ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 14, 2013

Fedha yaweza kununua kila kitu si uhuru wa mtu

KWANZA kabisa namshukuru Muumba kwa kuniamsha salama leo.
Nina imani kwa uwezo wake, wote mu wazima japokuwa wiki hii tumepata tena pigo lingine kwenye tasnia ya sanaa kwa kuondokewa na kipenzi chetu Jaji Khamis ‘Kashi’. Mungu ampokee na kumpa mapumziko mema yenye furaha ya milele.

Leo nazungumzia uwezo mdogo wa watu kufikiri kuwa fedha inaweza kununua kila kitu chini ya jua.
Kweli fedha ina nguvu sana chini ya jua kwa kufanya chochote, lakini vipo ambavyo fedha haiwezi kuvinunua. Leo nafafanua fedha ina nafasi gani katika mapenzi.
Fedha katika mapenzi inaweza kununua mahitaji yote muhimu kama nguo, nyumba, gari lakini haiwezi kununua moyo au furaha ya mtu.
Huwezi kusema fedha yako ndiyo inaweza kumtuliza mpenzi wako bila mapenzi ya kweli, penzi linalolindwa na fedha huwa la upande mmoja na lililokosa kujiamini.
Ukimuona mtu amekaa kwenye uhusiano bila mapenzi basi kuna kitu anakihitaji lakini si mapenzi yako kwa vile ipo siku atataka uhuru wa moyo wake na lazima ataondoka na kuachana na fedha zako.

Nasema haya baada ya kupokea ujumbe toka kwa dada mmoja ambaye alinilalamikia tabia za mume wake kumnyima uhuru kwa vile tu ana fedha. Toka aolewe na yule bwana amekuwa mtu wa ndani kama utumbo, kazi kamuachisha japokuwa ana elimu kubwa aliyoisomea nje ya nchi. 

Kutokana na wivu wa yule mwanaume alimuachisha kazi na kuamua kumlipa mshahara.
Mumewe ana uwezo mkubwa kifedha, wana nyumba nzuri ya kisasa, magari na kila kitu muhimu katika maisha ya mwanadamu, lakini fedha za yule bwana zimemfanya atengane na ndugu jamaa na marafiki. Haendi popote bila kuongozana naye, akisafiri nje ya nchi haruhusiwi kuvuka nje ya geti.
Hapo mwanzo nilimshauri lakini maji yamemfika shingoni na kuamua kubwaga manyanga, hivi tunavyozungumza amerudi kwao. Nina imani kwa uchache umeona jinsi gani fedha za yule mwanaume zilivyomgeuza kuwa mfungwa.

Inawezekana mwanaume nia yake ni nzuri kwa kutaka kummiliki mkewe peke yake kwa kumwekea ulinzi ili kuona hatoki nje ya ndoa, lakini amesahau kwamba unaweza kununua kila kitu lakini huwezi kununua moyo wa mtu. Siku zote kila kiumbe kinahitaji uhuru wa moyo hasa katika mapenzi.
Kosa kumnyima uhuru mpenzi wako kwa kuonyesha humuamini hata asilimia moja, ambapo kama humuamini hakuwa sahihi kuwa mpenzi wako kwa vile ni kuukaribisha ugonjwa wa moyo. Siku zote mtu huanzisha uhusiano na mtu mwingine baada ya kuridhika na tabia yake.

Humuamini? Kwa nini umemuoa? Inawezekana kutokana na uzuri wake ndiyo unaokuchanganya na kujikuta ukitafuta njia ya kumdhibiti ili asitoke wengine wasikuchukulie.
Hivyo, unatumia fedha zako kuununua moyo wake kwa kumnunulia kila kitu lakini uhuru unamnyima, hapo hakuna mapenzi bali uhaini wa mapenzi.

Fedha yako iwe katika maendeleo yenu lakini kamwe isichukue uhuru wa mwenzio. Naye anahitaji kubadilishana mawazo na watu kupata mawazo mapya, si kila siku kukaa ndani peke yake eti umemnunulia laptop na mtandao au kuzungumza na watu kwa simu haitoshi.

Mtu huyo ana tofauti gani na mfungwa? Moyo wa uvumilivu una kikomo na mateso yakizidi hugeuka chuki isiyo na msamaha.
Mpe uhuru mpenzi wako kama humuamini hafai kuwa mkeo. Kwa leo haya machache yanatosha

Tukutane wiki ijayo.
GPL

No comments: