Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani akiwasilisha bungeni makadirio ya matumizi ya ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2013/14 mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani amesema vijana wengi wanaoomba ajira katika taasisi mbalimbali za Serikali, wanawasilisha nyaraka nyingi za kugushi.
Akiwasilisha taarifa ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Kombani alisema kuwa changamoto kubwa ambayo Serikali inapata katika kuajiri watumishi wapya ni tabia ya kughushi vyeti ili wahusika waonekane wanasifa za kupata ajira katika idara za Serikali.
Akiwasilisha Mpango wa Makadirio ya Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2013/14, Kombani alisema kuwa Serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya watumishi wake nchini. Alisema katika mwaka wa fedha 2013/14 inatarajia kuajiri watumishi 61,915 huku akisema hadi kufikia Machi mwaka huu, kati ya nafasi 4,377 za ajira zilizokuwa zimetolewa nafasi 3,346 zilikuwa mpya na 1,031 zilikuwa ajira mbadala.
Katika suala la rushwa waziri huyo alisema kuwa jumla ya kesi 578 zilifikishwa katika mahakama mbalimbali nchini, ambapo 79 zilitolewa hukumu huku kati ya hizo watuhumiwa 33 wakitiwa hatiani na wengine 41 wakiachwa huru na nyingine tano ziliondolewa.
Kombani alisema kuwa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), itaendelea na uchunguzi wa tuhuma takriban 2,000 zinazohusu rushwa katika idara mbalimbali zikiwamo maliasili, madini na gesi pia itaendelea kushughilia kesi 495 zilizopo mahakamani zinazohusiana na rushwa.
Alisema pia taasisi hiyo itaendelea kutoa mafunzo kuhusiana na athari za rushwa na kuweka mikakati ya kudhibiti mianya ya vitendo hivyo ambayo inarudisha nyuma maendeleo kwa kunufaisha watu wachache.
Mbali na hayo alisema kuwa watatoa mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ikiwa ni sehemu ya kuwapatia mafunzo ya kazi watendaji wake.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment