ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 23, 2013

Unyama Kenya : Waliouawa na magaidi wafikia 69

Bado jengo hilo limezingirwa na wanajeshi, kuhakikisha magaidi hao hawatoki nje kuhatarisha usalama wa wananchi.
Baadhi ya raia, waliokuwa ndani ya jengo hilo wakitoka nje kwa hofu kubwa jana, Picha na AFP
Nairobi. Magaidi wanaokadiriwa kuwa kati ya 10 na 15 wamelitikisa Jiji la Nairobi kwa siku mbili mfululizo baada ya kuteka jengo kubwa la biashara la Westgate lililopo Westlands na kuua watu wapatao 69 hadi leo asubuhi.
Magaidi hao walivamia jengo hilo juzi saa tano asubuhi na hadi jana, jitihada za kuwadhibiti zilikuwa hazijafanikiwa. Zaidi ya watu 1,000 wameokolewa na wengine zaidi ya 170 wamejeruhiwa.
Tukio hilo limesababisha shughuli mbalimbali katika Jiji la Nairobi kusimama na hata maduka mengine makubwa ya Nakumatt kufungwa, hivyo kusababisha upatikanaji wa bidhaa mbalimbali kuwa shida kwa wakazi wengi wa Nairobi.
Wakazi wengi wa eneo la Westlands jana walikwama kufika katika maeneo yao na watu wengi waliokuwa kwenye jengo hilo waliacha magari yao na kukimbia huku na huko ili kujiokoa huku vyombo vya usalama vikiwataka wananchi kukaa mbali na eneo hilo.
Magaidi hao wanaodaiwa kuvalia vitambaa vyeusi vinavyofunika nyuso zao, wameteka eneo hilo kwa siku mbili, huku wakiwa wamezima taa zote za ili kujilinda na askari wa Kenya ambao waliingia kupambana nao.
Risasi zimekuwa zikisikika usiku kucha na watu zaidi wameendelea kuuawa huku Serikali ikisema mateka wanaodaiwa kuwepo ndani ya jengo hilo wakiwa chini ya magaidi hao ni 30.
Jengo hilo limezingirwa na vyombo vya usalama vya ndani na nje ya Kenya vikiongozwa Mkuu wa Majeshi ya Kenya pamoja Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), David Kimaiyo, ambaye amekuwa akitoa taarifa mbalimbali za tukio hilo kupitia account yake ya Tweeter ili kuhakikisha vyombo vya habari na jamii vinajua kinachoendelea.
Pia Wizara ya Mambo ya Ndani imekuwa ikitoa taarifa kupitia mitandao yake, huku televisheni zote za Kenya zikirusha tukio hilo moja kwa moja tangu lilipotokea juzi.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph Ole Lenku akizungumza na vyombo vya habari alisema watu 69 waliouawa ni pamoja na raia wa kigeni kutoka nchi mbalimbali. Hata hivyo, alisema haijajulikana ni wangapi na wanatoka nchi gani haswa.
Canada imethibitisha kuwa raia wake wawili wameuawa kwenye tuko hilo, pia raia wawili wa Ufaransa nao wameuawa.
Kundi la kigaidi la Al-Shabaab limedai kuhusika na tukio hilo ambalo ni kubwa kutokea Kenya tangu ubalozi wa Marekani ulipolipuliwa mwaka 1998 jijini Nairobi
Jengo lote limezingirwa na wanajeshi pamoja na askari polisi huku wengine wakiwa ndani kuhakikisha kuwa wanaokoa mateka wengine na kupambana na magaidi hao, huku helikopta za jeshi zikizunguka angani usiku kucha kuhakikisha usalama wa watu katika jiji hilo.
Tayari askari hao wamefanikiwa kushikilia ghorofa ya kwanza na pili ya jengo hilo, huku ikielezwa kuwa magaidi hao wamejificha katika duka kubwa la Nakumatt lililopo katika jengo hilo.
Askari wawili wa jeshi walijeruhiwa na kupelekwa hospitalini, huku wengine wakiwa ndani kupambana na magaidi hao.
Cameron, Ki Moon watuma salamu
Viongozi mbalimbali wa kimataifa wametuma salamu za rambirambi na kutoa pole kwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kutokana na tukio la kigaidi lililotokea nchini humo.
Pia viongozi hao wamelaani tukio hilo ambalo ni kubwa kutokea Kenya tangu ubalozi wa Marekani ulipuliwe mwaka 1998.
Waziri  Mkuu wa Uingereza, David Cameron, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa(UN), Ban Ki Moon pamoja na Serikali ya Rwanda wamelaani tukio hilo na kuwataka Wakenya kuwa pamoja.
Pia Naibu Rais wa Kenya, William Ruto ambaye yuko The Hague, Uholanzi akihudhuria kesi inayomkabili, ametuma salamu za rambirambi na kutaka nchi kuwa na utulivu wakati vyombo vya usalama vikifanya kazi yake.
Mwananchi

No comments: