ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 17, 2013

Tanzania yakanusha vikali kuwanyanyasa Wamalawi

Msemaji wa Serikali,Assah Mwambene

Serikali imekanusha vikali taarifa kuwa wananchi wa Malawi wanaoishi nchini wanaishi kwa kujifungia ndani huku wakinyanyaswa, kudhalilishwa na kubakwa. Akizungumza kufuatia habari zilizoandikwa na gazeti la Malawi News toleo la juzi, Msemaji wa Serikali, Assah Mwambene, alisema habari hizo hazina ukweli wowote.

Mwambene ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), alisema kuwa juzi ulifanyika msako ulioendeshwa na ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam ambao uliwanasa Wanamalawi 1,030 ambao ni wahamiaji haramu.


Mwambene aliongeza kuwa baada ya kuwakamata, hakuna hata mmoja aliyewekwa ndani wala kufanyiwa kitu chochote kibaya, bali wote walipewa fomu ili kuhalalisha ukaaji wao nchini.

Mwambene alisema kuna raia 25,000 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia, Rwanda waliorudishwa kwao kufuatia agizo la Rais Kikwete na kwamba raia hao waliondoka wengine kwa hiari yao kwa hiyo zoezi hilo linaendelea kufanyika, hivyo hakuna jambo baya alililofanyiwa Mmalawi yeyote.

“Katika taarifa hizo, wamedai wamenyanyaswa, kudhalilishwa na mmoja imedaiwa amebakwa na inadaiwa habari hizo zimethibitishwa na Balozi wa Malawi nchini kuwa Wamalawi wote wanaishi kwa hofu na kwa kujificha baada ya kunyanyaswa, kudhalilishwa na mmoja wao kubakwa, jambo ambalo siyo kweli.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments: