ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 12, 2013

Awalipua Spika Makinda, Ndugai

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Deo Filikunjombe

Bagamoyo. Siku chache baada ya kumalizika kwa Mkutano wa 13 wa Bunge, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Deo Filikunjombe amesema kamati yake inashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo kutokana na kubanwa na Ofisi ya Spika.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamisi Kigangwala kuongoza harakati za kumng’oa Spika wa Bunge Anne Makinda kwa madai kuwa anaongoza Bunge kwa upendeleo na hasa kwenye uendeshaji wa kamati. Alikusanya saini za wabunge wapatao 30 ili waunge mkono hoja yake, ambayo kwa sasa inashughulikiwa na Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.
Filikunjombe ambaye pia ni Mbunge wa Ludewa (CCM), alisema hayo jana wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Wajumbe wa PAC na Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC), yaliyohudhuriwa pia na Ndugai pamoja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh.

Alisema mara nyingi kamati hiyo inapozihoji idara mbalimbali, Spika Makinda au Naibu wake, Job Ndugai wamekuwa wakiwapigia simu na kuwataka kutoruhusu vyombo vya habari kusikiliza majadiliano hayo, kitendo alichosema kuwa kinazorotesha uwajibikaji.

“Mara nyingi tumekuwa tukipokea simu kutoka kwao zinazolalamikia utendaji wa kamati hii,” alisema na kuongeza: “Hatua hiyo inatokana na kamati (PAC) kuwa na tabia ya kuruhusu vyombo vya habari kuingia katika vikao vyetu wakati tunapokuwa tunahoji watendaji wa idara mbalimbali. Wamekuwa wakitupigia simu na kututaka tusifanye hivyo.”

Ndugai alisema kanuni za Bunge zinaruhusu vyombo vya habari kushiriki katika vikao vya kamati za Bunge lakini wanaandaa utaratibu wa ushiriki wao.

“Kuanzia sasa tunajaribu kuangalia namna ya kuweka utaratibu ili kuvisaidia vyombo vya habari kupata taarifa za matumizi ya fedha za umma bila ya kuathiri utendaji wa kamati,” alisema.

Filikunjombe alipendekeza kubadilishwa kwa kanuni ili vikao vya PAC na LAAC virushwe moja kwa moja katika televisheni kama ilivyo mikutano ya Bunge ili kama kuna mtu anasema uongo wananchi wamwone.

Alisema hali hiyo itasaidia watendaji kuongeza uwajibikaji na uwazi katika matumizi ya fedha za umma… “Inashangaza… maana tukiwaita watendaji kujieleza mbele ya kamati juu ya matumizi ya fedha tunapigiwa simu na Spika Makinda au Naibu wake, hii inaondoa dhana nzima ya uwajibikaji,” alisema.

Alisisitiza kuwa idara hizo huwa zinaomba fedha za umma bila kificho kwa nia ya kuzitumia kwa mambo ya msingi lakini ameshangazwa na hofu ya viongozi kuhojiwa wakati vyombo vya habari vikiwapo.

Alisema umefika wakati kwa Ofisi ya Spika kuziamini kamati na kuziacha zifanye kazi zake kwa umakini ili kuwa na uwajibikaji.

“Ni vizuri kamati hizi mbili zikaachwa zifanye kazi zake kwa sababu zina umuhimu mkubwa katika usimamizi wa fedha za umma,” alisema Filikunjombe.

CAG aililia POAC
Kwa upande wake, Utouh alisema kuna haja ya Spika Makinda kuunda kamati nyingine ili ifanye kazi ya kukagua mashirika ya umma.

Bunge lilifanya mabadiliko ya muundo wa kamati zake mwaka huu na PAC iliongezewa kazi ya kukagua hesabu za mashirika ya umma baada ya kuvunjwa kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC).

“Kamati ya POAC ilikuwa na umuhimu wake. Umefika wakati Bunge likaona umuhimu wa kazi zilizokuwa zikifanywa na kamati hiyo ya kukagua mashirikia badala ya kuiachia PAC mzigo mkubwa,” alisema Utouh

Mwenyekiti wa LAAC, Rajab Mbaruku Mohamed alisema katika kipindi cha miaka miwili, Ofisi ya Bunge imeshindwa kuwapa fedha za kuwawezesha kukagua miradi ya maendeleo.
“Kamati zimechoka kuwa washauri, sasa tunataka kupewa meno ili tuweze hata kufuatana na polisi tunapokwenda kufanya ukaguzi,” alisema.

Mwananchi

No comments: