MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imempa nafasi nyingine Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kukata rufaa kupinga kuachiwa huru kwa aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam (RCO), Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe na wenzake wanane.
Katika shauri hilo, mahakama inamtaka DPP kuwasilisha nia ya kukata rufaa nje ya muda ndani ya siku 14 na imefanya hivyo kwa maslahi ya umma baada ya rufaa ya awali kutupwa na Mahakama ya Rufaa kutokana na kasoro za kisheria.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Aloysius Mujuluzi, baada ya kupitia hoja za pande mbili zinazopingana.
“Uamuzi wa mahakama hii uliowaachia huru washtakiwa ulifuata msimamo wa kisheria wa kutambua muhusika mkuu wa kosa la jinai pale watu wanapokuwa wengi katika kesi moja, kwa maslahi ya umma ingehitaji mahakama ya juu kupitia vipengele vilivyotumika kuwaachia huru washtakiwa.
“Maslahi ya umma ni kuweka bayana tafsiri sahihi ya vipengele hivyo vya sheria, tunaipa nafasi Jamhuri kwa niaba ya umma kuwasilisha kusudio la kukata rufaa ili ionekane haki ikitendeka.
“Mahakama imeyakubali maombi ya DPP ya kuongezewa muda wa kuwasilisha kusudio la kukata rufaa na inatoa siku 14 kuanzia leo, kusudio hilo liwe limewasilishwa,” alisema Jaji Mujuluzi.
Akizungumzia upungufu wa ofisi ya DPP, alisema kuna udhaifu katika hati nyingi zinazotoka katika ofisi hiyo hali inayotia wasiwasi.
“Ni kweli kuna udhaifu katika hati nyingi zinazotoka kwa DPP, zinatia wasiwasi, suala hili linatakiwa kufanyiwa kazi liondoshwe kwa maslahi ya umma.
“Hata katika maombi haya ukitupia jicho huwezi kukosa makosa, afisa aliyeapa hakusema yeye ana cheo gani kwa DPP, hizi ndizo hati zinazotoka huko,” alisema.
Awali DPP alikata rufaa akipinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomwachia huru Zombe na wenzake katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro na dereva teksi mmoja wa Manzese jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, Mei 8, 2013, Mahakama ya Rufani ilitupilia mbali rufaa hiyo kutokana na kasoro za kisheria zilizobainika katika hati ya kusudio la kukata rufaa.
Kasoro hiyo iliyobainika kwenye taarifa ya kusudio la kukata rufaa, ni kuandika kuwa hukumu inayopingwa ilitolewa na Jaji Salumu Massati wa Mahakama ya Rufani, badala ya Jaji wa Mahakama Kuu.
DPP alilazimika kuwasilisha maombi Mahakama Kuu akiomba kibali cha kukata rufaa hiyo nje ya muda, maombi ambayo yamekubaliwa.
Mbali na Zombe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Christopher Bageni, Ahmed Makele, WP 4593 PC Jane Andrew, D 1406 Koplo Emmanuel Mabula, D 8289 DC Michael Shonza, D. 2300 Abeneth Saro, D.4656D/Koplo Rajabu Bakari na D.1317D/XP Festus Gwasabi na jana washtakiwa wote walifika mahakamani hapo.
Washtakiwa hao walidaiwa kuwa Januari 14, mwaka 2006 waliwaua wafanyabiashara watatu wa madini wa wilayani Ulanga, mkoani Morogoro; Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe pamoja na dereva teksi, Juma Ndugu, mkazi wa Dar es Salaam kwa madai kuwa walikuwa majambazi.
Waliachiwa huru Agosti 17, 2009, baada ya mahakama kuona Jamhuri haikuweza kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka.
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment