Pichani na sehemu ya raia wakiwamo wanawake, watoto na wanaume wakikimbia machafuko katika eneo la Mashariki ya Kongo, siku ya Jumatano, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lilikuwa na majadiliano ya siku nzima kuhusu ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama. Katika Majadiliano hayo, ilidhihirisha wazi kwamba licha ya juhudi mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Jumuiya ya Kimataifa katika kupigania na kutetea haki na usalama wa wanawake katika maeneo yenye vita, bado wanawake, watoto na hata wanaume, wanaendelea kudhurumiwa utu na hadhi yao kwa kufanyiwa ukatili mkubwa ikiwa ni pamoja na kubakwa, mbinu inayoendelea kutumiwa kama mbinu ya kivita. Ukatolewa wito wakati wa majadiliano hayo wa kuendelea kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaobainika kuhusika na ukatili huo ikiwa ni pamoja na kutafuta namna ya kuwafidia waliodhulumiwa utu wao.
Na Mwandishi Maalum.
Tanzania imeungana na mataifa mengine katika kuendelea kukemea vitendo vya udhalilishaji wa kingono vinavyoendelea kufanyika dhidi ya wanawake, watoto na hata wanaume katika maeneo yenye migogoro.
Kwa siku nzima ya jumatano, Baraza Kuu la Usalama, lilikuwa na mjadala kuhusu wanawake, amani na usalama, ambapo wazungumzaji zaidi ya 60 waliozungumza, licha ya kukiri kwamba kumekuwa na mafanikio fulani katika kukabiliana na unyanyasaji na udhalilishaji huo lakini hali bado ni ngumu na ya kutisha.
Majadiliano hayo ambayo yamefanyika chini ya urais wa Rwanda ambaye ndiye anayeongoza Baraza hilo kwa mwezi huu wa April, yalifunguliwa na Katibu Mkuu Ban Ki Moon kwa kuwasilisha Taarifa yake iliyotoa tathimini ya kina kuhusu hali ya wanawake, amani na usalama katika maeneo mbalimbali ambako migogoro bado inaendelea.
Katika taarifa yake, Ban Ki Moon, anakiri kwamba vitendo vya udhalilishaji wa kingono ukiwamo ubakaji, vinaendelea katika maeneo yenye migogoro kama vile huko, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Syria, Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, akasema kwamba, ingawa jukumu la awali la kuzuia na kukabiliana na udhalimu huo ni la serikali husika, lakini bado jumuiya ya kimataifa inatakiwa kutumia kila mbinu na raslimali zilizopo kutafuta vyanzo vya udhalimu huu ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria watuhumiwa na wahusika wa udhalilishaji huo.
Ban Ki Moon, akaelezea zaidi kwamba Misheni zote Umoja wa Mataifa zinazohusika na ulinzi wa Amani, zimepewa mafunzo ya namna ya kufuatilia, kukukusanya na kuzifanyia tathimini na kisha kuwasilisha taarifa zinazohusu matukio ya udhalilishaji wa wanawake , watoto na hata wanaume katika eneo lao la jukumu.
Akaongeza kwa kusema udhalilishaji wa kijinsia si tu kwamba unadhalilisha utu wa yule aliyedhulumiwa lakini pia unaharibu mfumo mzima wa familia, na kwamba jambo hili halikubali.
Mjumbe wa Tanzania katika Mkutano huo, Afisa Mwandamizi katika Ubalozi wa Tanzania, Dr. Justin Seruhele akizungumza kwa niaba ya serikali, alisema pamoja na kuunga mkono hoja ya kufikishwa mbele ya sheria watuhumiwa wa uharamia huo, na kuongeza kasi ya kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo, Tanzania pia inasisitiza matumizi ya vyombo vya kisheria vya ndani ya nchi husika katika kuwashughulikia wahalifu hao.
Akasema ikiwa vyombo vya kisheria vya nchi husika vitawezeshwa vitasaidia sana katika kuhakikisha kwamba mkondo wa sheria unachukua nafasi yake, na haki inatendeka.
Hata hivyo Tanzania inasema, ikidhihirika kwamba nchi husika haina vyombo imara kuifanya kazi hiyo, na kama ambavyo mara nyingi imeshadhihirika hivyo. Basi nchi husika zikubali kuwapeleka watuhumiwa katika vyombo vya kimataifa kama vile Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ( ICC) , chombo ambacho licha ya kasoro zake, lakini kimeonyesha uwezo mkubwa wa kuwashughulikia watuhumiwa wa makosa ya jinai.
Tanzania ikasema inaunga mkono ICC na inakubaliana na wazungumzaji wengine, kwamba ICC inapashwa kuungwa mkono ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu.
No comments:
Post a Comment