ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 31, 2013

AFIA MAHAKAMANI AKISUBIRI KUMWEKEA DHAMANA MWANAYE TUKUYU

Tiger Mwaigomole (70) Mkazi wa kata ya Masukulu wilayani Rungwe amefariki dunia ghafla akiwa katika chumba cha Mahakama ya Wilaya ya Rungwe akifuatilia mwenendo wa kesi inayomkabili mtoto wake wakati Mahakama ikiendelea.

MTU mmoja aliyefahamika kwa jina la Tiger Mwaigomole (70) Mkazi wa kata ya Masukulu wilayani Rungwe amefariki dunia ghafla akiwa katika chumba cha Mahakama ya Wilaya ya Rungwe akifuatilia mwenendo wa kesi inayomkabili mtoto wake wakati Mahakama ikiendelea.

Tukio hilo la aina yake lilitokea hivi karibuni majira ya saa 9 alasiri ndani ya Mahakama hiyo ambapo Marehemu alifika mahakamani hapo akiwa na mwanaye aliyejulikana kwa jina la Lusajo Tiger (40) wakiwa na lengo la kumwekea dhamana ndugu yao Gwakisa Tiger ambaye alifikishwa mahakamani hapo akituhumiwa kwa kosa la kupigana na kujeruhi katika ugomvi uliotokea kijijini kwao.

Kwa mujibu wa mtoto wa Marehemu aliyekuwa ameongozana nae Mahakamani hapo Lusajo Tiger alisema wakati kesi ikiendelea chini ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Rungwe, Kingwele, ndugu yao alipandishwa kizimbani kusomewa mashtaka yanayomkabili ndipo marehemu alipoanza kutetemeka kwa madai kuwa anajisikia baridi kali sana.

Alisema kutokana na marehemu kulalamikia baridi aliamua kumnunulia chai ya moto ili anywe na kupunguza baridi ambapo baada ya kufanya hivyo marehemu alikata roho muda mfupi baada ya kumaliza kunywa chai aliyokuwa amepelekewa huku akiwa amekaa ndani ya chumba cha mahakama hiyo.

Kutokana na tukio hilo Askari polisi waliokuwepo mahakamani hapo waliuchukua mwili wa marehemu na kuukimbiza katika Hospitali ya Wilaya ya Rungwe Makandana kwa ajili ya vipimo lakini hata hivyo mwili ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi ingawa ripoti ya kifo chake haikutolewa mapema.

Wakati huo huo Hukumu ya kesi ya mauaji dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Rungwe, John Mwankenja inayowakabili Hakimu Mwakalinga na wenzie watatu huenda ikatolewa Novemba 11 mwaka huu baada ya Mahakama kuu kanda ya Mbeya chini ya Jaji Samwel Karua kumaliza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka pamoja na utetezi kwa upande wa watuhumiwa.

Kwa mujibu wa Jaji Karua alisema baada ya kumaliza kusikiliza pande zote mbili atatumia muda wa siku mbili kwa ajili ya kuandika hukumu ambayo itaitoa Novemba 11, Mwaka huu, kesi ambayo inasimamiwa na Mwanasheria wa Serikali Archiles Mulisa huku watuhumiwa wakitetewa na Mawakili wawili wa kujitegemea ambao ni Simon Mwakolo na Victor Mkumbe.

Na Mbeya yetu

No comments: