ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 16, 2013

Simba yaifunga mdomo Mtibwa


Simba ilipata ushindi wake wa pili mfululizo katika mechi tatu za ligi kuu ya Bara jana, ilipoifunga Mtibwa Sugar 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa na kufikisha pointi saba.

Lakini ushindi huo ulikuwa na maanza zaidi kwa Wekundu wa Msimbazi ambao walifanikiwa kuzima wimbi la kufungwa mechi mbili mfululizo zilizopita na walima miwa hao wa Manungu, mkoani Morogoro.

Bao la kwanza la Simba lilifungwa na Henry Joseph katika dakika ya 70 kwa kichwa ikiwa ni chini ya robo saa tangu aingie uwanjani kuchukua nafasi ya Said Hamisi.

Henry ambaye alisajiliwa Simba dakika za majeruhi za dirisha lililopita la usajili aliporudi nyumbani kutoka kuchezea Kongsvinger ya daraja la pili nchini Norway, alipiga kichwa hicho baada ya mpira wa kona ya Issa Rashid kuwababatiza mabeki wa Mtibwa karibu na lango.

Mchezaji mwingine mpya Betram Mwombeki kutoka Pamba ya Mwanza aliihakikishia Simba ushindi baada ya kufunga bao la pili katika dakika za majeruhi.

Mtibwa Sugar wakiamini watatoka uwanjani na matokeo yenye heshima, ya dalili za ushindi wa taabu kwa Simba, Mwombeki alifunga kwa shuti kali la mguu wa kushoto kutokana na pasi ya Ramadhani Singano aliyenzia benchini pia.

Kocha wa Mtibwa Mecky Mexime alisema timu yake ilijisahau kipindi cha pili na kuruhusu Simba kufunga magoli rahisi.

Mwalimu wa Simba, Abdallah Kibadeni alisifu kikosi chake kwa kuonekana kuimarika kila baada ya mechi licha ya nyota wake kadhaa, akiwemo Amisi Tambwe, kuonyesha kiwango duni jana.

Licha ya kuanza na mfungaji bora wa Kombe la Kagame

la klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Tambwe kutoka Vital'O ya Burundi, Simba ilipiga shuti moja tu katika dakika 45 za kwanza ambalo halikulenga lango hata hivyo.

Shuti hilo lilipigwa na Twaha Ibrahim mwanzoni kabisa mwa robo ya pili ya mchezo huo ambao Simba ilikuwa ikiwania kuzima wimbi la kufungwa mechi zote mbili msimu uliopita na kuchangia kushika nafasi ya tatu ya nje ya uwakilishi wa michuano ya Afrika.

Katika mechi nyingine za ligi kuu jana, JKT imeendelea kuongoza ligi na kuwa timu pekee yenye asilimia 100 ya pointi baada ya michezo mitatu, baada ya kuifunga Ashanti 1-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Coastal Union na Prisons zilitoka suluhu kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Ruvu Shooting ikaifunga Mgambo 1-0 kwenye Uwanja wa Mabatini, JKT Oljoro na Rhino zilitoka 1-1 mjini Arusha na Kagera Sugar na Azam zikapata matokeo kama hayo Uwanja wa Kaitaba.

Televisheni ya Azam ambayo haijaanza kuonekana hewani, lakini ambayo imenunua haki za kuonyesha michuano hiyo kwa miaka mitatu kwa mkataba wa sh. bilioni 5.6, jana ilikua ikichukua picha za mchezo huo kwa kutumia kamera tatu kubwa.

Timu zilikuwa:

SIMBA: Abel Dhaira, Nassoro Masoud, Issa Rashid, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas Mkude, Twaha Ibrahim (Betram Mwombeki dk.66), Said Hamisi (Henry Joseph dk.57), Amisi Tambwe, Amri Kiemba, Haruna Chanongo (Ramadhani Singano dk.88).

MTIBWA SUGAR: Hussein Sharif, Hassan Ramadhani, Paul George, Dickson Mbeikya, Salim Abdallah, Shaban Nditi, Ally Shomari, Masoud Mohammed, Juma Luzio (Mussa Hassan 'Mgosi' dk., Shaaban Kisiga (Abdallah Juma dk.78), Vincent Barnabas.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: