`Haiwezi kusikilizwa` kikanuni
Juzi uongozi wa klabu ya Yanga ulisema kuwa umewasilisha rufaa TFF kuomba mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya 1-1 irudiwe katika uwanja huru kutokana na vurugu zilizotokea kabla na baada ya kuanza kwa mechi hiyo.
Akizungumza katika mahojiano maalum na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema hadi jana alasiri shirikisho hilo lilikuwa halijapokea rufani hiyo ya Yanga.
"Tumesikia kupitia vyombo vya habari kwamba Yanga wanawasilisha rufani mechi yao ya juzi (Jumamosi) irudiwe lakini mpaka sasa (saa 9:14 alasiri) hatujapokea barua yoyote kutoka kwao," alisema Osiah.
Afisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto aliliambia gazeti hili jana jioni kuwa waliwasilisha rufani yao kwa njia ya barua pepe kwa Osiah na kwamba hawakulipia ada ya rufaa hiyo.
"Kamishna wa mechi alikuwa hapatikani, tukaamua kuwasilisha rufani yetu kwa njia ya 'email' kwa Katibu Mkuu wa TFF (Osiah)," alisema Kizuguto.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo ya Yanga, Osiah alijibu kifupi kwa kusema; "Kanuni zinaelekeza nini kuhusu rufani za mechi? Walituma kwenye 'email' yangu kama mtu binafsi au shirikisho?"
KANUNI ZA LIGI
Kanuni ya 6 ya Kanuni za Ligi za TFF inataka rufani ya kupinga matokeo iwasilishwe kwa kamishna wa mechi au ofisi za shirikisho hilo ndani ya saa 24 baada ya mchezo huo kumalizika ikiwa imeambatanishwa na ada yake ambayo kwa mujibu wa Kanuni ya 17(a) cha Kanuni za Ligi ni Sh. 300,000.
"Kamishna wa mchezo atawasilisha kwenye Sekretarieti ya TFF siyo zaidi ya saa ishirini na nne (24) tangu kupokea rufaa hiyo. Rufani yoyote itakayowasilishwa baada ya muda uliowekwa chini ya kanuni hii (Kanuni ya 6), haitasikilizwa na ada ya rufaa haitarudishwa kwa mrufani," inaeleza sehermu ya Kanuni ya 6 ya Kanuni za Ligi za TFF.
"Kamati husika itaketi kusikiliza na kuitolea uamuzi rufaa hiyo katika kipindi kisichozidi wiki tatu, baada ya kupata vielelezo husika na wajumbe wa kamati hiyo kukamilika. Mkata rufaa atawasilisha vielelezo kuhusu rufaa yake, rufaa isiyokuwa na vielelezo na ambayo haijalipiwa ada itatupwa," inaeleza zaidi kanuni hiyo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment