ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 18, 2013

YANGA YAENDELEA KUJIFUA

Mshambuliaji kutoka nchini Nigeria Brendan Ogbu akiwania mpira na mlinda mlango Deogratius Munishi 'Dida' leo asubuhi katika mazoezi yaliyofanyika uwanja wa shule ya sekondari Loyola

Mabingwa wa Ligi kuu Tanzania bara 2012/2013 Young Africans leo imeendelea na mazoezi katika uwanja wa shule ya sekondari Loyola ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom inayotazamiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.

Ikiwa imeshatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara mara 24 tangu kuanzishwa kwake, ilianza maandalizi ya msimu mpya tangu mwanzoni mwa mwezi Julai kwa ziara ya wiki moja katika kanda ya ziwa ambapo ilicheza michezo mitatu ya kirafiki.

Kocha Mkuu wa Young Africans mholanzi Ernie Brandts mara baada ya mazoezi ya leo amesema anashukuru uongozi kwa ziara ya ubingwa ambayo ilimpa nafasi ya kuwaona wachezaji wake katika michezo hiyo ya kirafiki na kwa sasa anayafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika michezo hiyo.

"Unajua tulienda ziara tukiwa na wachezaji wapya na wengine chipukizi kutoka kikosi chetu cha U-20, hii ilitokana na wachezaji wetu 9 kuwa katika majukumu ya timu za Taifa hivyo ilikuwa ni nafasi kwangu kuwaona wachezji wapya na kuhakikisha sasa nawaandaa kwa ajili ya kutetea kikombe cha ubingwa msimu unaofuata na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa" alisema Brandts.

Katika hatua nyingine mshambuliaji kutoka timu ya Heartland ya Nigeria Brendan Ogbu amefanya mazoezi leo ikiwa ni siku yake ya pili katika mazoezi hayo ambapo makocha wa Yanga wamesema mchezaji huyo anayecheza nafasi ya ushambuliaji yupo katika kiwango kizuri na ni mchezaji anayeonekana kuwa na uzoefu mkubwa.

Young Africans inaendelea na mazoezi katika shule ya sekondari ya Loyola kila siku asubuhi saa 2 kamili amnapo kikosi hicho cha watoto wa Jangwani kinanolewa na kocha mkuu Brandts akiwa na wasaidizi wake Fred Felix Minziro na kocha wa makipa Razak Siwa.

No comments: