ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 31, 2013

Mwalimu akwamisha wanafunzi 11 kufanya mtihani kidato cha nne

Ni kwa kurotoka na ada zao za shule
Philipo Mulugo

Chuo cha Badan kilichopo Tabata jijini Dar es Salaam kimeingia katika kashfa baada ya mwalimu wake mmoja kudaiwa kutoroka na ada ya mtihani wa taifa Sh. 550,00 ya wanafunzi 11 na kusababisha wasifanye mtihani wa taifa wa kidato cha nne unaotarajia kufanyika wiki ijayo.

Kufuatia hali hiyo, wanafunzi hao watalazimika kufanya mtihani huo mwakani kwa kuwa mwaka huu wamekosa namba kwa sababu fedha za ada walizotoa hazijawasilishwa katika Baraza la Taifa la Mitihani (Necta).

Wakizungumza na NIPASHE wanafunzi hao walieleza kusikitishwa na kitendo cha uongozi wa shule hiyo kutowasilisha ada ya mtihani Necta wakati wamelipa Sh. 50,000 kila mmoja pamoja na ada ya shule Sh. 250,000.


Walisema walikwenda kutoa taarifa katika kituo cha Polisi Tabata, lakini suala lao halijapatiwa ufumbuzi.

Mmiliki wa chuo hicho, Nicodemo Abely Baruty, alithibitisha kuwapo kwa tatizo hilo na kwamba limesababishwa na mwalimu (jina lake tunalihifadhi kwa sasa) kudaiwa kukimbia na fedha za ada za wanafunzi hao.

Baruty alisema mwalimu huyo ambaye alitoweka na kwenda kusikojulikana, ameshafunguliwa jalada katika kituo cha Polisi Tabata namba TBT/RB/1758/13 na anaendelea kutafutwa.

Alisema uongozi wa chuo umekubaliana na wanafunzi hao kusubiri hadi mwakani na watarudishiwa nusu ya ada ya shule waliyotoa.

“Tumekubaliana mbele ya Mkuu wa Kituo cha Polisi Tabata kwamba hawa wanafunzi tuwarudishie nusu ya ada na pia mwakani tuwasaidie wafanye mtihani wa taifa na kimsingi wote wamekubali na tumesainiana,” alisema.

Alisema anashangaa hatua ya mwalimu huyo kukusanya ada ya mtihani ya wanafunzi, wakati utaratibu ni kwamba mwanafunzi anatakiwa akajisajili mwenyewe kwenye kituo cha mtihani na pesa za ada anakwenda kulipia mwenyewe Posta.
CHANZO: NIPASHE

No comments: