Spika wa Bunge, Anne Makinda akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjni Arusha jana. Kushoto ni Mkurugenzi wa Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa wa Bunge, Jossey Mwakasyuka. Na Mpigapicha Wetu
Spika wa Bunge, Anne Makinda, amekuwa makini au pengine ‘kukwepa’ kueleza iwapo atagombea kuwa mwenyekiti wa Bunge la Katiba, lakini amesema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba itakapokamilika itaelekeza namna uendeshaji wa bunge hilo utakavyokuwa.
Mwandishi wa NIPASHE alitaka kujua utaratibu uliowekwa kuongoza vikao vya Bunge la Katiba na kama yeye (Spika) angeweza kugombea kuwa mwenyekiti wa bunge hilo.
Akijibu Spika Makinda hakueleza iwapo atagombea au la, lakini alisema suala hilo ni la kisheria na itakapokamilika itaelekeza namna uongozi wa bunge hilo utakavyokuwa.
“Tutasimama katika sheria, sheria ni upanga, itakapokamilika nafasi zitatangazwa na wajumbe wanaotaka watagombea,” alisema.
Hata hivyo, Spika Makinda aliwataka wanahabari kuwa wazalendo zaidi na kuacha ushabiki katika kipindi hiki cha mchakato wa kutunga katiba mpya.
“Tuwe wazalendo zaidi…kutunga katiba tunaweza, tubishane kwa busara na kujenga hoja katika mijadala, tusiangalie nitakuwa nani baadaye, bali tuangalie maslahi ya taifa,” alisema.
Mapema Spika Makinda alikuwa akizungumzia kuhusu Mkutano Mkuu wa 34 wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambao unafanyika jijini hapa kuanzia Oktoba 16 hadi 24, mwaka huu.
Alisema jukwaa hilo ambalo lilianzishwa mwaka 1997, limefanikiwa kuongeza idadi ya wanawake kwenye mabunge ya nchi wanachama na katika suala la uangalizi wa chaguzi kwenye nchi wanachama.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa wa Bunge, Jossey Mwakasyuka, alisema baadaye kuwa wajumbe wa bunge hilo ndio watakaomchagua mwenyekiti wao.
Alisema iwapo mwenyekiti atachaguliwa kutoka Tanzania Bara, makamu wake atatoka Tanzania Visiwani au mwenyekiti akitoka Visiwani basi makamu wake atatoka Bara.
Kauli mbiu ya mkutano huo ni “Vigezo vya kuendesha na kutathmini chaguzi kwa nchi za Kusini mwa Afrika.”
Spika Makinda alisema uamuzi wa kuwa na kauli mbiu hiyo umekuja baada ya miaka 13 ya uangalizi wa chaguzi kuu, hivyo kuonekana kuwa kuna umuhimu wa kuvipatia upya vigezo vya kusimamia na kutathmini mwenendo wa chaguzi za nchi wanachama wa SADC.
Wajumbe wapatao 150 wakiongozwa na maspika, wabunge kutoka nchi wanachama wa SADC pamoja na wadau kadhaa kutoka taasisi mbalimbali za kimataifa wanashiriki mkutano huo utakaofunguliwa rasmi Jumapili ijayo na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Billal kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete.
Nchi zinazoshiriki mkutano huo ni Afrika Kusini, Angola, DR Congo, Lesotho, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Shelisheli, Zambia, Zimbabwe na mwenyeji Tanzania, wakati Botswana na Swaziland zimetoa udhuru kwa kuwa ziko kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment