hakuna jambo lolote lililopo mahakamani hivyo aangalie vizuri.
“Mheshimiwa Naibu Spika napenda kumpa taarifa mtoa taarifa kwamba hakuna lolote lililopo mahakamani, ukurasa wa kwanza unazungumzia Idara ya Usalama wa Taifa, haipo mahakamani, ukurasa wa pili umemtaja Dk Stephen Ulimboka, halipo mahakamani hivyo hakuna lolote lililopo mahakamani,” alisema.
Baada ya hapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisimama na kueleza kuwa aliyoyasema Serukamba ni kwamba hotuba hiyo inafanya kesi iliyopo mahakamani kuwa ya kisiasa akisema... “Kifungu cha 16 cha Sheria ya Usalama wa Taifa hakiruhusu watumishi wa Usalama wa Taifa kutajwa humu ndani wala kuchapishwa popote.”
Naibu Spika alisimama na kusema jambo hilo limeshajitokeza ndani ya Bunge na Akoonay alishawakumbusha kuwa ni kuingilia Mahakama.
“Jambo hili lilishaleta kasheshe humu ndani na ruling (uamuzi) ya hili ilishatolewa na Spika, ‘ruling’ yangu ni kwamba kuanzia ukurasa wa kwanza mpaka wa nne, mambo ya Dk Ulimboka, Usalama wa Taifa na Lwakatare.........,” aliishia hapo Ndugai na kuwaruhusu Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki na Ole Sendeka kuzungumza.
Mdee alisema ukurasa wa kwanza mpaka wa tatu wa hotuba hiyo hakuna sehemu jina la Lwakatare lilipotajwa na kwamba ukurasa wa nne uliotaja jina la Lwakatare hauzungumzii mwenendo wa kesi... “Hoja anazoleta Lukuvi atusomee hiyo Sheria ya Usalama na atuelezee na alinganishe na kilichopo hapa.”
Mdee aliungwa mkono na Lissu aliyesema kuwa sheria anayozungumzia Lukuvi ipo lakini haikatazi kutajwa majina ya wanausalama ndani ya Bunge... “Ninayo hiyo sheria hapa ya mwaka 1996, haya maneno kwamba Sheria ya Usalama inakataza masuala ya Usalama wa Taifa kutajwa ni uchochezi. Hicho kinachoelezwa kukataza ‘disclosure’ (kuwataja) ni huko nje na si humu ndani.”
Lissu alisema sheria hiyo inakataza kuchapishwa majina hayo nje ya Bunge na si vinginevyo.
Kairuki alipingana na Lissu akieleza kuwa amepotosha kwa kuwa sheria hiyo ya Usalama wa Taifa hairuhusu kuwataja watumishi wake bila kuomba ruhusa kwa waziri.

“Lissu anapotosha kwa kuwa hairuhusiwi mtu yeyote kuchapisha jina la mtumishi wa Usalama wa Taifa bila kuomba ruhusa kwa waziri,” alisema Kairuki.Ndipo Naibu Spika alipompa tena nafasi Serukamba na alipoanza tu kuchangia kuliibuka maneno ya chinichini ambayo yalionekana kumkera ndipo alipotoa neno hilo zito.
Baadaye Ndugai alisema kwa kuwa hilo suala ni la kikanuni, anaiagiza Kamati ya Kanuni ikutane ili tujadili suala hilo.
Katika hotuba hiyo ambayo awali, waandishi walipata nakala yake, Profesa Kahigi alikuwa ameandika mambo mbalimbali yanayohusu kutekwa na kuteswa kwa Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka na masuala mengine yanayohusiana na kesi ya ugaidi inayomkabili Mkurugenzi wa Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare.
Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

HIVI SERIKALI KUU IPO KAZINI AU IPO LIKIZO ??????? NINACHOKISHANGAA MIMI NI KUWA HAKUNA NIDHAMU BUNGE LA SASA KABISA kulikoni????????? YAANI INAFIKIA HATUA MBUNGE ANATOA TUSI KUBWA HIVYO NA HAKEMEWI NI KWANINI? NI KWA VILE NI WA CCM AU HEBU WANA CCM BUNGENI KUWENI WA WAZI MNAHARIBU IMANI ZA WATANZANIA KWA KUWACHAGUA NA KUWAAMINI KUWAPA KURA ZAO HALAFU MNAKWENDA KUSIMAMIA MAADILI MABOVU BUNGENI TUNAKEMEA NA KUYAKATAA KWA KAULI MOJA haki haitafutwi kwa vita ila kwa AMANI ,UKWELI ,NA SHERIA (DEMOKRASIA YA KWELI NI IPI BASI?????)