Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akisalimiana na Naibu Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Mambo ya Nje na Jumuiya ya madola, mhe. Mark Simmonds walipokutana kwa mazungumzo Mjini New York wakati wa Kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Ujumbe ulioambatana na Mhe. Simmonds.
Mhe. Membe akizungumza na Mhe. Simmonds kuhusu masuala ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.
Ujumbe wa Tanzania wakati wa mazungumzo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Balozi Dora Msechu, akifuatiwa na Bi. Tully Mwaipopo, Bw. Grayson Ishengoma na Bw. Togolani Mavura Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) ameishukukuru na kuipongeza Serikali ya Uingereza kwa kuanzisha huduma mpya itakayowawezesha Watanzania kupata viza za kuingia nchini humo kwa haraka.
Huduma hiyo ambayo ilitangazwa na nchi hiyo hivi karibuni kupitia Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Mhe. Diana Melrose ni moja ya mipango ya nchi hiyo ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizi mbili. Huduma hiyo hukamilika kwa takribani siku tano hadi kupata viza.
Akizungumza hivi karibuni na Naibu Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Mambo ya Nje na Jumuiya ya Madola, Mhe. Mark Simmonds Mjini New York, Marekani wakati wa Kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Mhe. Membe alisema kuwa anaishukuru nchi hiyo kwa kuichagua Tanzania katika mpango huo ikiwa ni mshirika wake muhimu wa maendeleo na kwa kuzingatia kuwa uchumi wa Tanzania unakua kwa haraka katika siku za hivi karibuni hivyo itarahisisha na kuimarisha biashara baina ya nchi hizi mbili.
Aidha, Mhe. Membe aliongeza kuwa Watanzania wengi wamekuwa wakijishighulisha na biashara mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwemo Uingereza hivyo mpango huo wa viza za haraka utawasaidia kuimarisha biashara zao badala ya kukatishwa tamaa na mlolongo mrefu wa kufuatilia viza uliokuwepo hapo awali.
“Tunaishukuru sana Serikali ya Uingereza kwa kuanzisha huduma hiyo ya utoaji viza za haraka, hata hivyo bado tunaiomba ifikirie tena uwezekano wa kurejesha huduma ya utoaji viza Jijini Dar es Salaam badala ya kufuatilia viza hizo Nairobi nchini Kenya”, alisema Waziri Membe.
Aidha, aliomba kiwango cha nyongeza kilichowekwa cha shilingi laki mbili na nusu kwa ajili ya kukamilisha mchakato wa viza hiyo ya haraka kipunguzwe kwani ni kikubwa kwa Watanzania.
Akizungumza kwa upande wake, Mhe. Simmonds alisema kuwa Uingereza itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania hususan katika masuala ya biashara na uwekezaji.
Mkutano huo wa Mhe. Waziri Membe na Mhe. Simmonds ulihudhuriwa na Wajumbe wengine akiwemo Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Dora Msechu.
No comments:
Post a Comment