ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, November 3, 2013

Brandts aihofu Mbeya City

Kocha wa mabingwa wa ligi kuu ya Bara, Yanga, Ernest Brandts.

Kocha wa mabingwa wa ligi kuu ya Bara, Yanga, Ernest Brandts, amesema ana hofu ya kutibuliwa harakati za kutetea taji hilo na timu ya Mbeya City.

Brandts alisema lengo la Yanga siku zote ni kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi kuu kwa mwaka mzima lakini City ina nafasi kubwa ya kuongoza kutokana na soka la jihadi inalocheza.

"(City) Hawajapoteza mchezo wowote hivyo wana uhakika wa kupata pointi katika kila mchezo," alisema Brandts katika mazungumzo kwa njia ya simu na Nipashe jana.

"Ukiangalia wana mchezo mmoja mgumu dhidi ya Azam na wanaweza kufanya lolote.

"Wao na Azam wanaweza wakatuharibia mipango yetu."

Aidha, Brandts alisema Yanga imepanga kumaliza mzunguko wa kwanza ikiwa kileleni ili kusaidia timu yake kuanza kwa kasi mzunguko wa pili Februari mwakani.

"Muda wote nilikuwa nimepanga kuhakikisha tunamaliza mzunguko huu tukiwa juu ya timu zote na hili linaelekea kutimia japo Mbeya City na hata Azam wana nafasi kama yetu," alisema Brandts.

Brandts alisema anatabiri mchezo kati ya Azam na City utakuwa mgumu na ndiyo utakaotoa picha ya timu gani kati ya hizo tatu itamaliza mzunguko wa kwanza ikiwa kileleni.

Wakati Azam itamaliza mzunguko wa kwanza wa ligi kuu nyumbani Azam Complex dhidi ya Mbeya City, Yanga itacheza na JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Taifa.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: