ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 29, 2013

MALINZI NDYE RAIS MPYA TFF, ATOA MSAMAHA

By Israel Saria on October 28, 2013


Jamal Emil Malinzi ndiye Rais mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Malinzi ameshinda wadhifa huo katika uchaguzi wa Kamati ya Utendaji ya TFF uliofanyika juzi (Oktoba 27 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

Aliibuka na ushindi wa kura 73 dhidi ya mpinzani wake pekee Athuman Jumanne Nyamlani aliyepata kura 52. Nafasi ya Makamu wa Rais imetwaliwa na Wallace Peter Karia aliyepata kura 67 na kuwashinda Ramadhan Omari Nassib kura 52 huku Imani Omari Madega akipata kura sita.

Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa, Rais Malinzi ametaka ushirikiano kutoka kwa wadau wote akiwemo mpinzani wake Nyamlani katika kuhakikisha mpira wa miguu nchini unasonga mbele.

Pia ametoa msamaha kwa watu wote waliokuwa wamefungiwa kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na TFF. Msamaha huo hauwahusu wale waliofungiwa kwa makosa ya rushwa au kupanga matokeo. Vilevile msamaha huo hauhusu adhabu zilizotolewa katika ngazi ya klabu.

Rais Malinzi pia amevunja kamati zote za TFF ambapo ataziunda upya kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji.
Kwa upande wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji walioshinda ni Kalilo Samson (Kanda namba 1- Geita na Kagera) aliyepata kura 102 za ndiyo na 17 za hapana. Kanda namba 2- Mara na Mwanza, mshindi ni Vedastus Lufano aliyepata kura 51 dhidi ya Jumbe Odessa Magati (11), Mugisha Galibona (24), na Samwel Nyalla (39).

Epaphra Swai ndiye mshindi wa Kanda namba 3- Shinyanga na Simiyu kwa kura 63 dhidi ya Mbasha Matutu aliyepata 61. Kanda namba 4- Arusha na Manyara mshindi ni Omali Walii Ali aliyepata kura 53 dhidi Elley Mbise (51), Ally Mtumwa (19).

Kanda namba 4- Kigoma na Tabora, mshindi ni Ahmed Idd Mgoyi aliyepata kura 92 dhidi ya 28 za Hamisi Yusuf Kitumbo.

Ayubu Nyaulingo na Blassy Mghube Kiondo ameshinda Kanda namba 6- Katavi na Rukwa kwa kura 73 dhidi ya Ayubu Nyaulingo aliyepata 52. Ayoub Shaibu Nyenzi ndiye mshindi wa Kanda namba 7- Iringa na Mbeya kwa kupata kura 59 na kuwapiku David Samson Lugenge (8), John Exavery Kiteve (12) na Lusekelo Elias Mwanjala (46).

Kanda namba 8- Njombe na Ruvuma inawakilishwa na James Patrick Mhagama aliyepata kura 93 dhidi ya 31 za Kapteni mstaafu Stanley William Lugenge. Athuman Kingombe Kambi ndiye mshindi wa Kanda namba 9- Lindi na Mtwara kwa kura 84 akiwazidi Francis Kumba Ndulane (30) na Zafarani Mzee Damoder (11).

Hussein Zuberi Mwamba ametetea ujumbe wa Kanda namba 10- Dodoma na Singida kwa kura 63 akiwapiku Stewart Masima (58) na Charles Komba (4). Geofrey Irick Nyange ameshinda Kanda namba 11- Morogoro na Pwani akipata kura 78 dhidi ya Juma Pinto (26), Farid Nahdi (14), Riziki Juma Majala (5) na Twahil Twaha Njoki (2).

Kanda namba 12- Kilimanjaro na Pwani, Khalid Abdallah Mohamed ndiye aliyeibuka kidedea kwa kura 69 dhidi ya 54 za mpinzani wake Davis Elisa Mosha. Kidao Wilfred Mzigama ameshinda Kanda namba 13- Dar es Salaam kwa kupata kura 60 dhidi ya wapinzani wake Muhsin Said Balhabou (50), Omar Isack Abdulkadir (10) na Alex Crispine Kamuzelya (4).

KIM AITA 30 FUTURE YOUNG TAIFA STARS
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ametaja kikosi cha wachezaji 30 wa timu ya pili (Future Young Taifa Stars) kitakachoingia kambini Novemba 9 mwaka huu ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Chalenji.

Kipa Ivo Mapunda wa Gor Mahia ya Kenya ni miongoni mwa wachezaji walioitwa na Kim kwenye kikosi hicho ambacho hukitumia kuangalia uwezo wa wachezaji kabla ya kuwajumuisha kwenye timu ya wakubwa.

Kikosi hicho kamili ambacho Novemba 13 kitacheza mechi ya kirafiki na Taifa Stars kinaundwa na; makipa Aishi Manula (Azam), Hussein Shariff (Mtibwa Sugar) na Ivo Mapunda (Gor Mahia, Kenya).

Mabeki ni David Luhende (Yanga), Hassan Mwasapili (Mbeya City), Himid Mao (Azam), Issa Rashid (Simba), Ismail Gambo (Azam), John Kabanda (Mbeya City), Kessy Khamis (Mtibwa Sugar), Michael Pius (Ruvu Shooting), Miraji Adam (Simba), Mohamed Hussein (Kagera Sugar), Said Moradi (Azam) na Waziri Salum (Azam).

Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Farid Mussa (Azam), Haruni Chanongo (Simba), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Jonas Mkude (Simba), Khamis Mcha (Azam), Ramadhan Singano (Simba), Simon Msuva (Yanga), William Lucian (Simba).

Washambuliaji ni Elias Maguli (Ruvu Shooting), Hussein Javu (Yanga), Joseph Kimwaga (Azam), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar), Mwagane Yeya (Mbeya City) na Paul Nonga (Mbeya City).

Kim amesema kikosi cha Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager chenyewe kitaingia kambini Novemba 12 jijini Dar es Salaam ambapo siku inayofuata ndipo kitakapocheza mechi na Future Young Taifa Stars.

Baada ya mechi hiyo, kambi ya Future Young Taifa Stars itavunjwa wakati Taifa Stars itaondoka Novemba 14 mwaka huu kwenda Arusha ambapo itaweka kambi na kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa kabla ya kwenda Nairobi, Kenya kwenye michuano ya Kombe la Chalenji itakayofanyika kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 12 mwaka huu.

Wachezaji 16 wa kikosi cha Taifa Stars kitakachoingia kambini Novemba 12 mwaka huu kinaundwa na Ally Mustafa (Yanga), Mwadini Ali (Azam), Aggrey Morris (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (AC Cannes, Ufaransa) na Nadir Haroub (Yanga).

Erasto Nyoni (Azam), Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar), Salum Abubakar (Azam), Mwinyi Kazimoto (Markhiya, Qatar), Frank Domayo (Yanga), Athuman Idd (Yanga), Mrisho Ngasa (Yanga), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC), Mbwana Samata (TP Mazembe, DRC) na John Bocco (Azam).

Wachezaji wengine kumi kutoka Future Young Taifa Stars baadaye wataongezwa katika kikosi kitakachounda timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) kwa ajili ya michuano ya Kombe la Chalenji.

PAMBANO LA THE TANZANITE LAINGIZA MIL 6/-
Pambano kati ya timu ya Taifa ya wanawake kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Tanzania (The Tanzanite) dhidi ya Msumbiji lililochezwa juzi (Oktoba 26 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 6,190,000.

Washabiki waliohudhuria mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika iliyomalizika kwa The Tanzanite kuibuka na ushindi wa mabao 10-0 walikuwa 5,003. Viingilio vilikuwa sh. 1,000, sh. 2,000, sh. 5,000 na sh. 10,000.

Mgawo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 944,237.29, gharama za kuchapa tiketi sh. 2,247,900, gharama za mchezo sh. 599,573 wakati wamiliki wa uwanja walipata sh. 449,679.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) lilipata sh. 149,893 huku Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) likipata sh. 1,798,718.

Mechi ya marudiano kati ya The Tanzanite na Msumbiji itachezwa kati ya Novemba 8 na 10 mwaka huu.

YANGA, MGAMBO KUUMANA UWANJA WA TAIFA VPL
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inakamilisha raundi ya kumi na moja kesho (Oktoba 29 mwaka huu) kwa mechi tatu huku Yanga ikiwa mwenyeji wa Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mbeya City na Tanzania Prisons. Rhino Rangers na JKT Ruvu zitacheza katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Raundi ya 12 ya ligi hiyo itaanza Oktoba 31 mwaka huu kwa mechi kati ya Simba na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Novemba Mosi mwaka huu kutakuwa na mechi kati ya Yanga na JKT Ruvu kwenye uwanja huo huo.

Novemba 2 mwaka huu kutakuwa na mechi nne; Mgambo Shooting na Coastal Union (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Tanzania Prisons na Oljoro JKT (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Azam na Ruvu Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), na Mtibwa Sugar na Rhino Rangers (Uwanja wa Manungu, Morogoro).

Raundi hiyo itakamilika Novemba 3 mwaka huu kwa mechi moja ambapo Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Ashanti United kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Mechi za kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo zitachezwa Novemba 6 na 7 mwaka huu. Novemba 6 ni JKT Ruvu vs Coastal Union, Ashani United vs Simba, Kagera Sugar vs Mgambo Shooting, Rhino Rangers vs Tanzania Prisons na Ruvu Shooting vs Mtibwa Sugar.

Novemba 7 mwaka huu, Azam itacheza na Mbeya City wakati Yanga itacheza na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

EL MAAMRY KUONGOZA BODI YA TFF
Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) umemteua Said Hamad El Maamry kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ambayo kazi yake kubwa ni kusimamia mali za shirikisho.

El Maamry ambaye kitaaluma ni mwanasheria na Mwenyekiti wa zamani wa TFF wakati huo ikiwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) ataongoza bodi hiyo yenye jumla ya wajumbe watano.

Wajumbe wengine wa bodi hiyo ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera ambaye anakuwa Makamu Mwenyekiti, Dk. Ramadhan Dau, Mohamed Abdulaziz na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Stephen Mashishanga.

No comments: