UAMUZI wako wa kusoma safu hii ni kielelezo tosha kwamba, uwezo wako wa kufikiri ni wa kiwango cha juu. Hilo halitoshi, kusoma kwa makini, kuchuja na kufuata yaliyo mema yatathibitisha zaidi uelewa wako
Tunahitaji sana kujifunza kuhusu mapenzi maana siku hizi ulaghai umekuwa mwingi. Hapa kwenye All About Love ni mahali sahihi pa kupeana elimu hii.
Huwa inatokea mtu (zaidi kwa wasichana) yupo kwenye uhusiano na mpenzi wake. Kila anapoangalia mwelekeo hakuna. Ana tabia zote mbaya, wakati mwingine hata majibu yake yanaonesha wazi ama hamtaki tena, amemchoka au hampendi tu.
Pamoja na majibu hayo, bado anaendelea kung’ang’ania tu akisubiri muujiza. Wengine wamelemewa na mapenzi, hata kama amemfumania mpenzi wake zaidi ya mara nne, anaendelea kuwa na imani kuwa “atabadilika tu” au “lakini bado nampenda, siwezi kumuacha”.
Rafiki zangu, hebu fungueni vichwa vyenu sawasawa, halafu tuendelee na darasa letu.
JIFUNZE KUHUSU MOYO
Moyo hupenda. Kwa kawaida moyo haupendi ‘stress’ kwa hiyo kila wakati huhakikisha unatejitengenezea furaha ya kudumu. Kwa kawaida moyo ukishamwingiza mwenzi na kumficha ndani, haupendi na si desturi yake kuachia kirahisi.
Hujawahi kusikia mtu akisema: “Naachana naye lakini moyo wangu unauma. Bado nampenda sana ila kwa tabia zake namwacha.”
Ndivyo moyo ulivyo. Hata mtu awe vipi, haupo radhi kumwachia. Unaogopa sononeko na haupo tayari kupata jakamoyo. Mara kadhaa moyo hudanganya hasa kwenye sehemu inayotakiwa kufanya uamuzi mgumu.
Kazi kubwa ya moyo ni kutafuta, kutunza na kuzalisha furaha. Si huzuni. Si machozi. Si maumivu. Haupendi kuacha, kwa sababu una hakika na ndivyo ilivyo, kuwa maumivu, mateso, simanzi na vyote vibaya vitatokea pindi jambo hilo likifanyika.
AKILI...
Hufanya kazi kwa karibu sana na ubongo. Ndiyo fikra na kiongozi wa mwili baada ya ubongo kufanya kazi yake sawasawa. Ubongo ukifikiri, hupeleka majibu kwenye akili ambapo uamuzi hutolewa.
Uamuzi wake mara zote ni sahihi na huegemea zaidi kwenye faida za mwili mzima wa mhusika. Haina ubinafsi na haipendi kuonewa. Kwa kawaida hufuatilia na kulinda masilahi ya mhusika kwa kila eneo.
ANGALIA TOFAUTI
Akili inatambua kwamba, kama mtu akiingia kwenye matatizo ya mapenzi, anaweza kupata madhara mengi yakiwemo magonjwa. Kwanza ugonjwa wa akili. Lakini pia ugonjwa wa moyo.
Unaona eeh? Yaani (akili) inaogopa kuwa na kichaa ila kwa upande mwingine, inaogopa moyo kupata maradhi ya shambulio na shinikizo. Upo ushahidi wa kutosha kuwa kuna baadhi ya watu wameugua kichaa (wengine mpaka leo) kwa sababu ya mapenzi.
Achana na hao wa maradhi ya moyo, shinikizo la damu na mengineyo. Chanzo ni moyo. Angalia... moyo hauna muda wa kutafakari matatizo utakayokumbana nayo wenyewe, achana na akili na mwili kwa ujumla.
TOA NAFASI KWA AKILI
Sikia rafiki, moyo hueleza hisia za kweli. Hutunza upendo na kusambaza furaha mwilini. Ndiyo ukweli lakini linapokuja suala la masilahi ya MAISHA yako, toa nafasi kwa akili itafakari kwa kina.
Kuacha, kuachwa au kuachana kunaumiza sana lakini kwa masilahi ya mwili mzima na maisha yako unapaswa kufanya hivyo. Kumbuka moyo hauwezi kukuruhusu uachike lakini akili inaweza na inakuwa na sababu za msingi ambazo ni zao la furaha hapo baadaye.
USIISHI KWA KUBAHATISHA
Acha kufikiria kwamba, mwanaume/mwanamke uliyenaye umebahatisha tu. Ondoa fikra hizo kichwani mwako. Kwenye penzi la kweli hakuna kubahatisha.
Yapo matatizo ambayo ni makubwa na hayavumiliki kwa kweli. Kwa mfano, jiulize, kama mpo kwenye urafiki tu, mwanaume anakupiga kama mnyama. Umeshamfumania zaidi ya mara nne, umekuta meseji za hovyo kwenye simu yake, ukimwuliza vibao!
Kuna mapenzi kweli hapo? Ni marafiki tu, vipi akikuoa? Achia akili ifanye uamuzi sahihi, moyo utakuongopea. Niamini rafiki yangu.
NDOA IPO, HAILAZIMISHWI
Kama ipo ipo tu. Hata kama ndoa ni yako, itakuwa na faida gani kwa mwenzi ambaye atakuwa anakesha baa? Mwenzi ambaye atakuwa anakudunda kila siku? Ana wapenzi wengine nje ya ndoa? Itakusaidia nini?
Sikia, kumbuka kwamba, kuendelea kumng’ang’ania maana yake unaacha umri wako uzidi kusogea na mwisho wake, hakuna atakayekubali kuoa ‘kikongwe’. Kazi kwako rafiki yangu.
MAISHA NI NINI HASA?
Maisha yana changamoto nyingi lakini kikubwa kila mtu anapenda kufurahi. Maisha ni furaha, amani na upendo. Kwa mwenzi mwenye tabia za hovyo, ‘stress’ kila siku, ngumi, usaliti na kufumaniana kutakupa furaha katika maisha yako? Utaipata wapi? Amua sasa.
Mada imeisha. Natafakari kuhusu mada ya wiki ijayo lakini nitafurahi kama nawe utapendekeza cha kuandikwa hapa wiki ijayo. Mawasiliano yako wazi. Nawapenda sana!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers.
No comments:
Post a Comment