Ile nyumba ambayo mke wa Hance alikuwa anajivunia, haipo tena. Kaka wa mwanamke huyo (yaani shemeji yake Hance), aliiuza kwa madai kwamba ni mali ya dada yake.
BAHATI MBAYA
Wanawake wa kundi hili, kwa bahati mbaya huwa na bahati ya kupata wanaume wanaowapenda lakini mapenzi huwa hayadumu, chanzo kikiwa ni fedha. Kauli yao kuu ni kwamba hawataki mwanaume suruali, wao huhitaji wanaoweza kutoa.
Bahati mbaya nyingine ni kuwa hata kama unajiweza, ukajitoa muhanga na kumtwaa, tambua kuwa wewe siyo tajiri nambari moja, atatokea anayekuzidi kipato na atajimilikisha bila woga. Wewe utaitwa mpenzi/mume jina, mwenzako atapata huduma zote muhimu.
Kama wewe ni mjenzi wa maisha ya kesho na familia yako, utaambulia matusi, dharau na kejeli. Utaitwa bahili, hujui kuhudumia na maneno mengineyo yasiyo na tafsiri nzuri. Kwa kifupi ni kwamba unatakiwa kumsoma mwanamke wako mapema na ukishagundua ana sifa za wanawake wa kundi hili, hebu fanya kung’atuka mapema.
Vile walivyonena wahenga kwamba mja asili hasahau asili au jasiri hasahau asili, mwanamke mwenye wasifu wa kundi hili, hata akiolewa wakati mwingine tabia zake huwa kama changudoa. Huonesha mapenzi ya juu zaidi kwa mumewe anapopewa fedha, vilevile mahaba hufifia au kupotea kabisa kipindi cha ukata.
KUNDI LA NNE
Kundi hili ambalo nimeliteua kuwa la mwisho, linawahusu wanawake ambao kila mwanaume anaota kuwa nao. Inawezekana nao wakawa wanakutana na misukosuko ya kimapenzi ya hapa na pale, yaani nao wanaumizwa na wanaachwa, hilo lisikushangaze, kwani dunia ni tambara bovu.
Upo msemo mwingine kuwa palipo na miti mingi hakuna wajenzi. Kwamba wakati asilimia kubwa ya wanaume wanaota wangekuwa na wake mithili ya wanawake wanaounda kundi hili, kuna wengine wanawachezea, hawajui thamani yao.
Bado nasisitiza kuwa hutakiwi kushangaa, kwani kuna anayejuta hivi leo baada ya kugundua kuwa alipiga teke almasi wakati alipokuwa ‘bize’ kukusanya mawe. Wanawake wa kundi hili, huwa na faida kubwa pale wanapokutana na wanaume sahihi zaidi katika maisha ya kimapenzi.
Ukipenda unaweza kuwaita ‘wife materials’, kwa maana hawa ni wanawake ambao wanakuwa wameshapevuka kimawazo na mtazamo kuhusu mapenzi na maisha kwa jumla. Hawaangalii sura, mavazi, fedha wala starehe, bali huzingatia yule ambaye anaweza kumfanya ajione yupo salama, vilevile atakayejenga naye maisha.
Zingatio lao ni amani, furaha, upendo, usalama na maisha. Mwanaume anayeshindwa kumpa mwanamke vitu hivi, hujiwekea doa bila mwenyewe kujua. Jambo zuri zaidi kwa wanawake wanaounda kundi hili ni kwamba wao ni walimu, halafu ni wavumilivu wakubwa.
Kwa kawaida ni wagumu kuingia kwenye uhusiano lakini wakishanasa ni ngumu sana kuchomoka. Wakishaingia wameingia, hata wanaume wakiwa majanga, wao huvumilia. Ukiona wameacha, ujue ama wameona pale alipo hakuna sura njema ya kimaisha au wamepata ushawishi wenye matarajio ya faraja.
Wanawake wa kundi hili huhitaji wanaume ambao kipaumbele chao ni maisha. Mara nyingi ni wachapakazi na hupigania kushirikiana na waume zao katika kujaza pato la familia. Ni walezi wazuri wa watoto, inapotokea waume zao kushindwa kuwajibika ipasavyo kwa namna yoyote ile.
Inawezekana mwanaume ametelekeza familia, anasumbuliwa na maradhi yanayomfanya ashindwe kutafuta riziki, amefariki dunia au amekumbwa tu na msukosuko wa kiuchumi, mwanamke wa kundi hili hubaki imara na kuhakikisha familia inaendelea kupata mahitaji muhimu.
Wanawake wa kundi hili, siyo kila mara wanaweza kuwa wafanyakazi au wafanyabiashara. Wengine ni akina mama wa nyumbani lakini uwezo wao ni mkubwa katika kudhibiti matumizi, kupanga maendeleo na kusimamia familia, kuanzia kwa baba mpaka watoto.
Hawa ndiyo huipa nguvu ile tafsiri kwamba nyuma ya kila mwanaume aliyefanikiwa, yupo mwanamke imara, aliyetia msukumo wa hayo mafanikio. Mara nyingi si watu wa kujikweza na kukimbilia mahitaji ya gharama kubwa, huonekana wa kawaida kwa faida ya familia zao.
Itaendelea wiki ijayo.
Global Publishers
No comments:
Post a Comment