Kila mtu ana mahitaji binafsi. Hutakiwi kukwepesha mambo yako kwa lengo ama la kumfurahisha mwenzi wako au kudharau yako na kujali ya mwenzio. Hilo ni kosa sana, kwani naye anatakiwa atambue mahitaji yako muhimu na akuunge mkono katika kuhakikisha unafurahia mapenzi na maisha kwa jumla.
Pamoja na ukweli kwamba unapoanzisha uhusiano inakubidi baadhi ya vitu uviache ili kwenda sawa na mwenzi wako, ila hutakiwi kupuuza yale mahitaji ambayo kwako huona ni ya lazima. Endapo utakosea na kuthubutu kuyapuuza, utayafanya mapenzi yako kuwa na kasoro nyingi.
Mathalan, wewe ni mtu wa mazoezi, kwa hiyo kila jioni unapendelea kwenda gym kwa ajili ya kuuweka mwili wako katika hali nzuri. Itakuwa ni jambo la ajabu sana, endapo utaamua kuacha utaratibu huo kwa vile mwenzi wako anapenda kila siku jioni mwende ufukweni na maeneo mengine kula raha.
Jambo la muhimu kwako ni kuhakikisha unapanga vizuri muda wako. Yaani mahudhurio yako ya gym yawe palepale, hakikisha unaiheshimu ratiba yako ili na mpenzi wako naye aiheshimu. Ukifanikisha hilo, sasa mtahamia kwenye ratiba yake. Baada ya gym mtakwenda ufukweni kuburudika.
Asili ya kila binadamu, ndani yake kuna kipawa cha kujiuliza (reasoning capacity). Wengi hukosea kwa sababu hukitumia kipawa hicho baada ya matokeo, badala ya mwanzoni kabla ya kuamua. Ni kituko kama siyo kichekesho, kujiuliza ni kwa nini umeacha utaratibu wako baadaye, wakati ulipaswa kufanya hivyo mwanzoni.
Kila mtu anaishi kwa masilahi. Usipozingatia masilahi yako, unataka nani mwingine akufikirie? Kutoweka wazi au kupuuza vipaumbele vyako ni usaliti wa hali ya juu. Utamfanya mwenzi wako asijue mambo unayoyapenda, halafu ataishi na wewe bila kujua kile ambacho anatakiwa kukitekeleza kwa ajili yako.
Hali hiyo, itamfanya akupunje yale ambayo pengine unatamani akufanyie ili uyafurahie maisha ya kimapenzi. Kosa linakuwa siyo la kwake, ni uzito wako wa kuweka wazi vipaumbele vyako. Tafadhali sana, usijidhulumu nafsi yako, usijipe mateso wakati kupata utamu ni hiari yako.
Binadamu huishi kwa kusikilizia. Mwanzoni kabisa katika uhusiano wao, hutumia muda mwingi kuwasoma wenzi wao. Ajabu ni kwamba kipindi hicho ndicho huzaa mazingaombwe ya aina yake, kwani kila mmoja huwa ‘bize’ kuficha kucha, hivyo kusababisha hali ya kusomana, isiwe na mafanikio yoyote.
Ufafanuzi; Wewe unamsoma halafu unaficha kucha, naye anakusoma lakini naye hataki ajulikane. Unadhani mafanikio gani yatapatikana? Tatizo hili ndilo ambalo husababisha watu wengi kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi wakiwa hawajuani, hivyo kuleta migogoro baadaye.
Baada ya uhusiano kufikisha umri fulani, kila mtu humzoea mwenzake. Ile hofu ambayo ilikuwa mwanzoni huondoka, sasa zile kucha zilizofichwa, kila mmoja huanza kuzichanua. Ni hapo ndipo lawama za “siku hizi umebadilika” huibuka. Ukweli ungezingatiwa, lawama hizo zisingetokea.
Kumbe sasa, kama ni mabadiliko, basi alibadilika mwanzoni mwa uhusiano kwa sababu alificha kucha. Baadaye anapoonesha tabia zake halisi, huonekana amebadilika. Ni kazi nzito sana kudumu na uhusika wa bandia. Unaweza kuuvaa kwa kipindi kifupi lakini baadaye utakushinda. Siku zote wewe utabaki kuwa wewe.
USIWE MTU WA WASIWASI
Ukishakubali kuwa utamu au mateso ya mapenzi ni wewe mwenyewe, utazingatia kipengele hiki. Hupaswi kabisa kuwa mtu wa wasiwasi. Jaribu kujitengeneza kila siku iendayo kwa Mungu, kuepuka mawazo mabaya ambayo yatakufanya uwe mwenye wasiwasi.
Fikiria chanya. Mpe mwandani wako fursa ya kujiamini ili aweze kufikiria mazuri kwa ajili yako. Endapo atabaini humwamini na una wasiwasi juu yake, utamsababishia awe na hali hiyohiyo kwako. Mambo hayo huchanua kwa kasi ya moto wa kifuu kikavu na kusababisha kupotea kwa uaminifu.
Wasiwasi wako huzaa wasiwasi wake. Matokeo ya jumla kila mmoja kutomwamini mwenzake. Hayawezi kuwa mapenzi matamu kama hamuaminiani. Maisha ya uaminifu huanza na wewe mwenyewe. Shakashaka zisizo na maana unatakiwa uziweke mbali nawe. Ishi kwa uhuru, epuka wasiwasi.
Itaendelea wiki ijayo.
GPL
No comments:
Post a Comment