Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, katika Kanda ya Maziwa Makuu, Bi. Mary Robinson, ameanza ziara maalum katika DRC na Kanda ya Maziwa Makuu akiongoza ujumbe mzito unaolenga kutafuta suluhu ya kidiplomasi baada ya kurejea upya kwa mapigano makali katika eneo la Mashariki mw DRC hali ambayo imelifanya eneo la Maziwa Makuu kuwa katika wasiwasi. Mapigano ya wiki iliyopita yalikuwa baina ya Kundi la waasi la M23 na FARD ambayo ni Majeshi ya DRC yakisaidiwa na Majeshi ya Kulinda Amani ya Umoja wa Mataifa katika DRC ( MONUSCO) Ujumbe wa Bi. Robinson unawahusisha wawakilishi kutoka AU, EU, USA na UN
Na Mwandishi Maalum
Kufuatia kurejea tena kwa mapigano makali yaliyotokea wiki iliyopita kati
ya majeshi ya Serikali ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo ( FARD)
yakisaidiwa na Jeshi la MONUSCO na kundi la
waasi la M23. Umoja wa Mataifa sasa unajaribu kutafuta suluhu ya kidiplomasia
inayolenga katika kujaribu kuweka sawa
hali ya mambo.
Mapingano hayo ambayo siyo tu
yanasadikiwa kuliondoa kundi la M23
katika ngome yake ya vilima
vya Kibati Magharibi ya Kivu. Yamelaaniwa vikali na Baraza Kuu la Usalama
la Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu Ban
ki Moon hasa baada ya kundi hilo la M23
kusababisha kifo cha mwanajeshi Mtanzania na kujeruhi wengine kumi
wakiwamo wanajeshi kutoka Afrika ya
Kusini.
Mchakato huo wa kisiasa
unafanywa na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
katika Kanda ya Maziwa Makuu, Bi. Mary
Robinson, ambaye amewasili katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo siku
ya jumapili na kutoa rambirambi zake kwa wahanga wa mapigano hayo.
Taarifa kutoka ofisi ya
Mjumbe huyo Maalum, inataarifu kwamba, Katika mchakato huo wa kutafuta suluhu ya kidiplomasia ,
Mary Robinson ataongoza
ujumbe maalum utakaowahusisha Mwakilishi wa
Umoja wa Afrika, Bw. Boubacar
Diaraa, Bw. Russ Feigold, ambaye ni
Mjumbe Maalum wa Serikali ya Marekani katika Eneo la Maziwa Makuu, Bw. Martin Kobler Mwakilishi
Maalum wa Katibu Mkuu katika DRC na Mkuu wa MONUSCO, wakati Jumuiya ya Ulaya
itawakilishwa na Mratibu Mwandamizi
katika Maziwa Makuu, Bw. Koen Vervaeke.
Kabla ya kuungana na ujumbe huo, Bi. Mary Robison
atafanya mazungumzo ya ndani na
washirika wa Umoja wa Mataifa katika DRC na kisha atakwenda Goma kama hatua ya kuonyesha mshikamano wake
na wananchi wa eneo hilo na Jeshi la Kulinda Amani
la Umoja wa Mataifa ( MONUSCO).
Kwa mujibu wa Ofisi ya
Bi Mary Robison ziara ya Mjumbe huyo na ujumbe wake, pamoja na kutembelea DRC pia watakwenda Uganda na Rwanda kati ya Septemba 4-7, ambapo pamoja na mambo mengine watakutana na kufanya mazungumzo na viongozi
waandamizi wa Serikali Kuu pamoja na Serikali za Mitaa, wawakilishi wa Jumuiya
ya Kimataifa na Mashirika ya Kiraia pamoja
na kuhudhuriwa kikao cha dharura cha Mkutano wa Kimataifa wa Kanda ya Maziwa Makuu ( IGCLR).
Taarifa hiyo
inabainisha kwamba akiwa katika nchi hizo, Bi. Mary Robinson atasisitiza haja
na umuhimu wa pande zinazohusika kusitisha vitendo vya uhasama na kuelekeza nguvu zao katika majadiliano ya kisasa pamoja na mchakato wa Kampala ( Kampala Process).
Aidha inaelezwa
kwamba wakati Bi. Robison na ujumbe wake watakapohudhuria mkutano
wa IGCLR
utakaofanyika Septemba
5 jijini Kampala, watahimiza
uharaka wa utekelezaji wa Mpango Mpana
wa Kisiasa wa Umoja wa Mataifa kuhusu amani, usalama na maendeleo katika DRC na
Eneo la Maziwa Makuu, mpango ambao
ulisainiwa mapema mwaka huu na nchi 11 na wadhamini wanne wa kimataifa .
Ziara hiyo ya Bi. Mary Robison na ujumbe wake inafuatia kurejea upya kwa mapigano makali katika eneo
la Mashariki ya DRC mapigano ambayo yameifanya hali
ya mambo katika eneo la Maziwa
Mkuu kuwa tete, huku kukiwa na
ongezeko kubwa la wakimbizi, hali inayochagiza uharaka wa kutafuta suluhu ya kisiasa ili kurejesha hali
ya utengamano katika DRC na eneo la Maziwa Makuu.
No comments:
Post a Comment