ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 29, 2013

Mbunge: Mafisadi wa ardhi wafukuzwe kazi mara moja

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Amina Makilagi ametaka uongozi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwatimua watumishi wake wanaojihusisha na ufisadi wa ardhi kwani hao ndiyo wanaosababisha watu wakichukie Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akichangia katika bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2013/14, Makilagi alisema watumishi wanaojilimbikizia viwanja hawapaswi kufumbiwa macho bali wachukuliwe hatua za haraka.

“Kuna watumishi katika wizara yako wenye viwanja vingi lakini wanachofanya ni kuviweka katika majina tofauti,naomba wachukuliwe hatua kwani hao ndiyo wanasababisha CCM ichukiwe na wananchi,” alisema Makilagi ambaye ni Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).

Alisema wanaobanika kufanya ufisadi wa ardhi wasihamishwe bali wafukuzwe kazi kwani wakiachwa watakwenda kuendelea na tabia hiyo.

Makilagi alisema kwenye halmashauri viongozi wengi wamejilimbikizia viwanja hali ambayo wizara inahitaji kufuatilia kwa karibu ili kuwabaini watu hao.

“Watumishi kama hawa ndiyo wanatuharibia katika chama chetu tusiwaonee haya ni lazima tuwang’oe,” alisema.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Grace Kihwelu alitaka wizara hiyo ipewe fedha za kutosha ili iweze kupima ardhi nchi nzima kwa ajili ya kuepusha migogoro ambayo imekuwa tishio hapa nchini.

“Kupima viwanja kunahitaji fedha za kutosha, tuamue sasa kuwekeza katika upimaji wa ardhi ili kuondokana na migogoro ya muda mrefu,” alisema.

Mwananchi

No comments: