“Usiku huo, nikamuwaza sana Shantale, ni mwanamke mrembo lakini simthamini. Kipindi chote nikiwa nusu mwehu kwa sababu ya mapenzi ya Jannine, sikumhesabu kama mpenzi wangu, isipokuwa nilikuwa nashindwa jinsi ya kumtamkia tuachane kutokana na mambo aliyonifanyia.
“Kuna siku nilimwambia tuachane, alilia sana. Alituma SMS kila siku kubembeleza turudiane, baadaye akaniambia endapo nitashindwa kumwelewa ombi lake, nitasababisha afeli chuo, kwa maana alikuwa hawezi kufanya kitu chochote tangu nilipomwambia tuachane.
“Kwa maana hiyo, nilikuwa na Shantale kama mwanamke wa kwenye kapu, sikumjali kabisa, marafiki na wafanyakazi wenzangu walimjua Jannine peke yake. Ndugu zangu, hususan dada zangu waliwajua wote na siku zote waliniambia mwanamke mzuri ni Shantale na kwamba Jannine hanifai, kwani si mjenzi wa familia, bali ni mwanamke mwenye dharau, maringo na kauli chafu.
“Nilipomuwaza sana Shantale nikakumbuka ukarimu na wema wake kwangu. Hata siku moja hajawahi kuninyanyasa. Alinisaidia nikiwa na shida, tena hakunisimanga. Nilipomwambia tuachane, hakusema vitu alivyoninunulia nimrudishie, alinibembeleza tu nisimuache kwa sababu ananipenda sana.
“Nilichanganua kwa marefu na mapana, mwisho nikagundua kwamba Shantale ni mwanamke mwenye thamani kubwa lakini namnyanyasa. Nilimuona ni almasi iliyochanganywa na chupa, kwa hiyo si rahisi kuitambua na kujua thamani yake. Kikubwa kilichonivutia kwake ni kauli, Shantale ana kauli nzuri sana.
“Kikubwa kilichonikimbiza kwa Jannine ni kauli, maana mdomo wake ni mchafu mno. Asubuhi kulipopambazuka, nilimtumia SMS Jannine, nikamwomba tuonane, kwanza alichelewa kunijibu, baadaye akaniambia ataangalia ratiba zake kama itawezekana.
“Alizidi kunifanya nimuone hanifai baada ya mimi kumuuliza kama ana ratiba gani tofauti na za kawaida akitoka kazini, akasema alikuwa amepanga kukutana na marafiki zake waende ufukweni. Akanisisitizia ni mtoko wa yeye na wanawake wenzake na ni muhimu kwake.
“Nikamtumia SMS Shantale kuomba kuonana naye, baada ya muda mfupi ilijibiwa kwamba yupo tayari, akaniuliza muda. Kwa mara ya kwanza nilimtoa ‘out’ Shantale, tukaenda kwenye hoteli yenye mandhari tulivu, nikamuomba msamaha kwa kujifanya kipofu siku zote hata nikaacha kuuona upendo wake.
Itaendelea wiki ijayo. GPL
No comments:
Post a Comment