Wabunge waanza kupigwa msasa
Ni wajumbe wa kamati sita
Mafunzo hayo yalianza kutolewa jana kwa kundi la kwanza la wabunge, ambao ni wajumbe wa kamati sita za kudumu za Bunge, katika Ofisi Ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam, na wataalamu kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Mafunzo hayo yanatolewa kupitia semina maalumu iliyoandaliwa na Bunge kupitia Mradi wake wa Kuwajengea Uwezo wa Wabunge (LSP) kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
Wabunge walioanza kupewa mafunzo hayo ni wajumbe wa kamati za kudumu za Bunge za Kilimo, Mifugo na Maji; Katiba, Sheria na Utawala; Fedha na Uchumi; Huduma za Jamii; Mambo ya Nje na Miundombinu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Pindi Chana, aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa, semina hiyo inalenga kuwajengea wabunge uwezo wa kuelewa namna ya kuichambua Rasimu ya Katiba, na kwamba itafanyika kwa awamu tofauti.
“Semina imeandaliwa ili kutufundisha kuelewa namna ya kuichambua Rasimu ya Katiba ili iwe rahisi kuelewa kwenye Bunge la Katiba. Watu wakishaelewa, uchambuzi unakuwa mzuri,” alisema Chana.
Kamati nyingine za Kudumu za Bunge, ambazo wajumbe wake wanatarajiwa kupewa pia mafunzo kupitia semina hiyo, ni ya Uongozi; Kanuni za Bunge; Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na ya Masuala ya Ukimwi.
Nyingine ni Sheria Ndogo; Viwanda na Biashara; Ulinzi na Usalama; Maendeleo ya Jamii; Ardhi, Maliasili na Mazingira; Hesabu za Serikali na Hesabu za Serikali za Mitaa.
Chana alisema kutokana na hatua ya mchakato wa mabadiliko ya Katiba iliyofikiwa, wananchi wenye maoni wayapeleke kwa wawakilishi wao (wabunge), ambao nao wataziwasilisha katika Bunge Maalumu la Katiba.
Aidha, alisema baada ya Bunge hilo itaitishwa kura ya maoni ambayo inaweza kupigwa mara mbili iwapo zaidi ya asilimia 50 ya wananchi wa Tanzania Bara na asilimia 50 ya wananchi wa Zanzibar zinazotakiwa, hazitafikiana katika kuipitisha Rasimu ya Katiba.
Pia alisema iwapo mara zote mbili, kiwango hicho cha asilimia hakitafika, kuna haki ya kuitisha tena Bunge Maalumu la Katiba kwa ajili ya kuijadili upya Rasimu ya Katiba kabla ya kuirudisha kwa wananchi ili kupigiwa kura ya maoni.
Maandalizi ya Bunge hilo yanafanyika wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikiendelea na kazi ya kuchambua maoni ya mabaraza ya katiba ya wilaya, asasi mbalimbali na makundi maalumu.
Tume hiyo inayoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, yenye wajumbe 30; wakiwamo 15 kutoka Tanzania Bara na 15 kutoka Zanzibar, ilitangazwa na Rais Jakaya Kikwete, Aprili 6 na kuapishwa Aprili 13, mwaka jana.
Ilianza kazi ya kukusanya maoni ya wananchi Mei mosi, mwaka jana.
Baada ya kukamilisha kazi hiyo, iliyachambua na kuandika Rasimu ya Katiba.
Kazi ya kukusanya maoni hayo iliwahusisha wananchi mmoja mmoja kupitia mikutano ya hadhara na ilikamilishwa na Tume Desemba, mwaka jana.
Baadaye Tume ilikutana na makundi maalumu na watu mashuhuri, wakiwamo viongozi wakuu wastaafu na waliopo madarakani, kati ya 7-28, mwaka huu.
Bunge hilo ambalo litachukua siku 70 litaundwa na wajumbe takribani 600 wakiwamo Wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na wajumbe kutoka makundi mbalimbali ya kijamii 166.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment