Ni kuteleza kwa ULIMI au KIDOLE?
Sote tunafahamu
na kukubali kwamba katika mazungumzo hutokea mzungumzaji akateleza ulimi. Na
kwa vile siku hizi baadhi ya mazungumzo yanafanyika kwa kutumia keyboard, basi uwezekano wa kidole
kuteleza ni mkubwa sana. Wakati mazungumzo ya uso kwa uso huishia pale
yanapotokea, “mazungumzo” ya keyboard yanaifikia hadhira pana sana,
hadhira ya mtandaoni.
Huwa
ninachungulia sana katika majamvi na majukwaa ya Kiswahili ya mtandaoni kama
vile VIJIMAMBO BLOG na blogu nyinginezo na pia Jamii Forums – hususani Jukwaa
la Siasa. Na ni dhahiri kuwa “utelezaji” kati ya ‘r’ na ‘l’ na kati ya ‘ha’ na ‘a’ ni mkubwa sana. Ikumbukwe kwamba
katika Kiswahili hizi ni fonimu huru/sauti bainifu (phoneme), yaani kila moja
ina thamani ya kiisimu tofauti na nyingine na hivyo zikibadilishana nafasi basi
neno husika huwa na maana nyingine au maana yake huweza kupotoshwa. Katika
baadhi ya lugha za Kibantu kama vile Kihaya, fonimu hizi sio bainifu. Kwa hivyo
zinaweza kubadilisahana nafasi bila kuathiri maana ya neno au kikundi husika.
Kwa mfano, kikundi (cha maneno) buli kilo
na buri kiro kina maane ile ile (=
kila siku) kwa wazungumzaji wa lugha hii.
Pamoja
na ukweli kuwa washiriki katika mazungumzo ya Kiswahili wanaelewa mzungumzaji
anachomaanisha, je tunaweza kuudhibiti utelezaji huu ili kukuza na
kuhifadhi utumiaji sahihi wa Kiswahili – iwe katika maandishi au mazungumzo? Kwa maneno mengine, tukiendekeza utelezaji
huu, si kutokitendea haki Kiswahili?
Ushauri:
kwa vile tunatumia mitandao kuongea, kama mtu hana uhakika na tahajia
(spelling) za neno anaweza kuli-google na
tahajia sahihi itajibaini na hatimaye
atazoea kuliandika na kulitamka kwa usahihi.
Hapa
chini ni mifano hai michache ambayo nimeinukuu kutoka mtandaoni:
1. Kuna
tetesi za ndani nimesikia kutakuwa na mabadiriko ya wakuu wa wilaya nchi nzima wengine
watatoka na wengine watapangiwa sehemu zingine hii ni kutokana na wengine
kushindwa kumudu nafasi walizoteuliwa...... (JF)
2. ..wakati wa chama chashika hatamu, ukuu wa wilaya ulikuwa
ni cheo cha mtu wa dalasa la saba waliohitimu Hombolo au handeni.
sijui siku hizi kigezo ni kipi! (JF)
3. Post na Comments zako kwenye media zinajichanganya kiasi
kwamba watu wenye hakiri wanakushangaa. (JF)
4. Huwa napata raha sana JF, hapo mwenzenu ndo kaona
kajipaaaaanga, akatafakari na kufikiri kwa akili yake yoooote (kwa sababu
naamini kiongozi, hasa mwanasiasa huwa anafanya hivo kulinda status kabla
hajaongea) alafu
comments zikianza anagundua akili ndogo kuongoza kubwa ni kazi sana! (JF)
5. Baadhi ya Wanafunzi wa Chuo cha Dipromasia, wakijisevia futari
wakati wa hafla hiyo ya futari ya pamoja iliyoandaliwa na Mke wa Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Asha Bilal, kwa wanafunzi hao. (VIJIMAMBO: Agosti 4, 2013) (Hili neno lilirudiwa mara
tisa katika habari husika!)
6. Pamoja na kumkubari Dr Slaa kwa kuonyesha kuwa anaweza kuisaidia
nchi yetu kutuondoha
katika umaskini lakini amekosea kumkosoa Kikwete hadharani na kumpa kichwa Paul
Kageme, hata kama ni mpinzani lakini kwa mambo ya kitaifa kwa masalahi ya nchi
lazima tuwe pamoja, hata kama Rais wetu amekosea basi tusichukulie swala hili
kuwapa faida adui zetu. (JF)
7. Mkuu nakuhunga mkono, hoja hii inapashwa kujadiriwa
kwenye kikao cha Bunge cha mwezi huu - ukaribu wa Marais hawa watatu si jambo
la kupuuzia kwa usalama wa Taifa letu na Rais wetu, jamaa hawa kuna vitu
wanapanga behind the scene, (JF)
8. Kufuatia agizo la Mhe. Rais la kuwataka watu wote
wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kusalimisha silaha hizo, pamoja na watu
wote wanaoingia ama kuishi na kufanya shughuli hapa nchini bila kufuata
utaratibu (wahamiaji haramu) kutakiwa kuondoka au kuharalisha ukaazi wao, Jeshi la
Polisi linawataka watu hao kuendelea kutekeleza agizo hilo la Serikali kabla ya
Operesheni kabambe kuanza itakayoendeshwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana
na Vyombo Vingine vya Ulinzi na Usalama.
Imetolewa
na:-
Advera Senso- SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi. (Agosti 6, 2013)
9. …halafu
hivi Zanzibar inaweza kweli kubadiri mitizamo ya Wakristo wa Bara kweli? watu
wenyewe wako wangapi? Jimbo la Ubungo au hata Magomeni, Nyamagana yana watu
wengi zaidi kuliko Zanzibar yote, ushawishi gani Zanzibar inaweza kuufanya Bara
ili bara ibadiri
maamuzi? (JF)
10.
Watanzania tusikubari
maslahi ya watu binafsi na siasa za wagawanye-watawale zitawale.. (sehemu
ya kipeperushi klichobandikwa katika Blogu ya MICHUZI, 8/8/13. Mwandishi
angeweza kujipa nafasi ya kuhariri kabla ya kukibandika)
(Charles Bwenge, cbwenge@ufl.edu
)
No comments:
Post a Comment