ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 17, 2013

Mgambo yaichelewesha Yanga

Mshambuliaji wa Yanga Hamis Kiza (kushoto) akiwania mpira na mlinzi wa JKT Mgambo, Bashiru Chacha wakati wa mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga jana. Matokeo sare ya 1-1. Picha na Salim Mohamed.

Dar es Salaam. Yanga waliduwazwa na kiwango kizuri cha JKT Mgambo na kusubiri mpaka dakika tano kabla ya mchezo kumalizika kusawazisha bao na kuambulia sare ya bao 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Mkombozi aliyefuta aibu ya kipigo Jangwani, alikuwa Simon Msuva aliyemalizia wavuni piga nikupige kwenye lango la Mgambo katika dakika ya 40.
Sare hiyo imeweka gavana mbio za Yanga kutwaa ubingwa mapema, kwani kama ingeshinda leo, basi ingehitaji pointi nne tu kutwaa ubingwa, lakini kwa sare hiyo sasa inahitaji pointi sita.
Pia sare hiyo ni furaha kwa Azam, kwani ndiyo timu pekee inayoweza kuitatiza Yanga kwenye mbio za Ubingwa. Yanga sasa imefikisha pointi 53 na Azam katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 47.
Kocha wa Yanga, Ernest Brandts mara baada ya mchezo alimlaumu mwamuzi kwa madai ya kutoitendea haki timu yake, huku Kocha wa Mgambo Ramadhani Kampira aliwasifu wachezaji wake baada ya kuonyesha kiwango kizuri na kuibana Yanga.
Mgambo walikuwa wa kwanza kulifikia lango la Yanga dakika ya pili tu tangu kuanza kwa mchezo baada ya Isa Kanduru kufumua shuti kali lililochezwa vizuri na mlinda mlango wa Yanga, Ali Mustafa.
Yanga ilijibu shambulizi katika dakika ya 11 kupitia kwa Simon Msuva, ambaye shuti lake lilikwenda juu ya lango la Mgambo, huku dakika ya 15 Nizar Khalfan akipiga shuti ovyo lilikokwenda nje ya lango akiwa yeye tu na kipa wa Mgambo, Godson Mmasa.
Dakika ya 28, mwamuzi alilazimika kusimamisha mpira baada ya Frank Domayo kuumia na kutolewa nje baada ya kugongana na mchezaji wa Mgambo, Issa Kanduru.
JKT Mgambo walizigusa nyavu za Yanga dakika tatu kabla ya mapumziko kupitia kwa mshambuliaji Kanduru aliyemalizia vizuri pasi ya Nassoro Gumbo na matokeo kubaki hivyo mpaka mapumziko.
Dakika tano kabla ya mchezo kumalizika, Yanga walisawazisha bao hilo kupitia kwa Msuva aliyemalizia wavuni piga nikupige kwenye lango la Mgambo na hivyo kuambualia pointi moja.
Mwananchi

No comments: