Cheka anatarajia kusoma masomo ya Kiingereza na Biashara.
Dar es Salaam. Leo bingwa wa dunia wa WBF, Francis ‘SMG’ Cheka ataandika historia mpya ya maisha yake kwa kuanza rasmi masomo yake ya awali ya sekondari katika shule ya St Joseph mjini Morogoro.
Cheka anayepigania uzani wa super middle (kg 76) alifikia uamuzi wa kurudi shule baada ya kupewa ufadhili na Shule ya Sekondali ya St Joseph.
“Sijui masomo yatakuwaje, lakini vyovyote itakavyokuwa nitapambana nayo kwani uamuzi wa kurudi shule umetoka moyoni hivyo sitateteleka, lakini kabla ya kwenda shule nitaanza mazoezi kwanza,” alisema Cheka katika mahojiano na Mwananchi.
Cheka baba wa watoto wawili, Boniface na Historia anadai alikuwa na ndoto za kujiendeleza kielimu tangu zamani japo alishindwa kutokana na majukumu ya kifamilia.
“Naenda kusoma kweli, sitafanya mzaha hata kidogo kwenye masomo yangu, pia sitaacha kufanya mazoezi kwani Desemba natakiwa kutetea taji langu la dunia,” alisema bondia huyo asiyekamatika hapa nchini kwenye ngumi za kulipwa.
Cheka alihitimu elimu yake ya msingi miaka kadhaa iliyopita Shule ya Msingi Kinondoni B, Dar es Salaam ambapo kwa mujibu wa bondia huyo hakubahatika kuendelea kutokana na matatizo ya kifamilia na kujikita kwenye ngumi za ridhaa wakati huo kabla ya mwaka 2000 kujiunga rasmi kwenye ngumi za kulipwa.
Tangu wakati huo amefanikiwa kutwaa ubingwa wa taifa, mataji ya Afrika ya UBO, IBO, IBF, WBC na WBO kabla ya mwishoni mwa Agosti mwaka huu kutwaa ubingwa wa dunia wa WBF baada ya kumpiga Phil Williams wa Marekani kwa pointi, Dar es Salaam.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment