ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 31, 2013

Majambazi yatikisa

Yapora mamilioni ya fedha yakihamishwa kutoka benki kwenda nyingine
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro,Robert Boaz

Tukio la kushtua na kushangaza la uporaji wa Sh. milioni 220 limefanyika mjini Moshi baada ya watu wanaodaiwa kuwa majambazi kuvamia gari na kumteka Mkurugenzi wa Fedha wa Kampuni ya Ujenzi ya Dott, Shuresh Bab (45), kisha kuondoka na kitita hicho.

Katika tukio hilo lililotokea jana asubuhi na kuacha maswali mengi ambayo hata Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, hana majibu yake, ni uamuzi wa kampuni hiyo kuhamisha kwa gari lisilo na aina yoyote ya ulinzi kiasi hicho cha fedha kutoka benki ya Standard Charted tawi la Moshi ili kuzipeleka benki ya NMB tawi la Mandela.

Waporaji hao wanaodaiwa kuwa wawili wanaelezwa kuwa walijihami kwa silaha za moto, lakini katika uporaji wote hadi kufanikiwa kuondoka na fedha hizo, hakuna hata risasi moja ilifyatuliwa wakati wa utekaji eneo la makutano ya barabara ya Arusha na Old Boma mjini hapa.

Kampuni Dott ilipewa zabuni ya ujenzi wa barabara ya Same-Mkumbara mkoani Kilimanjaro kwa kiwango cha lami.
Majambazi hayo yakiwa kwenye pikipiki wanadaiwa kuteka gari lililokuwa limechukua fedha hizo.

Habari zinasema kuwa majambazi hayo yalifanikiwa kupora kiasi hicho cha fedha baada ya kuteka gari la Bab, lakini alifanikiwa kuwazidi nguvu na kuruka kutoka katika gari hilo na kukimbia kuelekea barabara kuu inayopita mkabala na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na kutoa taarifa.

Haikufyatuliwa risasi hata moja wakati akifurukuta kuwatoroka na kukikimbia.

Baada ya kutoa taarifa, polisi walifika eneo la tukio na kulikuta gari alilokuwa mkurugenzi huyo likiwa limetelekezwa katika Mto Karanga ndani yake kukiwa na wafanyakazi wa kampuni ya ujenzi ya Dott waliokuwa wametekwa pamoja na mkurugenzi wao.Wafanyakazi hao walikuwa salama, hakuna aliyejeruhiwa.

Kamanda Boaz alisema polisi walifanikiwa kuokoa zaidi ya Sh. milioni 80 kati ya Sh. 220,000,000 zilizoporwa. Kiasi cha Sh. milioni milioni 140 zinasadikiwa kuwa majambazi wamefanikiwa kuondoka nazo.

Akisimulia tukio hilo, Kamanda Boaz alifafanua kuwa mkurugenzi na wafanyakazi wa kampuni ya Dott walitekwa na kuporwa fedha hizo wakiwa njiani kuelekea katika benki ya NMB tawi la Mandela wakiwa katika gari aina ya Toyota Hilux Double Cabin yenye namba za usajili T 864 AZM.

Alisema wakiwa njiani kuelekea katika benki hiyo, ghafla ilipita pikipiki ikiwa na watu wawili na kusimama mbele na kumwamuru dereva wa gari hilo, Wenslaus Mambo (32), asimame na baadaye wakamwamuru abadili mwelekeo.

Kufuatia tukio hilo, watu wawili wanashikiliwa na uchunguzi wa Sh. milioni 140 ambazo hazijapatikana unaendelea kufanyika.

Kamanda huyo alipoulizwa sababu za mkurugenzi huyo kuchukua kiasi kikubwa cha fedha taslimu benki kinyume cha sheria ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inayoelekeza kwamba malipo yoyote yanayozidi Sh. milioni 10 ni lazima yafanyike kwa njia ya uhamishwaji fedha kwa njia ya benki (interbank money transfer), alisema kuwa wanaendelea na uchunguzi.

Pia alipoulizwa sababu za kutokukamatwa mkurugenzi huyo kwa kukiuka sheria hiyo, alisisitiza kuwa wanaendelea na uchunguzi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: