ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, September 25, 2013

Sh. milioni 45 chungu kwa Ngasa

Shilingi milioni 45 Mrisho Ngasa alizotakiwa kuilipa Simba, zimegeuka kuwa chungu kwake baada ya klabu ya Yanga kukubali kulipa deni hilo lakini kwa sharti la winga huyo kuitumikia hadi Mei 2018.

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), ilimpa Ngasa adhabu ya kutocheza mechi sita msimu huu pamoja na kumtaka ailipe Simba Sh. milioni 45 baada ya usajili wake kuleta utata kutokana na kujisajili klabu mbili tofauti, Simba na Yanga.

Katika shilingi hizo milioni 45, Sh. milioni 30 ni alizopewa kama ada ya usajili Simba, wakati ambapo Sh. milioni 15 zikiwa ni asilimia 50 ya faini ya kiasi hicho cha fedha alichopokea.

Tayari Ngasa amemaliza adhabu ya kwanza ya kutocheza mechi sita msimu huu ambapo alianza kwa kuikosa ile ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC na kisha tano za Ligi Kuu Bara wakati Yanga ikicheza dhidi ya Ashanti United, Coastal Union, Mbeya City, Tanzania Prisons na Azam FC.


Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto aliliambia NIPASHE jijini Dar es Salaam juzi kuwa, suala hilo kwa sasa haliko chini ya klabu yao, bali ni la Ngasa mwenyewe.

"Maamuzi yaliyotolewa na Shirikisho la Soka nchini (TFF), yanamtaka Ngasa na si klabu ya Yanga kulipa fedha hizo. Klabu ilikata rufaa kupinga maamuzi ya kumfungia mechi sita na si suala la kulipa fedha hizo," alisema Kizuguto.

Lakini wakati Kizuguto akiyasema hayo juzi, jana Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, wapo tayari kumsaidia Ngasa kulipa deni hilo ila kwa masharti mawili.

"Kwanza akubali kukatwa kiasi hicho kidogo kidogo katika mshahara wake hadi deni hilo litakapomalizika, ama aridhie kuingia mkataba mwingine wa miaka mitatu," alinukuliwa Mwalusako.

Nipashe lilimtafuta Ngasa jana ili kujua endapo atakubali masharti hayo ama la, lakini alipoulizwa alisema suala hilo lipo mikononi mwa klabu na kwamba hayupo tayari kulizungumzia kwa sasa.

Hata hivyo, rafiki yake wa karibu aliliambia gazeti hili kuwa Ngasa amekubaliana na uamuzi huo na kwamba hawezi kupinga kwa sababu anataka kucheza soka.

"Soka ni maisha yake. Amesema hana ujanja wa kupindua uamuzi huo kwa kuwa kinyume na kufanya hivyo, itamlazimu kuendelea kukaa benchi hadi atakapolipa deni hilo la Simba kama alivyotakiwa kufanya na Kamati ya TFF," alisema rafiki huyo huku akiomba hifadhi ya jina lake kwa kuwa yeye si msemaji wake.

Kwa mantiki hiyo, kama Ngasa atakubaliana na uamuzi huo na kusaini mkataba mpya wa miaka mitatu, atalazimika kuitumikia Yanga hadi Mei 2018 kwani ule wa awali aliosaini majira haya ya joto ulikuwa wa miaka miwili na ulitarajiwa kumalizika Mei 2015.

Endapo Yanga itakamilisha taratibu za kulipa deni hilo kabla mechi yao ya Jumamosi, basi siku hiyo mashabiki wa klabu hiyo watamshudia Uwanja wa Taifa akiwa amevalia uzi wa kijana na njano kuivaa Ruvu Shooting.

Lakini hilo pia litategemeana na uwamuzi wa kocha Ernie Brandts endapo atamuona yupo 'fiti' kucheza mechi hiyo.

Hata hivyo, Simba na Ngassa wana kila sababu ya kuishukuru Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, kwa kutumia busara katika kulitolea uamuzi suala hilo.

Kitendo alichokifanya Ngassa kwa kujisajili klabu mbili, alitakiwa kuhukumiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 44 (3) cha Kanuni za Ligi za TFF na Sura ya IV Ibara ya 17 (4) cha Kanuni za Fifa, ambapo winga huyo alipaswa kufungiwa kucheza soka kwa mwaka mzima huku klabu ya Simba ikistahili kifungo cha misimu miwili mfululizo pasipo kusajili wachezaji wa ndani na nje.

"Klabu inayomshawishi mchezaji kumsajili wakati akiwa na mkataba na timu nyingine kwa kusaini au kuvunja mkataba wake na klabu hiyo pasipo kuitaarifu klabu husika, itafungiwa na chama cha soka cha nchi husika kusajili wachezaji wa ndani na nje kwa misimu miwili mfululizo," inaeleza Sura ya Nne Ibara ya 17(3) cha Kanuni za Fifa.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments: