Aidha, Serikali ya Tanzania imeahidi kuilipa China mkopo wadeni la Dola za Marekani milioni 24.6 kwa ajili ya kufufua kiwanda cha nguo cha urafiki.
Mikataba hiyo ilisainiwa jana mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri Mkuu wa China, Li Keqiang baada ya viongozi hao kufanya mazungumzo jijini Beijing, China.
Mikataba hiyo ni Mkataba wa Ushirikiano baina ya Tanzania na China kwenye masuala ya sayansi na teknolojia; mkataba wa kuruhusu bidhaa za baharini ziuzwe China; mkataba wa ushirikiano baina ya Tanzania na China kwenye masuala ya utalii.
Mingine ni makubaliano baina ya Tanzania na China wa kuanzisha ukanda wa kisasa wa viwanda vya nguo pamoja na kukuza zao la pamba na wa mkataba wa kutoa vitalu namba 60 na 61 kwa ajili ya ujenzi wa Ubalozi wa China jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo yao, Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya pili ya ziara ya kikazi yake ya siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo, aliishukuru Serikali ya nchi hiyo kwa misaada mbalimbali ambayo China imekuwa ikiitoa kwa Tanzania.
Alisisitiza uwekezaji kwenye sekta za kilimo, nishati, elimu na miundombinu hasa reli, bandari na teknohama.
Kwenye kilimo, Pinda alikumbusha suala la upatikanani wa soko kwa zao la tumbaku lakini akaomba uwapo umuhimu wa pekee kwa wawekezaji wa viwanda vya kusindika korosho katika mikoa ya kusini.
Alimweleza Waziri Mkuu wa China dhamira ya Serikali ya Tanzania kulipa deni la Dola za marekani milioni 24.6 ambalo lilitolowa kama mkopo kwa ajili ya kufufua Kiwanda cha Nguo cha Urafiki.
Leo Waziri Mkuu atafungua mafunzo ya siku 10 kwa maofisa 20 kutoka idara na taasisi za serikali za hapa nchini yanayoendeshwa kwa pamoja baina ya Chuo cha Uongozi cha China na Taasisi ya Uongozi ya Tanzania.
Pia atatembelea Kiwanda cha Aluminium hapa Beijing, atakutana Bodi ya Tumbaku, kampuni za umeme za China Power Investment (CPI) na State Grid Corporation na baadaye atakutana na Watanzania wanaoishi hapa Beijing kwenye Ubalozi wa Tanzania nchini China.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment