Mwenyekiti wa Umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Sadifa Juma akizungumza katika mkutano wa umoja huo mjini Zanzibar.Wengine ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Ali Seif Iddi na Katibu Mkuu wa CCM, Adulrahman Kinana. Picha ya CCM
Dar na Zanzibar. Mvutano mkubwa umeibuka ndani ya Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi (UVCCM), kutokana na baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu la umoja huo kudhamiria kumng’oa madarakani mwenyekiti wao, Sadifa Juma Khamis.
Mgogoro huo ulisababisha kikao cha Baraza Kuu kilichokuwa kikifanyika Zanzibar juzi, ambacho mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Balozi Seif Ali Iddi kutofikia mwisho kutokana na baadhi ya wajumbe kumtaka Sadifa na Kamati yake ya Utekelezaji kutoka nje ili wajadiliwe kwa kukiuka kanuni.
Sadifa anadaiwa kukiuka Ibara ya 91 ya toleo la nane la Kanuni za UVCCM kwa kutangaza uteuzi wa wakuu wa idara tatu za umoja huo, kabla ya kuundwa kwa Kamati ya Utekelezaji ambayo kimsingi alipaswa kushirikiana nayo kuwateua, kabla ya kuidhinishwa na baraza kuu.
Habari kutoka katika mkutano huo uliofanyika katika Ofisi ya CCM, Kisiwandui zinasema Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ndiye aliyeokoa jahazi baada ya kuingilia kati mvutano baina ya baadhi ya wajumbe na Sadifa.
Inaelezwa pia kuwa Katibu Mkuu mpya wa UVCCM, Sixtus Mapunda naye alionja chungu ya mgogoro huo pale alipopingwa vikali na wajumbe, alipojaribu kumtetea mwenyekiti wake.
Hata hivyo, Sadifa na Mapunda kwa nyakati tofauti jana walisema kuwa mkutano huo ulimalizika bila tatizo na ulikuwa na ajenda moja tu ya kumthibitisha Katibu Mkuu jambo ambalo lilifanyika kama ilivyokuwa imepangwa.
“Kwa mujibu wa kanuni, mwenyekiti ndiye mwenye mamlaka ya kufungua na kufunga kikao na vyote hivyo tulifanya, hakuna kikao kilichovunjika,” alisema Sadifa.
Alipotakiwa kueleza kuhusu kanuni anayodaiwa kuivunja, alikataa kuzungumzia suala hilo akitaka kwanza mwandishi amwambie chanzo chake cha habari.
“Nani huyo aliyetaka nitoke, wewe nisikilize, kuna watu ambao wanajua kabisa unataka kuzungumza nini hata kabla hujasema na mmoja wa watu hao ni Sadifa kwa hiyo nilishajua kabisa ni nini unataka,” alisema Sadifa na baada mwandishi kuendelea kumuuliza maswali alikata simu.
Kwa upande wake, Mapunda alisema: “Mkutano ulifanyika na kumalizika kama ulivyokuwa umepangwa. Ule ulikuwa ni mkutano maalumu na ulikuwa na ajenda moja tu, mwenyekiti aliufungua na kuufunga kama ilivyokuwa imepangwa. Ajenda ilikuwa ni kunithibitisha mimi tu (kuwa katibu wa UVCCM) na baada ya hilo kufanyika nilikaribishwa na mimi nikazungumza na nikamaliza”.
Ilikuwaje?
Habari zinasema wajumbe hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa UVCCM, Mkoa wa Ruvuma, Alex Nchimbi walikuwa wakilalamika kwamba Sadifa alikiuka kanuni katika kuteua wakuu hao wa idara hivyo uwepo wao katika kikao cha baraza hilo haukuwa halali.
Katika hoja hiyo iliyoungwa mkono na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mbeya, Amani Kajuna, Nchimbi alimtaka Sadifa na wajumbe wote wa Kamati ya Utekelezaji watoke nje, ili Baraza Kuu liwajadili.
“Sadifa alikataa na badala yake alimwambia Nchimbi akae chini la sivyo angemtoa nje ya mkutano hali ambayo ilizua mvutano mkali kwa sababu wajumbe wengine walisimama kumpinga Sadifa na wachache walikuwa wakimtetea,” alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho. Kutokana na hali hiyo, Kinana aliingilia kati na kuwaomba viongozi wa UVCCM waende faragha kwa muda ili wakajadiliane na waliporejea aliwatangazia wajumbe kwamba wamekubaliana kuwa kikao hicho kiahirishwe ili kiitishwe kingine mwezi ujao kwa ajili ya kuzungumzia pamoja na mambo mengine, uteuzi huo.
Habari hizo zilimnukuu Kinana akikiri kufanyika kwa makosa katika uteuzi wa wakuu wa idara aliowatangaza katika kikao cha Baraza Kuu cha Februari Mjini Dodoma.
“Kitaitishwa kikao kingine Dodoma mwezi wa 10 (Oktoba) ili tuweze kukamilisha taratibu hizo, lakini wewe subiri utaona tutakamilisha uteuzi halafu yeye naye (Sadifa) atang’oka maana hatuwezi kukaa na mwenyekiti ambaye hajui kanuni,” alisema mjumbe mwingine.
Kwa uamuzi huo, sasa ni dhahiri kwamba Baraza Kuu la UVCCM, limetengua uteuzi wa watendaji hao wa Idara za Oganaizesheni, Fedha na Uchumi na ile ya Chipukizi na Uhamasishaji.
Habari zaidi zinasema kulikuwa na ulinzi mkali wa polisi katika kikao hicho na kila mjumbe alifanyiwa ukaguzi wa hali ya juu ikidaiwa kwamba ilikuwa ni kuwabaini wajumbe ambao walikuwa wamepanga kuingia na silaha.
Fedha na simu
Kada wa CCM ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM lililopita, (jina linahifadhiwa), anadaiwa kugawa kwa kificho fedha kiasi cha Sh100,000 kwa kila mjumbe wa wa mkutano huo lengo likiwa ni kumwokoa Sadifa.
Inadaiwa kwamba mbali na fedha hizo, pia wajumbe walikodiwa usafiri wa boti kutoka Zanzibar hadi Dar es Salaam na baadhi yao kulipiwa gharama za vyumba vya kulala na chakula.
Kadhalika, wajumbe wote wa kikao hicho walizawadiwa simu aina ya Samsung Galax na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ili ‘kurahisiaha mawasiliano’ miongoni mwao, kitendo ambacho pia kinapewa tafsiri kwamba huenda kuna ajenda nyuma ya simu hizo.
Makamba alikiri kugawa simu hizo lakini akasema ilikuwa sehemu ya kutekeleza ahadi aliyoitoa kwenye mkutano wa Baraza Kuu la UVCCM uliofanyika Dodoma Februari 16, mwaka huu ambao wajumbe hao waliomba kupewa simu hizo.
Alisema katika mkutano huo, alialikwa kutoa mada na alizungumzia suala la matumizi ya mitandao ya kijamii katika kukijenga chama na baadhi ya wajumbe walisema wanashindwa kutumia njia hiyo kwa kuwa wapo mbali na maeneo ya mijini.
Alisema kabla ya kutoa simu hizo, umoja huo ulimkumbusha kuhusu ahadi yake kutokana na barua yenye kumbukumbu namba VMM/M.30/39/Vol.17/35 ambayo pia ilimwalika kuhudhuria kwenye mkutano wa juzi.
Makamba alisema ili kutimiza ahadi hiyo, alizungumza na baadhi ya makada wenzake na kuwaomba wamsaidie.
“Nilifanya kaharambee kadogo, mtu ukiombwa na wewe unahangaika huku na huko, walinipa na jana (juzi) tuligawa simu 138,” alisema.
Mgogoro UVCCM
Sadifa ambaye pia ni Mbunge wa Donge, aliwahi kulalamika kuhusu kuwapo kwa kundi la vijana wapatao 10 kutoka mikoa mbalimbali ambao wamekuwa wakimpiga vita na kuingilia utendaji wa kazi zake kinyume cha katiba ya jumuiya hiyo.
Hata hivyo, Sadifa amekuwa akilaumiwa na baadhi ya wanachama wa UVCCM kwamba ameshindwa kazi na badala yake amekuwa akitoa lugha chafu mbele ya vikao dhidi ya wajumbe ambao wamekuwa wakihoji mambo yanavyokwenda.
Baada ya kuchaguliwa, Sadifa na Makamu wake, Mboni Mhita walipingwa kwa mabango mbele ya Makamu Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kutokana na madai kwamba uchaguzi uliowaweka madarakani uligubikwa na rushwa.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment