ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 31, 2013

Mwanamke apigwa risasi akitishia Polisi bastola

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas

Mwanamke mmoja mkazi wa PPF jijini Arusha, amenusurika kifo baada ya kupigwa risasi na polisi kufuatia uamuzi wake wa kuwatishia (polisi) kwa bastola akikaidi maelekezo ya kutoegesha gari lake sehemu isiyoruhusiwa.

Mwanamke huyo, Violet Mathias, alinusurika kufa baada ya kupigwa risasi ya begani na askari polisi aliyekuwa anajihami baada ya kumtishia kwa bastola.

Violet anadaiwa kukaidi agizo la polisi la kutotakiwa kuegesha gari lake karibu na mlango unaotumiwa na magari yanayopeleka na kuchukua fedha katika benki ya CRDB tawi la Mapato jijini hapa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea juzi saa 7:00 mchana eneo la jengo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kusema kuwa Violet, alipigwa risasi baada ya kukaidi amri ya polisi ya kutakiwa kuondoa gari eneo lisiloruhusiwa kuegesha magari.

Kamanda Sabas alidai mteja huyo alifika eneo la jengo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuingia ndani ya benki hiyo, lakini kabla ya tukio aliamriwa na polisi kutafuta eneo lingine la kuegesha gari lake, lakini alikaidi maelekezo hayo, badala yake aliwaangalia tu na kuingia ndani.

Kutokana na hali hiyo, Kamanda alidai kuwa polisi waliamua kutoa upepo matairi ya gari lake na baada ya dakika chache, alipotoka benki na kukuta gari lake likiwa limeondolewa upepo, alipandwa na hasira na kumfuata mmoja wa askari polisi aliyekuwa kwenye lindo na kumtolea maneno ya kujeli.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, Violet alimwambia askari huyo kuwa hata kama ana silaha na yeye anayo.

Alidai kuwa baada ya kutamka maneno hayo, mwanamke huyo aliitoa bastola na kutaka kumpiga risasi askari huyo, lakini naye askari alimuwahi na kumpiga risasi kwenye bega la kushoto na kuanguka chini.

“Tunaomba kila mtu atii sheria bila shuruti na tukio hili ni matokeo ya ukiukwaji wa sheria. Alimtishia bastola askari wetu, naye askari aliweza kumdhibiti,” alisema.

Kamanda Sabas alisema baada ya tukio hilo, Violet alikimbizwa katika Hospitali ya Mount Meru, kwa ajili ya matibabu.

Hata hivyo, Sabas alisema kutokana na sababu ambazo hazikufahamika, baadaye waliamua kumkimbizia katika Hospitali ya Selian.
CHANZO: NIPASHE

No comments: