ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 18, 2013

SAKATA LA UFOO SARO LACHUKUA SURA MPYA UPANDE WA WAKWE ... RIPOTI KAMILI HII HAPA

UTATA wa risasi umegubika tukio la kifo cha mzazi mwenzake na mwandishi wa habari wa ITV, Ufoo Saro, marehemu Anthery Mushi, aliyejiua kwa kujipiga risasi. Utata huo umeibuka baada ya ndugu wa marehemu Mushi kushangazwa na kuhoji mazingira ya kifo cha ndugu yao anayedaiwa kujipiga risasi mbili kidevuni na kupoteza maisha papo hapo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, jana Msemaji wa familia hiyo ambaye pia ni kaka wa marehemu, Isaya Mushi alisema familia imebaki kizani juu ya kifo cha ndugu yao na kwamba anayejua siri nzito juu ya kifo hicho ni mzazi mwenzake, Ufoo.
Isaya, alisema mazingira ya kifo cha Mushi ni ya kutatanisha kwani baada ya mwili wake kufanyiwa uchunguzi na madaktari, zilitolewa risasi mbili kichwani, huku wakihoji risasi ya pili.

Kwa mujibu wa wataalamu waliobobea katika silaha, ni vigumu mtu kujiua kwa risasi mbili katika eneo la kichwa kwa maelezo kuwa risasi moja inatosha kumaliza uhai wa mtu katika eneo hilo.

“Sisi kama familia bado tukio hili linatupa utata, hivyo tunaomba Jeshi la Polisi litumie busara katika kufanya uchunguzi wa kina kwani, Mushi haiwezekani akajipiga risasi kidevuni ikanasa kwenye ubongo, halafu akajipiga tena kidevuni upande wa kushoto… imetushangaza na hatuelewi tukio hili,” alisema Mushi.


Alisema wanafahamu fika maisha aliyoishi kijana wao kwani alikuwa ni mtaratibu, hivyo maamuzi aliyoyachukua yalikuwa magumu.

“Kijana wetu enzi za uhai wake alikuwa ni mtaratibu, hivyo maamuzi aliyoyachukua yalikuwa ni magumu mno na mwenye siri hiyo ni mzazi mwenzake Ufoo, tuna imani ataeleza,” alisema Mushi.

Alisema chanzo cha mauaji hayo ilidaiwa kuwa ni kutokana na kutoelewana kati ya Ufoo na mzazi mwenzake huyo, ambapo walipokwenda kwa mzazi wake Ufoo nako walishindwa kupata suluhu.

Hata hivyo wakati wa kuaga mwili wa marehemu Anthery Mushi, jana vilio na simanzi vilitawala katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Anthery, alijiua kwa kujipiga na risasi baada ya kutokea kutoelewana kati yake na mzazi mwenzake ambaye ni mwandishi wa habari wa ITV/Radio One, Ufoo Saro.

Mbali na kujiua, Mushi pia alimuua kwa kumpiga risasi tano mama mkwe wake, Anastazia Saro (56), huku akimjeruhi kwa risasi mbili tumboni na begani Ufoo ambaye anaendelea kupata matibabu katika wodi ya wagonjwa wa Moyo Muhimbili kwa uangalizi maalumu.

Wakati huo huo, Happy Mushi ambaye ni mdogo wa marehemu, alisema kwa mara ya mwisho waliwasiliana na ndugu yao Oktoba 9, mwaka huu.

Alisema marehemu Mushi alimwambia kaka yake kuwa, anashukuru Mungu amefanyakazi katika mazingira magumu lakini muda si mrefu atarejea nchini na ana imani maisha yake yatabadilika.

Happy aliongeza kuwa, wao kama familia bado wamezingirwa na giza kuhusiana na kifo cha ndugu yao kutokana na mazingira halisi ya tukio hilo.

Alisema katika mazingira ya kawaida, haiwezekani mtu akajipiga risasi mbili ambazo wataalamu wamezibaini jambo ambalo linawafanya wao kama familia washindwe kuamini kifo cha ndugu yao huyo.

Pia alisema taarifa za ndugu yao kujiua wamezipata kupitia vyombo vya habari na pia hawana taarifa zozote za ugomvi kati ya Ufoo na mzazi mwenzake, kwani hata Desemba mwaka jana walikuwa pamoja katika sherehe za kifamilia zilizofanyika mkoani Kilimanjaro.

“Sisi kama familia bado tunapata ugumu kuhusiana na kifo cha ndugu yetu, tunaomba Jeshi la Polisi lichunguze kwa kina haiwezekani ndugu yetu akajipiga risasi mbili yeye mwenyewe,” alisema Happy.

Imedaiwa kuwa hadi Mushi anajiua mkataba wake wa kazi ulikuwa bado unaendelea nchini Sudan. 

Maiti ya Mushi imesafirishwa jana kwenda kijijini kwao Uru Ongoma Timbirini Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, ambapo misa itafanyika nyumbani kwao hapo leo na baadaye mazishi yatafanyika kijijini hapo.

Marehemu Mushi alizaliwa mwaka 1973 na kupata elimu ya msingi mwaka 1981 hadi 1987 katika Shule ya Msingi Ongoma, mwaka 1988 alijiunga na elimu ya Sekondari Visiwani Zanzibar hadi 1991, baada ya hapo alijiunga na Chuo cha Uandishi wa Habari.

Mwaka 1994, alijunga na kituo cha Utangazaji cha ITV, mwaka 2002 alijiunga na Mahakama ya Kimataifa mjini Arusha ya ICTR na mwaka huo huo akajiunga na Shirika la Umoja wa Mataifa (UN), Sudan akiwa mtaalamu wa mambo ya mawasiliano.

Pia, maiti ya mama yake Ufoo, Anastazia Saro imezikwa kijijini kwao Shari Machame Wilaya ya Hai Kilimanjaro.

Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Eligaesh, alisema hali ya Ufoo inaendelea kuimarika na hivi sasa ameanza kufanya mazoezi.

“Ufoo hali yake inaimarika vyema na ameanza mazoezi isipokuwa daktari wake ameshauri asionane na watu hadi hapo atakapotoa maamuzi daktari huyo,” alisema Aligaesha.

Tukio hilo la Ufoo kupigwa risasi lilitokea Oktoba 13, mwaka huu, Kibamba CCM jijini Dar es Salaam.
MTANZANIA

No comments: