ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 6, 2013

Mgombea wa CUF 'aangua kilio jukwaani

Mgombea wa udiwani wa Chama cha Wananchi (CUF) katika kata ya Elerai jijini Arusha, John Gilbert Bayo, ameangua kilio jukwaani wakati akinadi sera zake mbele ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Aliangua kilio hicho baada ya kuwaambia wakazi wa kata yake kuwa hakuwahi kupokea fedha kiasi cha Sh. milioni 50 kwa ajili ya kupata mwafaka wa umeya wa Jiji la Arusha kama wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wanavyodai na kuwa atakiuka maadili na kuwatosa wananchi watakapomchagua.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni hizo, Maalim Seif, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, aliwataka wakazi wa Kata ya Elerai kuwachagua wagombea wa CUF kwani chama hicho kimekuwa kikihimiza umoja na amani wakati wote. Maalimu Seif alisema, mgombea wa CUF katika kata hiyo ni mtu makini na mchapakazi na kuwa wao hawapo kwa ajili ya kumfukuza mtu bali wananchi ndio watakao amua hatma ya viongozi wanaowataka.
Alisema CUF ina imani na John Bayo kwa kuwa ndiyo chaguo la wananchi wa kata hiyo na kuwataka kumpa kura zote ili awe diwani wao na kusema hivi sasa Zanzibar imetulia baada ya mwafaka na hayo ni matunda ya chama hicho na kuwa hawatajuta kuchagua mgombea wa chama hicho kwenye kata zote waliosuimamisha wagombea.

Naye Bayo alisema kuwa akichaguliwa atapambana na kero mbalimbali zinazowakabili wakazi wa kata hiyo ikiwemo kutoa michango ya kununua madawati na majembe kila mwaka kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Aliwataka wakazi wa kata hiyo kuonyesha kuwa hakuchaguliwa na mafuriko ya Chadema kwa kumpigia kura ya ndiyo kwenye uchaguzi huo utakaofanyika Juni 16 mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: