Wachezaji wa Azam wakishangilia ushindi wao leo
AZAM FC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba SC ikitoka nyuma kwa bao 1-0.
Shujaa wa Azam leo alikuwa ni mshambuliaji kutoka Ivory Coast na mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Kipre Herman Tchetche aliyefunga mabao yote ya timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa.
Kwa matokeo hayo, Azam inatimiza pointi 23 na kujinafasi kileleni, ikiwazidi kwa pointi tatu Simba SC na Mbeya City katika nafasi ya pili.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Oden Mbaga aliyesaidiwa na Hamisi Chang’walu na John Kanyenye wote Dar es Salaam, hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1.
Simba SC ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 21 kupitia kwa Ramadhani Singano ‘Messi’ aliyemalizia mpira ulioingizwa kutoka pembeni na Zahor Pazi.
Bao hilo liliwaongeza kasi Simba SC na kushambulia zaidi langoni mwa Azam FC, lakini hawakufanikiwa kupata bao la pili.
Azam ilifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 44 kupitia kwa Kipre Tchetche aliyemalizia mpira wa Erasto Nyoni kutoka pembeni kulia.
Kipindi cha pili, timu zote zilishambuliana kwa zamu kabla ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kumpa pasi nzuri Kipre Tchetche upande wa kushoto, akamfunga tela William Lucian ‘Gallas’ kisha kumchambua Abbel Dhaira kwa ustadi wa hali ya juu.
Katika kipindi hicho, Simba SC ilipoteza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 60 kupitia kwa Sino Augustino aliyebaki yeye na kipa na kupaisha juu ya lango kufuatia pasi nzuri ya Ramadhani Singano ‘Messi’.
Kikosi cha Azam FC leo kilikuwa; Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Aggrey Morris, Said Mourad/David Mwantika dk47, Kipre Balou, Kipre Tchetche, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco, Humphrey Mieno/Khamis Mcha dk 73 na Joseph Kimwaga/Farid Mussa dk47.
Simba SC; Abbel Dhaira, William Lucian ‘Gallas’, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Joseph Owino, Hassan Hatibu, Jonas Mkude, Ramadhani Singano ‘Messi’, Said Ndemla, Betram Mombeki, Zahor Pazi/Sino Augustino dk55 na Amri Kiemba/Edward Christopher dk55.
Ligi hiyo itakamilisha raundi ya 11 kesho kwa mechi tatu huku Yanga ikiwa mwenyeji wa Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mbeya City na Tanzania Prisons. Rhino Rangers na JKT Ruvu zitacheza katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Raundi ya 12 ya ligi hiyo itaanza Oktoba 31 mwaka huu kwa mechi kati ya Simba na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Novemba Mosi mwaka huu kutakuwa na mechi kati ya Yanga na JKT Ruvu kwenye uwanja huo huo.
Novemba 2 mwaka huu kutakuwa na mechi nne; Mgambo Shooting na Coastal Union (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Tanzania Prisons na Oljoro JKT (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Azam na Ruvu Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), na Mtibwa Sugar na Rhino Rangers (Uwanja wa Manungu, Morogoro).
Raundi hiyo itakamilika Novemba 3 mwaka huu kwa mechi moja ambapo Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Ashanti United kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Mechi za kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo zitachezwa Novemba 6 na 7 mwaka huu. Novemba 6 ni JKT Ruvu vs Coastal Union, Ashani United vs Simba, Kagera Sugar vs Mgambo Shooting, Rhino Rangers vs Tanzania Prisons na Ruvu Shooting vs Mtibwa Sugar.
Novemba 7 mwaka huu, Azam itacheza na Mbeya City wakati Yanga itacheza na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment