Mfumo wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba unaonyesha dhahiri kukichanganya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mfumo huo ulipendekezwa katika rasimu ya Katiba mpya iliyozinduliwa Jumatatu ya wiki iliyopita na Tume ya Mabadiliko ya Katiba imayoongozwa na jaji mstaafu, Joseph Warioba.
Tume hiyo ilipendekeza kuundwa kwa serikali za Shirikisho, Tanzania Bara na ya Zanzibar huku ikiainisha mambo saba ambayo yatashughulikiwa na serikali hiyo..
Mambo hayo ni Katiba, Ulinzi na Usalama, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa, Ushuru wa Bidhaa na Mapato yasiyokuwa ya kodi.
Baada ya tume hiyo kutoa mapendekezo yake katika rasimu hiyo, makundi mbalimbali ya jamii yanahoji pendekezo la mfumo wa Muungano wa serikali hususani uundwaji wake na uendeshaji.
Miongoni mwa mambo yanayohojiwa ni muundo wenyewe, kiongozi mkuu wa serikali ya Tanganyika ataitwa Rais au waziri Mkuu, je, atakuwapo Makamu wa Rais.
Baadhi ya watu wanasema serikali tatu zitahitaji kuendeshwa kwa gharama kubwa na kuhoji serikali ya Shirikisho itaendeshwa kwa mapato gani wakati mapato yatakuwa yanakusanywa na serikali za Zanzibar na Tanzania Bara.
Lipo pia suala la utawala kwamba Rais wa Shirikisho anaposafiri au kupata udhuru ni nani atakaimu madaraka yake. Wengine wanahoji nani atakuwa na madaraka makubwa kati ya Rais wa Tanzania bara na Zanzaibar.
Wako wanaohoji kwamba ni utaratibu upi utawekwa kwa ajili ya watu wanaotaka kugombea urais wa Shirikisho, Zanzibar na Tanzania Bara.
Baadhi ya watu wanaoupigia hesabu urais mwaka 2015 kauli wanazozitoa zinaonyesha wazi kuwa wameingiwa na hofu kutokana na kushindwa kuelewa wagombee wapi.
Haya yote na mambo mengine yenye utata ndiyo yanayosababisha makundi mbalimbali ya jamii kuhoji mambo mengi kuhusiana na suala la mfumo wa serikali tatu.
Hata hivyo, CCM ambacho sera yake ya mfumo wa Muungano ni serikali mbili, kimejikuta katika wakati mgumu wa kuamua.
Kwa kuwa ni suala la sera, chama hicho tawala kitapaswa kwenda kwa wanachama wake kupata maoni yake kabla ya kuridhia mfumo wa Muungano wa serikali tatu.
Ni dhahiri kwamba ikiwa wanachama wa CCM watakataa pendekezo la mfumo wa serikali chama hicho ambacho ndicho kinachounda serikali kitatumia ushawishi wake katika vyombo vya maamuzi likiwamo Bunge kulikataa pendekezo hilo.
Chama hicho kina idadi kubwa ya wabunge katika Bunge Maalum la Katiba, lakini pia Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete ndiye kiongozi mkuu wa nchi ambaye atakabidhiwa rasimu hiyo kabla ya kupigiwa kura ya maoni na wananchi.
Katika hatua inayoonyesha kuwa chama tawala kinajipanga kabla ya kutoa msimamo wake, Kamati Kuu (CC) ya CCM leo itakutanakujadili suala hilo.
Wiki iliyopita, chama hicho kilitangaza kwamba CC itakutana leo kujadili mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba huku kikisema kuwa hakiyaungi mkono kwa asilimia mia moja mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu.
Kauli hiyo ya chama tawala ilitolewa na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana, baada ya kuulizwa na waandishi wa habari kuhusu msimamo wa chama chake juu ya rasimu mpya.
Kinana alisema uamuzi wa kutangaza msimamo wa chama utatokana na kikao cha CC), kitakachokutana leo chini ya mwenyekiti wake, Rais Kikwete.
“Kwa sasa hatuungi mkono rasimu hii kwa asilimia 100 wala kuipinga mpaka hapo tutakapokaa CC wiki ijayo (leo) na kuamua msimamo wetu ni upi katika hili,” alisema Kinana.
Alisema kila jambo ndani ya chama hicho huamuliwa kwa pamoja kupitia vikao na kwamba huo ndio utaratibu wao.
Wachambuzi wa mambo ya siasa wanaichukulia kauli ya Kinana ya kutounga mkono mapendekezo ya rasimu kwa asilimia mia moja kuwa alikuwa anamaanisha kwamba pendekezo kuhusu mfumo wa serikali tatu hawakukubaliani nalo.
Baadhi ya vigogo wa CCM wametoa maoni ambayo yanaonyesha wazi kuwa ndani ya chama hicho kuna mgawanyiko kuhusiana na suala hilo.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, anasema kuwa mchakato wa rasimu ya katiba umelenga kuvuruga Muungano na kuibebesha mzigo serikali.
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, anasema mfumo wa serikali tatu ni gharama kubwa ikilinganishwa na hali halisi ya pato la nchi.
Warioba ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu, anasema kama mfumo wa serikali tatu utakubalika, serikali ya Muungano haitakuwa na haja ya kukopa fedha na katika suala la uwakilishi wan chi kimataifa, Rais wa Muungano ndiye atakuwa na jukumu hilo na siyo Rais wa Tanzania Bara au wa Zanzibar.
Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela, anatahadharisha kuwa lazima suala la serikali tatu liangaliwe kwa umakini lisije kuleta matatizo.
Kauli hizo zinazokinzana, zinadhihirisha kuwa ajenda ya mfumo wa Muungano itazua mjadala mkali katika kikao cha leo cha CC.
Mfumo wa Muungano ni moja ya mambo ambayo serikali ya CCM imekuwa ikiyachukulia maamuzi kwa uangalifu mkubwa kama sera ya chama hicho.
Maoni yanayotolewa na vigogo wastaafu ynaweza kuleta ushawishi kwa vigogo wa CCM na kuamua kuitupa hoja ya serikali tatu kwa kuhofia yaliyowapata baadhi ya viongozi walioathiriwa na kushabikia mfumo wa serikali tatu.
Rais mstaafu wa Zanzibar, Alhaji Aboud Jumbe, mwaka 1984 alivuliwa nafasi zake zote za uongozi kutokana na kutaka mfumo wa serikali tatu.
Mapema miaka ya 90 suala la Muungano liliitikisa serikali ya awamu ya pili ya Ali Hassan Mwinyi, ilijikuta katika mtikisiko mkubwa, baada ya kuridhia kuundwa kwa serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.
Uamuzi huo ulitokana na shinikizo la kundi la wabunge 55 maarufu kwa jina la G55 ambalo lilikuwa linapinga uamuzi wa Zanzibar kuamua kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC) kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baada ya Bunge kupitisha hoja hiyo na serikali kuridhia, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliingilia kati kwa na kuwaambia wabunge wakiokuwa wakishinikiza kuundwa kwa serikali ya Tanganyika kusitisha hoja hiyo au wajiondoe ndani ya CCM.
Aliyekuwa waziri Mkuu, John Malecela na Katibu Mkuu wa CCM, Hayati Horace Kolimba, walivuliwa nyadhifa zao kwa madai ya kumshauri vibaya Mzee Mwinyi.
Wakati wa uongozi wa awamu ya tatu wa Rais Benjamin Mkapa suala la mfumo wa Muungano liliibuka upya, lakini alitumia nguvu kuzima mawazo ya kutaka serikali mbili.
Hata alipounda Tume ya kukusanya maoni chini ya uenyekiti wa Jaji Robert Kisanga kupitia utaratibu wa waraka maalum wa White Paper, Mkapa alikataa mapendekezo ya tume hiyo ya kupendekeza mfumo wa serikali tatu, akiwatolea lugha kali wajumbe wa tume kuwa hawakupewa adidu ya kutoa mapendekezo bali kukusanya maoni kuhusu Muungano.
MBOWE: KIFO CHA CCM CHAJA
Wakati huo huo; Mwenyekiti wa Chama Cha Demokreasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe, amesema CCM kimefikia ukomo wake kufuatia katiba mpya ambayo rasimu yake imetolewa na tume ya katiba hivi karibuni.
Akizungumza jana na wakazi wa Kata ya Iyela jijini Mbeya katika kampeni za uchaguzi mdogo wa kata ya hiyo ambao unatarajiwa kufanyika Juni 16 mwaka huu, alisema kufuatia muundo wa katiba inayokuja, CCM inaelekea kufa kutokana na katiba hiyo kuruhusu mgombea binafsi na serikali tatu.
Alisema kuwa viongozi wa chama hicho wamekuwa wakila fedha za walipa kodi wakiwa madarakani na ndiyo maana wamekuwa wakiutafuta uongozi kwa kasi kubwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment