Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Helen Kijo-Bisimba
Uamuzi wa ghafla wa serikali wa kuyafungia magazeti mawili, MWANANCHI na Mtanzania uliotangazwa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Asaah Mwambene, umepokelewa kwa mshituko mkubwa na wadau mbalimbali huku wengi wakihoji mwelekeo wa demokrasia nchini.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE jana kwa kuzungumza na watu wa kada mbalimbali, wakiwamo wanasheria, wanataaluma, wanahabari, wanaharakati, wanasiasa na watetezi wa haki za binadamu, wote walikuwa na kauli moja ya kufanana kwamba uamuzi huo ni mbaya na unatekelezwa chini ya sheria mbaya ambayo kwa zaidi ya miaka 20 imekuwa ikipigiwa kelele ifutwe.
Serikali ilitangaza kulifungia MWANANCHI kwa siku 14 na Mtanzania siku 90 kuazia Septemba 27, mwaka huu kwa madai kuwa magazeti hayo yaliandika habari na makala za uchochezi na uhasama kwa nia ya kusababisha wananchi wakose imani kwa vyombo vuya dola.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, katika taarifa yake aliyoitoa jana na gazeti hili kupata nakala yake, alisema sababu zilizotolewa na serikali kuyafungia magazeti hayo siyo za msingi.
Alisema kwa mfano moja ya sababu ya kufungiwa kwa gazeti la MWANANCHI ni kuchapisha taarifa kuhusu mishahara ya Serikali, ambayo kwa mujibu wa Serikali ni siri.
Kabwe alisema kwa Serikali kama ya Tanzania ambayo imesaini makubaliano ya kuendesha serikali kwa uwazi (Open Government Initiative) na kumwagiwa sifa na Rais Barack Obama wa Marekani, haikupaswa kulifungia gazeti kwa kuandika habari za mishahara ya watumishi wa Serikali.
“Mishahara kuanzia wa Rais mpaka wa mtendaji wa Kijiji haipaswi kuwa jambo la siri, na kwa kuonyesha kuwa jambo hili linapaswa kuwa wazi, katika mkutano ujao wa Bunge, tutatafuta kila namna kutaja mshahara wa Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu,” alisema.
Alisema watafanya hivyo kama njia ya kuwaunga mkono gazeti la MWANANCHI kwa habari yao hiyo, kwa kuwa Watanzania wana haki ya kujua wanawalipa kiasi gani watumishi wao.
“Mapato ya mbunge yanajulikana kuwa ni Sh. milioni 11.2 kwa mwezi, kabla ya kuongeza posho za vikao za Sh. 200,000 kwa siku na posho ya kujikimu ya Sh. 130,000 kwa siku, hivyo na mishahara ya watumishi wengine wa umma ni lazima sasa ijulikane,” alisema.
Kabwe alisema badala ya serikali kuyafungia magazeti hayo, ingeweza kufungua mashtaka ya kawaida mahakamani iwapo haikupendezwa na habari zilizochapishwa na magazeti hayo.
“Ni wakati sasa kwa wananchi kuifanya serikali kujutia uamuzi wake wa kuyafungia magazeti haya.
Nimeamua binafsi kama Mbunge, kesho Jumatatu (leo) kupeleka taarifa rasmi kwa Katibu wa Bunge ya kupeleka Muswada Bungeni, wa kuifuta kabisa Sheria hii kandamizi ya Magazeti ya mwaka 1976,” alisema.
Alisema ameamua kufanya hivyo kwa lengo la kupambana na kundi dogo la wahafidhina ndani ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wasiopenda mabadiliko, ili iwe fundisho kwao, na wengine waliopo ndani ya serikali, kwamba uhuru wa habari sio jambo la kuchezea kama golori.
Alisema magazeti haya yamefungiwa kutokana na shinikizo la wahafidhina walioko ndani ya serikali.
DK. BANA: INASHANGAZA
Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema haikutarajiwa katika kipindi hiki serikali kuyafungia magazeti kongwe na yenye wasomaji wengi, kama hayo ya Mwananchi na Mtanzania.
“Ni muhimu serikali ikajielekeza kuangalia inataka kupata nini, kwa sababu haitoshi kuchukua hatua dhidi ya magazeti kwa kuangalia vichwa vya habari. Ni wakati mwafaka sasa wa kuelekeza nguvu zetu kuwa na sheria mpya ya habari,itakayokidhi matakwa ya wakati,” alisema.
Dk. Bana alisema kufungia gazeti kwa sababu ya kuchapisha mishahara ya watumishi wa umma siyo kitu sahihi, kwa sababu mishahara hiyo inalipwa na kodi za wananchi, kwa hiyo wana haki ya kujua kile wanachopata watumishi hao wa umma.
Alisema mwananchi anayo haki ya kujua kwa mfano mwalimu analipwa Shilingi ngapi, kama ni 200,000 au 300,000 ili waweze kupaza sauti yake kuwa, anacholipwa ni kidogo na hakihamasishi kufundisha.
Alisema mishahara ya watumishi wa umma ni tofauti na ya sekta binafsi ambayo inaweza ikafanywa siri kwa sababu mbalimbali zikiwamo za kiushindani.
Hata hivyo, aliviasa vyombo vya habari kufuata sheria katika utendaji wao wa kazi na kufuata maonyo yanayotolewa na serikali.
LHRC: NI KUWANYIMA HAKI WANANCHI
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Helen Kijo-Bisimba, alisema hatua ya serikali kuyafungia magazeti hayo ni kuwanyika haki Watanzania kupata habari.
Alisema serikali ingepaswa kumwadhibu mwandishi au mhariri aliyeandika habari hiyo ya uchochezi na siyo kuliadhibu gazeti lote kwa kulifungia.
“Sina uhakika kama uongozi wa magazeti yaliyofungiwa waliitwa na kupewa nafasi ya kujitetea, sheria ya mwaka 1976 bado ni kandamizi,” alisema Bisimba na kusisitiza kuwa menekimenti za magazeti hayo zingeitwa kupewa nafasi ya kujitetea.
TLS: SHERIA NI KANDAMIZI
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Stolla, alisema Sheria ya magazeti ya mwaka 1976 iliyotumika kuyafungia magazeti hayo ni mojawapo ya sheria 40 zilizopendekezwa na Tume ya Nyalali kufutwa kwa kuwa zimepitwa na wakati.
Alisema sheria hiyo inaweza kutumika pasipo kuwapo na mipaka yoyote, pia haijaeleza wala kufafanua habari zipi ni za uchochezi na habari ipi ikiandikwa kwa mfumo fulani itakuwa imechochea uvunjifu wa amani nchini.
Alisema ni kifungu kibaya kinachokiuka katiba ya nchi, na kueleza kuwa serikali ingepaswa kutumia taratibu zingine kuliko hatua iliyochukua.
JUKWAA LA WAHARIRI
Katibu Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena, alisema wanatarajia kukutana hivi karibuni kujadili suala hilo na kulitolea tamko.
KAULI YA NEW HABARI
Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006) ambayo ni machapishaji wa Mtanzania, Absalom Kibanda, alisema wamepokea kwa mshtuko na mshangao mkubwa juu ya kufungiwa kwa gazeti lao kwa kuwa hawakupewa taarifa kabla.
Kibanda alisema hadi jana serikali haikuwapatia barua yoyote ya kufungiwa kwa gazeti lao na kueleza kuwa tangu Jumamosi zilipotoka taarifa za kufungiwa, wamekuwa wakizisikia kwenye vyombo vya habari.
KAULI YA MWANANCHI
Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Ltd ambayo ni mchapishaji wa MWANANCHI, Tido Mhando, alisema wamepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kufungiwa kwa gazeti lao.
Alisema walipokea barua kutoka serikalini Julai 29 wakitakiwa kujieleza baada ya kuchapisha habari iliyohusu mishahara mipya kwa watumishi wa serikali Julai 12, mwaka huu.
Alisema walipopata barua hiyo waliijibu, lakini wanashangazwa na hatua iliyochukuliwa ya kulifungia gazeti hilo.
“Tutatumia hatua mbalimbali kusahihisha hali hii kwani kufungiwa kwetu kumeleta athari kubwa kwa Watanzania kwa kuwa asilimia 50 ya wasomaji magazeti nchini wanaelewa Kiswahili,” alisema Tido.
Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut), Profesa Mwesiga Baregu, alisema sheria ya magazeti ya mwaka 1976 inapaswa kurekebishwa, na uamuzi ulichukuliwa na serikali haukufuata sheria na haki.
Alisema Tanzania kuna vyombo vya sheria na haki likiwamo Baraza la Habari Tanzania (MCT) ambalo linatambulika na liliundwa kwa dhumuni la kutatua matatizo kama hayo yaliyotokea.
Alisema serikali ilipaswa kuwasilisha malalamiko hayo kwa MCT au kupelea mahakamani kuliko kuchukua uamuzi wa haraka wa kuyafungia magazeti hayo.
“Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo alipaswa aangalie kwa mtazamo mwingine, hapa nchini kuna mahakama, MCT ambavyo vingeweza kutatua tatizo hilo, “ alisema Profesa Baregu.
Alifafanua kuwa uamuzi uliochukuliwa na serikali ni wa kibabe, unaopelekea wananchi kunyimwa haki ya kupata habari kutokana na magazeti hayo kuwa ni miongoni mwa vyombo vya habari vikubwa nchini.
MNYIKA AJA JUU
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, amevitaka vyombo vya habari nchini vichukue hasira ya kufungiwa kwa magazeti hayo kama changamoto ya kuibua maovu yanayotokea.
Pia alisema uamuzi huo uliochukuliwa na Serikali usihamishe mjadala wa kutetea Katiba Mpya na kwamba sheria ya magazeti ya mwaka 1976 ni mbovu na imekuwa ikipigiwa kelele mara kwa mara na wadau mbalimbali wa habari ambao wamepeleka muswada wa Sheria ya Habari, lakini hadi leo Serikali haitaki kuupeleka bungeni.
Mnyika ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema kama Serikali ilipaswa kupeleka malalamiko kwa MCT na siyo kugeuka wao wenyewe ndo walalamikaji, waendesha mashtaka na wao ndiyo majaji.
Alisema Serikali inatumia sheria mbaya, madaraka vibaya, na kufanya uamuzi mbaya wa kuyafungia magazeti.
Aliongeza kuwa wananchi na wadau wa habari nchini wasiishie kulaani tu kwani tangu gazeti la Mwanahalisi limefungiwa ni mwaka sasa na bado serikali iko kimya.
Mnyika alisema atachukua hatua ya kupeleka bungeni muswada wa sheria kwa hati ya dharura ili Serikali irekebishe Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976.
Ikitumia Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976, serikali kupitia kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Assah Mwambene, iliyafungia magazeti hayo kwa madai ya kuchapisha habari zenye mwelekeo wa uchochezi na uvunjifu wa amani.
Imeandikwa na Gwamaka Alipipi, Raphael Kibiriti na Jacqueline Yeuda ; Dar
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment