NIANZE kwa kukusalimu shoga yangu. Usije ukaanza maneno maneno ooh, Chau hasalimii watu. Aku, majungu yapikwe hukohuko, mimi nimefunzwa nikafunzika, nimefundwa nikafundika, simpiti mtu bila salamu, Abadan!
Bi. shosti wewe umezoea kusikia tu rais, mawaziri, wakuu wa mikoa na kadhalika wakifanya ziara za kushtukiza. Kwa taarifa yako hata mume, mchumba au buzi lako linazo zake. Tabia ya kujisahau na kujiachia, utaumbuka.
Sitaki unilaumu kwamba Chau hakunitahadharisha hili, kwa hiyo chukua hili somo. Kuna mwenzenu kapewa talaka, alizoea mume yupo mbali, katoka kwenda viwanja, karudi alfajiri kakuta mume kajaa tele kitandani. Aibu na talaka juu yake.
Mada hii inawahusu sana wale mashoga zangu ambao wanaishi mbali na waume zao. Pengine kwa sababu za kikazi au masomo. Vilevile inawachoma moja kwa moja wanawake walioolewa ndoa za mitala.
Kwako wewe uliyeolewa ndoa ya mtala, kuna tabia ya kupeana zamu kati ya mke mkubwa na mdogo. Chunga sana jambo hilo, maana mume hakawii kukatisha ziara ghafla akaja kwako. Sijui itakuwaje kama utakuwa umeutumia muda wako vibaya!
Hapa ndipo nataka nitoe somo haswa kwa sababu wengi wamejisahau. Mwanamke hafanyi usafi mpaka asikie mume anakuja nyumbani kwake, haya ni makosa makubwa. Unatakiwa kukaa msafi wakati wote kwa imani kwamba lolote linaweza kutokea.
Ni tabia mbaya sana kubweteka, wapo ambao hawaogi kabisa. Anaweza kukaa siku nzima mpaka jioni hajaoga. Akisikia mume anarudi ndiyo anaoga.
Utakuta mwanamke ameweka kibustani chake kichafu anasubiri kukipalilia siku akisikia mume anakuja, hivi akikujia usiku ghafla umelala utafanya nini? Huoni kama ni aibu? Je, akikuacha utamsingizia nani?
Wanaume wengine wamezoea kuwasaidia wake zao kupalilia bustani lakini utakuta wakati mwingine mume ana mambo mengi kwa nini umtegee yeye kila siku? Nawe palilia siku mojamoja akukute uko tayari ili akipita kuvuna mboga apite kirahisi.
Mwanamke mwenzangu uwe na diploma, digrii au hata ukiwa na fedha nyingi. Sifa ya mwanamke jasiri ni yule anayezingatia usafi. Kama wewe upo vizuri, sidhani kama unaweza kutetereka kama mumeo atakufanyia ziara ya kushtukiza.
Epuka tabia ya kupika mahanjumati wakati mumeo yupo nyumbani tu, halafu asipokuwepo unatengeneza chakula ilimradi tu watu wale. Hiyo siyo sawa, jiweke tayari kama mwanamke, ifanye nyumba yako iwe na thamani. Kama kuna watoto wawe wanafurahi muda wote.
Wanawake wengi wakijua waume zao hawapo, eti wanaamua kula chipsi au anafunga jiko, analala ndani akingojea chakula cha mama ntilie au mkate, mwanamke unapoteza sifa ya kuitwa mke jishughulishe mama utaachwa.
Kumbuka mwanaume mtundu mara nyingi anakuwa na vipimo mbalimbali kwa nyumba yake, hasa kwa wale walio kwenye uke wenza, kama wewe mke mkubwa unakuwa mvivu, hufanyi mazuri mpaka mume awepo itakula kwako bibi.
Wewe mke mkubwa yakikukuta utasingizia mwenzako analoga, si bure kamuweka kwenye chungu jalalani, kabla ya kuongea hayo hebu jaribu kujipeleleza mwenyewe na ujiulize, usitafute mbaya, mchawi wa ndoa yako ni wewe mwenyewe.
Mwanamke hujifushi udi, huvai asmini na vilua, wewe upoupo tu unasubiri mume akikwambia kesho nakuja ndiyo ujifanyishe, mume atakukimbia, shauri yako.
Global Publishers
2 comments:
I like this. it's entertaining and educational
Acheni kufanya wanawake watumwa wa Wanaume.
Huyu mwanaume yeye anamfanyia nini huyu mwanamke???
Kwani akimuacha yeye ni Mungu.
Post a Comment