ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 3, 2013

Benki Azania kutoa huduma kuzingatia kanuni za Kiislam

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa (kulia), akishiriki hafla ya kufuturisha wateja wa Kiislam wa Benki ya Azania ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uhusiano baina ya benki hiyo na wateja wake msimu huu wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Na Mpigapicha Wetu

Dar es Salaam. Benki ya Azania imejipanga kuanzisha dirisha la kutoa huduma zinazofuata kanuni na misingi ya Kiislam.
Hayo yalielezwa juzi na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Charles Singili, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Benki ya Azania, Bernard Haule, kwenye hafla ya kufuturisha iliyoandaliwa na benki hiyo kwa wateja wake Waislam Dar es Salaam juzi.
“Tupo kwenye maandalizi kuanzisha huduma za benki kwa wateja wetu ambao ni waumini wa dini ya Kiislam, baada ya kuanza kutoa huduma kupitia mawakala miezi michache iliyopita,” alisema Singili na kuongeza:
“Tunaamini huduma hii itasaidia kuleta ahueni kwa wateja wetu Waislam. Dhamira yetu ni kuhakikisha wanapata huduma za kipekee zitakazokidhi matakwa yao kikamilifu.”
Alisema benki yake imekuwa ikiandaa hafla za kufuturisha wateja wake Dar es Salaam na mikoa mingine, ikiwa ni sehemu ya benki hiyo kujumuika pamoja na wateja wake hususan wakati wa Ramadhan.
Naye Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa Salum, aliwaasa Waislam nchini kuungana na kufuata misingi ya dini ya Kiislam.
“Waislam inatakiwa tutumie Ramadhan kwa kuzidisha upendo miongoni mwetu. Upendo huu usijengeke kwa Waislam pekee bali hata kwa wasio Waislam,” alisema.
Mwananchi

No comments: