Loliondo. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ametengua tangazo la Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki la kuligawa eneo la Pori Tengefu la Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha kwa kutenga kilomita za mraba 1,500 kwa ajili ya uhifadhi na kilomita za mraba 2,500 kuwa chini ya Serikali za vijiji.
Machi 19, mwaka huu, Waziri Kagasheki alitoa tangazo la Serikali la kuligawa pori hilo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 4,000 ili Serikali iweze kuhifadhi eneo la kilomita za mraba 1,500 ambalo alieleza kuwa ni mapito na mazalia ya wanyamapori, pia kutunza ikolojia ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Tangazo hilo liliibua mgogoro mkubwa.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika eneo la Waso jana baada ya kutembelea eneo la mgogoro na kufanya kikao na ujumbe wa mawaziri alioambatana nao na watendaji wa wizara mbalimbali, Waziri Mkuu alisema amefikia uamuzi wa kuondoa tangazo hilo la Serikali na sasa wananchi wa eneo hilo wataendelea na utaratibu uliozoeleka.
Mawaziri waliokuwa katika ziara hiyo ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Naibu Waziri wa Maji, Dk Binilith Mahenge, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Benedict Ole Nangoro na Naibu Waziri (Tamisemi), Kassim Majaliwa.
“Mara baada ya lile tangazo kuliibuka mgogoro wa wananchi kupinga na baadhi ya viongozi walinifuata hadi Dodoma na kuniletea malalamiko yao. Pia CCM iliunda tume na kunipa taarifa lakini nikasema siwezi kutoa uamuzi hadi nifike mwenyewe katika eneo hili na sasa nakubaliana na hoja za wananchi kuwa kuligawa eneo kutakuwa na athari kwenu, naomba sasa mwendelee na utaratibu wenu kama vile halikuwepo tangazo hilo,” alisema Pinda.
Alisema miongoni mwa hoja za wananchi zilizosababisha afikie uamuzi huo, ni kuwa eneo hilo la kilomita za mraba 1,500 ndilo ambalo lina vyanzo vya maji vinavyotegemewa na vijiji vyote sita ambavyo vingeathiriwa na tangazo hilo. Vijiji hivyo ni Ololosokwani, Soitsambu, Olorieni Magaiduru, Arash, Piyaya na Oloipili.
Waziri mkuu pia alisema eneo hilo lililotengwa kwa uhifadhi ndilo tegemeo la wananchi kwa ajili ya malisho ya mifugo hasa nyakati za kiangazi, pia kuna makazi ya watu, shule na huduma nyingine muhimu.
Alisema kutokana na uamuzi huo, Serikali inajipanga kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika wilaya hiyo ili kutambulika maeneo ya ufugaji, makazi, kilimo na uhifadhi ili masilahi ya kila upande yaendelee kulindwa.
“Utaratibu wenu mliojiwekea kabla ya tangazo la Serikali uendelee kwani tunataka shughuli za uwindaji wa kitalii ziendelee, upigaji picha uendelee, pia ufugaji uendelee na hapa ni vyema kukawa na vikao vya wadau wote walau kila baada ya miezi mitatu,” alisema Pinda.
Waziri Mkuu aliagiza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Halmashauri ya Ngorongoro kuratibu vikao hivyo kwani lengo ni kutatua migogoro na kurejesha uhusiano.
Wakazi Loliondo vicheko
Mara baada ya Waziri Mkuu kutangaza uamuzi huo, shangwe zilitawala na Mbunge wa Ngorongoro, Saning’o ole Telele na madiwani wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri, Elias Ngolisa walieleza kuridhishwa na uamuzi huo wakisema umezingatia kilio cha mamia ya wananchi wa Tarafa za Loliondo na Sale.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Ortello Business Co operation (OBC), ambayo ingebaki katika eneo lililokuwa limetengwa kwa uhifadhi, Isack Mollel alisema hapingi uamuzi huo lakini anataka mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) wilayani Ngorongoro, kukubali mwafaka huo pia kushiriki katika vikao vya kupanga matumizi bora ya ardhi vijijini muda ukifika.
Hata hivyo, kabla ya kutangazwa kwa uamuzi huo, Mollel alisema Serikali isipotenga sasa maeneo ya uhifadhi na ufugaji, shughuli za utalii zitakufa Loliondo sambamba na kuathirika eneo zima la ikolojia la Serengeti kwani mifugo imeongezeka na imeanza kuingia hadi ndani ya Hifadhi ya Serengeti.
Profesa Tibaijuka atoa suluhu
Awali, Profesa Tibaijuka alisema suluhu ya migogoro ya ardhi Loliondo ni kuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi baada ya vijiji kupimwa kazi ambayo alikwishaianza.
Alisema umefika wakati pia kwa wafugaji wa Loliondo kupunguza mifugo na kuanza kufuga kisasa kwani ardhi haiongezeki.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment