ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 14, 2013

Nancy Sumari: Aelezea siri kuu ya mafanikio yake

Alipovikwa taji la umalkia wa Tanzania, wengi hawakutazamia mabadiliko yeyote katika mashindano ya ulimwengu.

Lakini yeye aliweza…akaleta nyumbani kwa mara ya kwanza, taji la Miss World Afrika.
Ni Nancy Sumari ambaye anasema, siri kuu ya mafanikio yake, ni kuthubutu na kujituma. Sumari anasema amefanikiwa katika mambo mengi kutokana na kujiamini katika kila jambo alilolifanya sambamba na kujituma.

“Utamaduni wangu ni kujiamini katika kila jambo ninalolifanya na hiyo ndiyo siri ya mafanikio yangu. Ndiyo maana niliweza kushinda mataji ya Miss Dar Indian Ocean, Miss Kinondoni, Miss Tanzania na hatimaye Miss World Africa,” anasema Nancy.
Nancy hakuanza na maisha ya mafanikio kwa usiku mmoja-bali aliwahi kupitia changamoto na kazi mbalimbali kabla ya kuwa mrembo mwenye hadhi ya kimataifa.

Aliwahi kuuza duka la samani za nyumbani na kulipwa mshahara wa Sh 120,000 kwa mwezi.
Kwa jitihada, zake na uthubutu kama asemavyo, hivi sasa Nancy ni mhitimu mtarajiwa wa taaluma ya biashara katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

Si hivyo tu bali ni Mkurugenzi wa Matukio wa Kampuni ya Frontline Management ambayo inahusika na masuala ya mahusiano ya umma.

Vilevile Nancy ni mwandishi wa vitabu na pia anahusika katika kuhakikisha mtandao wa Bongo 5.com unafanikiwa akishirikiana na mumewe.

Licha ya kazi za kiofisi Nancy pia ni mmoja wa mabalozi wa One Billion Living muunganiko wa wanawake duniani wanaopinga ukatili na kuelimisha wanawake.

Moja ya kazi zake za uandishi ni kitabu cha nyota yako ambacho Nancy anasema maudhui yake yametokana na uhaba wa hadithi za watoto zilizoandikwa na watanzania. “Mbali ya kuwa mimi ni mama kwa wakati huu, kila nilipokwenda kwenye maduka ya vitabu, nilikosa vitabu vya watoto vilivyoandikwa na waandishi wa Tanzania. Vingi vimeandikwa na waandishi wa nje,”alisema.

Anasema aliamua kuandika kitabu, ambacho watoto wa kike wa Tanzania wataweza kukisoma na kuvutiwa kufanya kile kilichoandikwa katika kitabu hicho.

“Nyota yako ni kitabu kinachoelezea nafasi ya mwanamke katika jamii. Kitabu hicho kinaonyesha namna gani wanawake wenye mafanikio walivyoweza kuyapata ili kutoa mwanga kwa watoto wa kike kusoma kwa bidii na kuzifikia ndoto zao,” anasema Nancy.

Nancy anasema hata wanawake wa majumbani wanapaswa kukisoma kitabu
hicho ambacho kwa sasa kipo katika maduka ya vitabu mbalimbali.
Mpangilio wa ratiba na maisha binafsi
Nancy anasema akiwa kama mwanamke mwenye familia anapangilia mambo yake ipasavyo ili kuhakikisha anatimiza majukumu yake yote kwa pande zote zinazomhusu.“Mwanamke amepewa kitu cha ziada, anaweza kutekeleza majukumu yote bila kusitasita. Kwa upande wangu namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kwani natekeleza majukumu yangu yote licha ya kwamba nina mambo mengi ninayoyafanya” anasema

Mama huyo wa mtoto mmoja aitwaye Zuri anasema anaweza kumlea mtoto wake, baba wa mtoto, na majukumu mengine ikiwamo masomo na kazi mbalimbali anazozifanya.
Anasema mara nyingi kazi hizo zimekuwa zikimchosha na anaporudi nyumbani anakutana na familia ambayo inamuhitaji

“Nashukuru Mungu familia yangu inanielewa hasa mtoto japokuwa ni vigumu kwake huwa najitahidi kuwa karibu naye ili asijione mpweke” anasema
Changamoto
Maisha hayakosi changamoto, nancy anaeleza vikwazo anavyokutana navyo katika maisha kuwa ni dharau kutoka kwa wadau.
Anasema anaposhughulikia masuala ya kiofisi wengi wamekuwa wakimchukulia kama mtu asiye makini katika jambo analotaka kulifanya.
“Unajua nakumbana na vitu vingi sana, kuna wakati naingia katika ofisi fulani kushughulikia masuala yangu ya kikazi, matokeo yake watu wananichukulia sivyo na kudhani kwamba sijadhamiria na siwezi kufanya jambo hilo,” anasema

No comments: