ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 18, 2013

Kingunge: Unafiki umeua Azimio la Arusha

Azimio la Arusha lililoanzishwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1967, lilipoteza mwelekeo wake kufuatia uamuzi wa Halmashauri kuu ya CCM uliofikiwa Februari 2, 1991 mjini Zanzibar.
Kulikuwa na mambo matano muhimu (miiko ya viongozi wa umma) yaliyoazimiwa katika azimio hilo ambayo ni kiongozi wa chama au Serikali sharti awe mkulima au mfanyakazi na asishiriki katika jambo lolote la kibepari au la kikabaila.
Jingine ni kiongozi kutokuwa na hisa katika makampuni, asiwe mkurugenzi katika makampuni ya kikabaila au kibepari, asiwe na mishahara miwili au zaidi na asiwe na nyumba ya kupangisha.
Lakini baadaye miiko hiyo ilikuja kuonekana kuwa mzigo siyo tu kwa viongozi bali hata kwa wanachama wa TANU na baadaye CCM.

Miiko ilipovunjwa
Kada mkongwe wa Chama cha Mapinduzi Kingunge Ngombare Mwiru amefafanua kupanda huko na kushuka kwa Azimio la Arusha alipokuwa akichangia mjadala wa Azimio la Arusha na Dira ya maendeleo ya mwaka 2025, ikiwa ni sehemu ya tamasha la Kigoda cha kitaaluma cha Mwalimu Nyerere lililofanyika hivi karibuni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 
“Wale waasisi wa Azimio la Arusha walipoweka sera waliona kuwa lengo ni kutekelezwa na viongozi, ndiyo maana wakawekewa miiko ili wasitumie madaraka kujineemesha, kama vile kiongozi asiwe na nyumba ya kupangisha, mishahara miwili na mengineyo,” anasema Kingunge.
Anaongeza kuwa miiko hiyo iliwekwa kwa kuzingatia mazingira ya wakati huo ambapo kabla ya Azimio la Arusha mwaka 1967 walishaanza kujineemesha.
Anasema mwaka 1977 wakati wanatathmi azimio hilo na kuviunganisha vyama vya TANU na ASP waliingiza misingi hiyo kwenye katiba ya chama kwa ushabiki.
“Mwaka 1977 nilikuwa katika kamati ya watu 20 ya kutengeneza katiba ya chama, lilikuja suala la miiko. Sisi wajumbe tulikuwa na ushabiki wa ujamaa, ile miiko iliyokuwa ya viongozi, tukaiweka kwenye rasimu ya Katiba. Kama mnafanya vitu kwa ushabiki, mnazalisha unafiki na huo ndiyo umeua azimio,” alisema Kingunge.
Anakumbusha tukio la mwaka 1989 baada ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Dodoma, ambapo Mwalimu Nyerere aliwaita ofisini akiwa na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi ofisini kwake.
“Tulipofika akamwita Rais Ali Hassan Mwinyi na kumwambia kuwa, yeye anazo mali nyingi alizopewa wakati anastaafu. Ana ng’ombe zaidi ya 500 aliopewa na Wasukuma, mashamba na msitu wake. Je, kwa hali hiyo akauliza kama anafaa hata kuwa mwana CCM. Baada ya kutafakari hilo na kwa kuwa mimi nilikuwa kiongozi wa itikadi akanipa kazi ya kurekebisha suala hilo kwenye katiba,” anasema.

CCM imeshindwaje kutekeleza?
Anasema kuwa baada ya kufanya marekebisho aliwasilisha ripoti yake mwaka 1990 ambayo ilionyesha makosa ya kuiingiza miiko hiyo kama masharti ya kuwa mwanachama wa CCM.
Anasema katika marekebisho hayo, waliweka katika Katiba ya CCM ibara ya 18 iliyokataza viongozi wake kutumia madaraka yao kujinufaisha.

“18. Ni mwiko kwa kiongozi:-
(1) Kutumia madaraka aliyopewa ama kwa ajili ya manufaa yake binafsi au kwa upendeleo, au kwa namna yoyote ambayo ni kinyume cha lengo lililokusudiwa madaraka hayo. (2) Kupokea mapato ya kificho, kutoa au kupokea rushwa, kushiriki katika mambo yoyote ya magendo au mambo mengine yaliyo kinyume cha lengo lililokusudiwa madaraka hayo. (3) Miiko mingine ya Viongozi itakuwa kama ilivyowekwa katika kanuni zinazohusika.”
“Suala la msingi unayatumiaje madaraka. Katika kujenga ujamaa inahiutajika dhamira ya kweli na kuujua mno, kwa Kiingereza ‘commitment’.
Lakini sisi kwenye dhamira watu wanaweka ubinafsi. Usimamizi wa kipengele (ibara ) hiki katika CCM haupo. Hiki siyo kikao cha chama cha kukosoana, ningesema mengi tu,” anasema Kingunge.

Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma
Kuhusu Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma inayohusika na kuratibu mali ya viongozi hao, Kingunge anasema kuna matatizo mengi.
“Mmezungumzia Sekretarieti ya maadili ya umma, nalo ni tatizo. Unasema tujaze mali zetu na kweli wanajaza lakini nani anasimamia? Kama tungekuwa tunafuatilia maneno ya wananchi huko tungejua mengi. Utasikia wananchi wanasema fulani ni mwizi…” anasema.
Mjadala huo ulitanguliwa na hotuba ya Jaji Mkuu wa Kenya, Dk Willy Mutunga ambaye aliyekuja na tafakuri ya ‘virusi vya Azimio bado vinaniandama’ akiwataka Waafrika kuwa na chembechembe za azimio hilo kwa kujenga Afrika inayojitegemea.
Kauli hiyo iliunga mkono na Mbunge wa zamani wa Ukerewe, Gertrude Mongela alipokuwa akichangia mjadala akisema kuwa viongozi wa zamani wameshindwa kuwarithisha vijana virusi vya azimio.
“Sisi viongozi wa zamani hatuenezi virusi vya azimio, kila mtu amevaa kondomu. Matatizo haya ya wanawake kubakwa, kunyanyaswa, uporaji ni kwa sababu ya kutoeneza Azimio la Arusha, tuvue kondomu,” alisema Mongela.  

Azimio la Arusha na Dira ya Maendeleo 2025
Awali akichangia mjadala huo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe alieleza tofauti iliyopo kati ya Azimio la Arusha na Dira ya maendeleo ya mwaka 2025 akisema kuwa Azimio hilo lilikuwa ni mwongozo wa maadili ya Watanzania wakati dira hiyo ililenga kuinua uchumi kufikia mwaka 2025.
“Azimio la Arusha lilikuwa na mtu wa kulitetea baada ya kutangazwa, wakati dira ya maendeleo ya mwaka 2025 haikuwa na mtetezi na ilikaa miaka 10 tangu ilipoanzishwa mwaka 1995 hadi kuanza kutekekelezwa,” anasema Zitto na kuongeza:
“Azimio lilizungumzia usawa wa binadamu wakati dira imezungumzia maendeleo ya uchumi bila kujali kama yataleta mgawanyiko wa kitabaka na kipato.”
Zitto anaongeza kuwa ni ujinga kufikiri kuwa maendeleo yataletwa bila kuwajali wakulima wadogo vijijini na kusisitiza haja ya kurudi kwenye misingi ya Azimio la Arusha.
Hata hivyo, Profesa Samuel Wangwe akichangia hoja hiyo anasema kuwa kulikuwa na ushirikishwaji wa vyama vya siasa wakati wa kuanzishwa kwa dira hiyo.
Profesa Wangwe ambaye ni mtaalamu wa uchumi, amekiri kuwepo kwa tatizo la utekelezaji tangu dira hiyo ilipoanzishwa.
“Vyama vyote vya siasa kasoro kimoja ambacho sitakitaja, vilishirikishwa. Misingi yote ya Azimio la Arusha haijawekwa kando bali imeingizwa, kwa mfano utawala bora na kujenga misingi ya uchumi,” anasema Profesa Wangwe.
Hata hivyo, kiongozi wa malumbano hayo Jenerali Ulimwengu amepinga hoja ya mfumo wa soko huria uliomo katika dira hiyo akisema kuwa inalenga kupora rasilimali za nchi.
“Usimshangae kuona mwewe akimshauri kuku aache vifaranga wake wawe huru, bali mshangae kuku atakayesikiliza ushauri huo,” anasema Ulimwengu.
Mwananchi

No comments: